Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula amekabidhi vifaa kwaajili ya uchaguzi unaoendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi ikiwemo karatasi, kalamu, mabati 22 yenye thamani ya laki nne na elfu themanini kwa CCM kata ya Kahama, Luninga mbili na ving’amuzi vyake kwaajili ya vijiwe vya Kahawa vya Mwigulu kata ya Pasiansi na Kirumba vyenye thamani ya laki sita na elfu thelathini, Viti hamsini vyenye thamani ya laki nane na elfu themanini na mbili ili kutekeleza shughuli za Chama
Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo Mhe Dkt Angeline Mabula mbali na kumshukuru Rais na Mwenyekiti wa CCM Taifa Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuimarisha Chama sanjari na kusisitiza kwake uchaguzi wa uhuru, haki na amani, akafafanua kuwa ni wajibu wake kama Mbunge kuunga mkono juhudi hizo kwa kusaidia vifaa kwa kuwa si matawi yote au kata zote zenye uwezo wa kugharamia shughuli za uchaguzi
‘… Kama Mbunge ni wajibu wangu kuwezesha matawi, kata au hata wilaya yangu vitendea kazi vya uchaguzi, Na hatutaishia hapa ule utatu wa Serikalini tutarudisha kwenye Chama tutajenga ofisi zetu za matawi na kata wanachama wajenge misingi, nitatoa tofali za ujenzi wa maboma na CCM wilaya kwa ushirikiano tutamalizia ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula amempongeza Rais Samia Kwa kutoa kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 29 kwaajili ya Utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya wilaya hiyo Kwa kipindi Cha mwaka mmoja tangu kuingia kwake madarakani hivyo kuwaasa wanachama na wananchi Kwa ujumla kuzidi kuunga mkono Jitihada hizo
Nae Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilemela Mhe Nelson Meshack amewataka watendaji wa Chama kuvitumia vyema vifaa hivyo Kwa malengo yaliyokusudiwa huku akimshukuru Mbunge wa Jimbo hilo Kwa uamuzi wake kwani vitendea kazi hivyo vimekuja muda muafaka Kwa kuwa hivi karibuni Chama kiliendesha semina ya kuwaongezea maarifa watendaji wake juu ya masuala ya uchaguzi
Aziza Isimbula ni Katibu wa CCM wilaya ya Ilemela amesema kuwa Kila Katibu ana wajibu wa kuwasilisha taarifa ya shughuli za uchaguzi wa ngazi ya chini yake Kwa ngazi ya juu yake Kila siku zoezi linapokwisha hivyo kuja Kwa vifaa hivyo kutasaidia kuharakisha Utekelezaji wa zoezi hilo
Akihitimisha Katibu wa UVCCM kata ya Kahama Cosmas Lutebeka kwa niaba ya wanachama wa kata hiyo wameshukuru Kwa mabati yaliyotolewa na Mbunge huyo kwani yatasaidia kupunguza kero ya muda mrefu ya ukosefu wa Ofisi jambo lililochangia kurudisha nyuma shughuli za ujenzi wa Chama hasa kipindi Cha uchaguzi kinapofika