Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma, Mhandisi Jeremia Maduhu akikagua Mradi wa Maji Kwambe.
Fundi Lucas Ngayele akiendelea na kazi ya kuchota kokoto kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji kijiji cha Kwambe wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma.
Muonekano wa Tanki la kuhifadhia maji katika kijiji cha Kwambe wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
*******************************
Na Selemani Msuya, Nyasa
WANANCHI wa Kijiji cha Kwambe wilayani Nyasa mkoani Ruvuma wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA), kuwapatia maji safi na salama baada ya miaka 50 ya kunywa maji yasiyo salama.
Kijiji hicho kimepata maji safi na salama kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 kwa fedha za mkopo usio na riba wa Sh.trilioni 1.3 za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)
Akizungumzia mradi huo Mwanakijiji wa Kwambe, Judith Kayuni mbele ya waandishi wa habari ambao wametembelea mradi huo, amesema kwa zaidi ya miaka 50 wamekuwa wakiteseka kutokana na ukosefu wa maji safi na salama, hivyo uamuzi wa Serikali inayoongozwa na Rais Samia kuwapatia maji hayo ni wa kiukombozi.
“Mimi sasa nina wajukuu, ila watoto wangu karibu wote hawajawahi kuona maji yakitoka bombani hapa kijijini, hivyo uamuzi wa Rais Samia na Serikali yake kuwatuma RUWASA kutuletea maji ya bomba ni wazi kuwa ameleta mapinduzi ya kiuchumi, maendeleo na kijamii,” amesema.
Kayuni amesema mradi huo umewatoa kwenye mateso ya kufuata maji Ziwa Nyasa, visimani na vijiji jirani vya Matenje au Chimate ambapo ni mbali.
Mwanamama huyo amesema ana imani kupitia mradi huo, wananchi watajikita kwenye shughuli za kilimo, uvuvi na biashara, hivyo kuongeza kipato.
“Pia naamini mradi huu ukikamilika ufaulu wa wanafunzi utaongezeka kwa kuwa watapata muda mrefu wa kusoma na sio kutafuta maji,” amesema.
Naye Beatrice Mtonga amesema wanamshukuru Rais Samia kuwapa kipaumbele cha kuwapelekea mradi huo kwani wanaamini watapambana na magonjwa ya kuambukiza.
“Maji ya Ziwa Nyasa yana changamoto nyingi kama watu kuogea au kufa, hivyo sio salama kwa matumizi ya binadamu, hali ambayo imekuwa ikisababisha magonjwa ya mlipuko. Sisi tutamuunga mkono Rais Samia 2025, hili alilofanya halina kifani,” amesema.
Mtonga amesema wao kama wanawake watahakikisha wanaulinda mradi huo kwani una faida nyingi kwao, ili uwe endelevu kwa miaka mingi.
Mariam Yohana amesema mradi huo unaotekelezwa na Ruwasa Ruvuma, unatekeleza kauli mbiu ya kumtua mama ndoo kichwani, hivyo wataulinda kwa nguvu zote.
Yohana ametoa wito kwa RUWASA Nyasa kuwaongezea vituo vya kutolea maji, ili kuweza kukidhi hitaji la wanakijiji wa Kwambe ambao watashuhudia maji bombani baada ya miaka 50 ya kunywa maji ya visimani.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwambe Dickson Nyoni amesema mradi huo wa maji utanufaisha kijiji chao na kuchochea maendeleo.
“Sisi kupitia mradi huu wa RUWASA sina cha kusema kama sio kuhakikisha Rais Samia anashinda uchaguzi 2025, ili aendelee kutuletea miradi mingine,” amesema.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kwambe, Phares Kapinga amesema wao wataulinda mradi huo kwa nguvu zote kuhakikisha mradi huo unakuwa endelevu.
Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyasa, Mhandisi Jeremia Maduhu amesema mradi huo wa fedha za Uviko-19 unagharimu Sh.milioni 500 ambazo zinatumika kujenga banio, vituo 16 vya kuchotea maji, tanki lenye ujazo wa lita laki moja, kuchimba mtaro na kusambaza mabomba yenye urefu wa kilomita 15.3 ambapo kazi zote zipo kwenye hatua za mwisho.
Mhandisi Maduhu amesema mradi huo utanufaisha watu 5,060 ambapo hadi mwishoni mwa mwezi Machi ulikuwa umekamilika kwa asilimia 65 na matarajio yao ni mradi huo kukamilika kwa wakati kama makubaliano yalivyo.
“Mradi huu ni mkombozi wa kiuchumi, kijamii na maendeleo ambapo hadi sasa zaidi ya vijana 20 wa kijiji hiki wamekuwa wakinufaika kwa kufanya kazi na kujiingizia kipato,” amesema.
Maduhu amesema pamoja na kuweka vituo vya kuuzia maji, pia wanatarajia kusambaza maji kwa mwananchi mmoja mmoja iwapo atahitaji kufanyiwa hivyo.
“Hapa Kwambe tangu mwaka 1972 hawajawahi kuwa na maji ya bomba, hivyo uamuzi wa Serikali kufanikisha mradi huu uliangalia uhitaji wa kumtua ndoo mama kichwani,” amesema.
Amesema pia RUWASA Nyasa inatekeleza miradi mingine kama Mradi wa Maji Lituhi unaofikia vijiji saba, Liuli ambao unagharimu Sh. bilioni 4 unahusisha vijiji sita, Likwilu na Linda, Malungu na Tingi ambao unagharimu Sh.bilioni 1 na mingine ambayo imeweza kuajiri zaidi vijana 500.
Maduhu amesema mwaka wa fedha unaokuja 2022/2023 upatikanaji wa maji Nyasa utafikia asilimia 80 kutoka 59 ambayo ilikuwa awali.