Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewahimiza wafanyabiashara wote ambao wamesajiliwa katika Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutumia mfumo mpya wa kielektroniki wa VAT unaojulikana kwa jina la e-VAT wenye lengo la kumrahisishia mlipakodi kuwasilisha ritani na kukokotoa kodi stahiki.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Bw. Richard Kayombo amesema kuwa, mfumo huo umeanza kutumika rasmi mwezi huu wa Aprili, 2022 ambapo walipakodi wanatakiwa kuutumia kuwasilisha ritani zao za VAT za mwezi Machi na mwisho wa kuwasilisha ritani hizo ni tarehe 20 Aprili, 2022.
Kwa mlipakodi ambaye hajawasilisha ritani ya VAT kwa mwezi Februari 2022 kurudi nyuma, anatakiwa kuwasilisha ritani hiyo kwa kutumia mfumo wa zamani.
“Wito wetu kama Mamlaka ya Mapato Tanzania, ni kuwaomba wahusika kwa maana ya wale wote waliosajiliwa katika Kodi ya Ongezeko la Thamani kuwahi kuwasilisha ritani zao kwa wakati, tukitambua kwamba, mwezi huu wa nne ni mwezi wenye sikukuu nyingi ikiwemo sikukuu ya pasaka hivyo tusingependa walipakodi wetu wapate usumbufu siku za mwisho za kuwasilisha ritani,” alisema Bw. Kayombo.
Mkurugenzi Kayombo ameongeza kuwa, TRA imejipanga vizuri kuwahudumia walipakodi wa VAT nchi nzima kwa kuweka watalaam kila mkoa na wilaya ambao wana wajibu wa kuwasaidia walipakodi kutatua changamoto mbalimbali wakati wa kujaza na kuwasilisha ritani za VAT kwa kutumia mfumo huo.
“Tumeweza na tunaendelea kuwaelimisha walipakodi waliosajiliwa katika Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kuhakikisha wanautumia mfumo huu vizuri, lakini pia tunao watumishi wetu vinara ambao wapo kila mkoa kwa ajili ya kutatua changamoto zinazoweza kuwakabili walipakodi hao wakati wa kutumia mfumo huu mpya.
Pamoja na kuweka watalaam kila mkoa, kituo chetu cha kuhudumia wateja kitakuwa wazi kuwahudumia walipakodi kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 3 usiku kila siku ili kuhakikisha kwamba, yeyote anayekwama awe kwenye mtandao au amekuja ofisini aweze kuhudumiwa na kuwasilisha ritani yake kwa wakati,” alieleza.
Amewakumbusha walipakodi kuzingatia vigezo vinavyotakiwa kwenye risiti za EFD ili ziweze kukubaliwa kwa ajili ya kudai marejesho ya VAT kwenye manunuzi.
Vigezo hivyo vya risiti za EFD ni pamoja na risiti kuwa na jina la mnunuzi, TIN ya mnunuzi, Namba ya Usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VRN) ya muuzaji, Namba ya Usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mnunuzi, tarehe na namba ya uthibitisho (verification code).
Kwa upande wa Kadhia za Forodha (TANSAD) inatakiwa iwe na TIN sahihi ya muagizaji wa mzigo (importer), tarehe ilipotolewa na kiasi cha VAT kilicholipwa.
Mfumo huu wa e-VAT ni sehemu ya maboresho endelevu yanayoendelea ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ikiwa ni moja ya malengo ya mpango mkakati wake wa tano wa kuleta urahisi, na kuongeza uhiari wa kulipa kodi.
MWISHO.