***********************
Adeladius Makwega-BUTIAMA
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema kuwa inashiriki katika maadhinisho ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Mwalimu Julius Nyerere ambapo kilele chake kitakuwa jumatano Aprili 13, 2022 Kijijini Butiama, mkoani Mara.
Akizungumza katika Viwanja vya Mwenge Kijijini Butiama, Boniface Kadili ambaye ni Mratibu wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika inayosimamiwa na Idara ya Maendeleo ya Utamaduni nchini ameyasema hayo kandoni mwa maandalizi hayo.
“Tumejiandaa na banda maalumu la kuonesha kazi mbalimbali za Mwalimu Nyerere zikiwamo vitabu, filamu na yale yanayosemwa na watu kadhaa namna alivyojitoa mhanga katika harakati za ukombozi wa mwafrika.”
Mratibu huyo wa Programu ya Ukombozi alikwenda mbali na kusema kuwa wameanza kuzunguka katika shule za msingi na sekondari Kijijini Butiama kuonesha kazi hizo za Mwalimu Nyerere kwani wanafunzi wengi wa sasa wamezaliwa baada ya Mwalimu Nyerere kufariki dunia.
“Tunaamini kulingana na kazi tulizonazo wanafunzi hawa wa msingi na sekondari wamevutiwa sana kumuona Mwalimu Nyerere katika filamu mbalimbali huku filamu hizo zikiambatana na waliofanya nae kazi kama Brigedia Hashimu Mbita, Samora Machel na wengine wengi.”
Akizungumzia muitikio wa mpango wao huo wa kuzunguka mashuleni Mratibu Kadili alisema bayana kuwa mpango huo unaonesha tija kubwa na wamejiwekea mpango wa kukusanya kazi zaidi na zaidi za maisha ya Mwalimu Nyerere na kuzunguka kuzisambaza kupitia vyombo vya habari na maonesha kadhaa yanapofanyika ili ziweze kufahamika na kila mmoja wetu.
Maandalizi ya maadhimisho ya miaka 100 ya tangu kuzaliwa kwa Mwalimu Julius Nyerere Kijijini Butiama yanaendelea huku mwandishi wa habari hii ameshuhudia mandhari ya Uwanja wa Mwenge Kjijini Butiama ikipambwa na maturubai ya rangi nyeupe yakizunguka uwanja huo mithili ya Yangeyange kwa mtindo wa herufi U.
Kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kuwa siku ya jumatano ambapo viongozi kadhaa watashiriki.