NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chamwino Mkoani Dodoma, Deo Ndejembi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumaliza changamoto ya kituo cha afya katika Kata ya Itiso iliyopo jimboni kwake.
Ndejembi amesema Rais Samia baada ya kusikia changamoto ya kituo cha afya iliyokua inawakabili wananchi hao wa Itiso alielekeza kiasi cha Sh Milioni 250 kipelekwe kwenye Kata hiyo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.
Naibu Waziri Ndejembi ametoa shukrani hizo kwa Rais Samia wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Ikombo na Itiso alipofanya ziara ya kuwasikiliza wananchi hao na kuwaeleza mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
” Hapa Itiso hapakuwahi kuwa na Kituo cha Afya iliwalazimu msafiri umbali mrefu kwenda Kata nyingine ya Haneti, Mimi niliwaahidi wakati wa Kampeni kuwa tutajenga Kituo cha Afya, Leo namshukuru Mhe Rais Samia nilipobisha hodi akasema akakubali kutupatia Sh Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi huu.
Wananchi wa Itiso hatuna budi kumshukuru Rais Samia ameonesha mapenzi makubwa kwa wananchi wa Chamwino, kwa kutambua umuhimu wa Afya akaelekeza Sh Milioni 250 kutoka kwenye makato ya Tozo zije kujenga Kituo cha Afya hapa kwetu, Tumshukuru sana Rais Samia,” Amesema Ndejembi.
Amesema ndani ya mwaka mmoja pia Rais Samia ametoa kiasi cha Sh Milioni 160 za ujenzi wa Madarasa Nane wakati yeye kama Mbunge amechangia Sh Milioni Nane za ujenzi wa Hosteli katika Shule ya Sekondari Itiso.
Pia Ndejembi ametoa wito kwa wananchi wa Kata hiyo na Jimbo la Chamwino kujitokeza pindi muda utakapofika wa zoezi la Sensa ili kuweza kuisaidia Serikali kujua idadi ya wananchi wake na kupanga mipango yake kulingana na idadi kamili ya watu wake iliyonayo.
” Zoezi la Sensa litafanyika mwaka huu niwaombe wananchi wangu tujitokeze na tutoe ushirikiano wakati wa zoezi hilo, Mimi Mbunge wenu natoa rai kwenu kushiriki zoezi hilo ambalo lina manufaa makubwa kwa Serikali katika kupanga mipango ya kimaendeleo, msiwasikilize watu wanaofanya upotoshaji,” Amesema Ndejembi.