Meneja Mkuu wa WETCU 2018 Ltd Samwel Jokeya (wa kwanza kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya WETCU 2018 Ltd Hamza Rajabu Kitunga ( kushoto) wakikabidhi mchango wa vifaa vya ukarabati wa hosteli ya wanafunzi kwa Mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondari Mibono Gaston Beno juzi.
………………………………………….
Na Lucas Raphael,Tabora
CHAMA Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Mkoani Tabora (WETCU) kimeunga mkono juhudi za serikali za kuboresha sekta ya elimu kwa kuchangia vifaa vyenye thamani ya sh 708,000 ili kukarabati hosteli ya wanafunzi katika shule ya sekondari Mibono wilayani Sikonge.
Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo Meneja Mkuu wa WETCU 2018 Ltd Samweli Jokeya alisema wametoa msaada huo ili kusaidia ukarabati wa hosteli hiyo ili wanafunzi waishi katika mazingira mazuri na kusoma kwa bidii zaidi.
Alisema mazingira ya kujifunzia yakiwa bora utoro utapungua na ufaulu utaongezeka, hivyo lengo la kutoa vifaa hivyo ni kuifanya hosteli hiyo kuwa bora ili kila mwanafunzi atamani kukaa karibu zaidi na mazingira ya shule.
‘Hosteli hii ilikuwa imechakaa sana, ndiyo maana tumeamua kutoa msaada wa nyavu za matundu madogo na makubwa zenye urefu wa zaidi ya mita 100 ili kuyafanyia ukarabati madirisha yote’, alisema.
Alibainisha kuwa vifaa hivyo vyenye thamani ya sh 708,000 vitasaidia kuimarisha ulinzi na usalama kwa mali za wanafunzi, kuwakinga na mbu ili wasipate malaria na kuboresha mazingira yao ya kuishi ili wasome vizuri.
Jokeya alifafanua kuwa mchango huo ni utekelezaji wa kanuni ya ushirika na.7 inayowataka kuchangia huduma za kijamii, hivyo akatoa wito kwa wadau wengine kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ili kuharakisha maendeleo ya jamii.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Gaston Beno Lukwene alishukuru WETCU kwa moyo wao wa kizalendo na kujali maendeleo ya shule hiyo, hosteli hiyo ni muhimu sana kwa kuwa inasaidia watoto kutoishi mbali na mazingira ya shule.
Alibainisha kuwa licha ya kuomba msaada kwa wadau mbalimbali lakini WETCU ndiyo wameguswa na kuwasaidia. ‘Tunawashukuru sana, tunaomba Mwenyezi Mungu awazidishie mafanikio makubwa katika shughuli zenu’, alisema.
Aliongeza kuwa msaada huo umekuja wakati mwafaka kwani mazingira ya hosteli hiyo yalikuwa siyo rafiki tena kwa watoto na baadhi ya wazazi walikuwa wameondoa watoto wao na kuamua kuishi nao nyumbani.
Diwani wa kata hiyo ya Kipanga Yuda William alisema kukarabatiwa kwa hosteli hiyo kutasaidia watoto wengi kuishi karibu na shule na kupata msaada wa walimu kwa karibu zaidi, hivyo kuongeza kiwango cha ufaulu katika masomo yao.