Na Innocent Kansha – Arusha
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amewataka wamiliki wa malengo ya kimkakati wote ndani ya Mahakama kutekeleza Mpango Mkakati wa awamu ya pili wa mwaka 2020/2021 hadi 2024/25 zilizopo chini yao kikamilifu ili zikamilike kwa muda uliopangwa.
Akiwasilisha taarifa fupi ya mafanikio ya Mpango Mkakati wa awamu ya kwanza wa mwka 2015/16 hadi 2020/2021 kwa wajumbe wa kikao kazi cha mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama awamu ya pili na Mradi wa uboreshaji huduma za Mahakama awamu ya pili 2022/2023 – 2024/25 jana tarehe 4 Aprili 2022 Jijini Arusha, Jaji Siyani alisema, kwa kuwa wao ndiyo wataalamu katika maeneo yao, Mahakama inatarajia watafanya tafiti za kina na hivyo kuibua mikakati mizuri ya utekelezaji wa kazi zao kwa weledi mkubwa.
“Kwa kuwa sote tunajenga nyumba moja na nia yetu ni moja niwaase wenzetu wa Kitengo cha Maboresho (JDU) na wamiliki wa malengo ya kimkakati (SO-Owners) kuimarisha mahusiano baina yao” alisema Jaji Kiongozi
Mhe. Siyani akaongeza kuwa ni vema JDU na wamiliki wa malengo ya kimkakati wawe na mtazamo chanya katika utekelezaji wa majukumu yao ili wanakutana na changamoto zozote zitakazojitokeza waweke meza ya pamoja na kuzitafutia ufumbuzi.
Jaji Siyani akafafanua kuwa, ili Mahakama ifanikiwe katika utekelezaji wa Mpango Mkakati na Mradi wa uboreshaji lazima kazi zote zinazotekelezwa zijulikane kwa Viongozi na watumishi wa Mahakama wa ngazi zote na wajibu na majukumu ya kila mmoja yakabainishwa wakati huu wa kuweka mipango ya utekelezaji.
Amesema SO Owners wote watapaswa kumiliki ipasavyo shughuli zao na kuzitekeleza kwa ufanisi mkubwa na kasi iliyokusudiwa hasa wakizingatia kwamba muda wa utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa Mahakama awamu ya pili ni mfupi sana takribani miaka mitatu (3) na una fedha nyingi ukilinganisha na miaka mitano ya awamu ya kwanza.
Aidha, Jaji kiongozi akawakumbusha watekelezaji wa Mpango Mkakati kuwa ucheleweshaji wa shughuli za mradi wa uboreshaji zinatokana na watekelezaji kutomiliki ipasavyo shughuli za wanazotakiwa kuzitekekeleza na kuzikasimu kwa Maafisa wa chini.
“Mfano maandiko mengi (Concept notes) zilizowasilishwa JDU bila wamiliki wa malengo ya kimkakati kuzipitia vizuri ilipelekea maandiko hayo kurejeshwa tena kwao kwa ajili ya kurekebishwa na kusababisha kuchelewesha utekelezaji wa shughuli husika,” alisema.
Mhe. Siyani akawaasa watekelezaji wa mradi kutatua changamoto ya umiliki mdogo wa shughuli za mradi (low ownership) zinazotekelezwa kwenye maeneo mbalimbali.
Alisema hilo lilidhihilishwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama kutokuwa na taarifa za kina za miradi inayatekelezwa na katika maeneo husika na hivyo kushidwa kusimamia ipasavyo miradi hiyo.
“Kwa kiasi kikubwa jambo hili lilichangiwa na ushirikishwaji hafifu na pia Viongozi wa Kanda kuona kuwa masuala ya maboresho ni ya Makao Makuu na wao hayawahusu,” Jaji Kiongozi huyo amesema.
Kwa mujibu wa Jaji Siyani, kwa kuwa utekelezaji wa Mpango Mkakati sio suala la Makao Makuu pekee bali ni la Mahakama zima hivyo baadhi ya kazi zitashushwa chini (Cascading) ili zitekelezwe na kila mmoja wenu kwa ufanisi mkubwa.
Amesema mafanikio ya utekelezaji wa Mpango Mkakati pamoja na Mradi wa uboreshaji huduma za Mahakama utategemea zaidi kujitoa kwa kila Kiongozi, Mtumishi na Wadau wa Mahakama na kuongeza ushirikiano katika ngazi zote.
Jaji Kiongozi akawakumbusha wote wanahusika na uboreshaji kuhakikisha kunakuwa na ushirikishwaji wa kutosha baina yao, Viongozi wote wa Mahakama kwa ngazi mbalimbali wahakikishe wanajihusisha na usimamizi wa shughuli zote zinazotekelezwa katika maeneo yao, kama ambavyo zitakuwepo kazi zitakazo gatuliwa kwao ili zitekelezwe.
“Bila kuacha shaka kazi hizi zitaenda sambamba na kufanya ukaguzi, kutoa ushauri na mapendekezo ya namna bora zaidi ya kufanikisha utekelezaji wa miradi husika katika maeneo mbalimbali inakotekelezwa na kutoa taarifa za miradi hiyo kwa wakati ili maamuzi sahihi yaweze kufanyika kwa wakati,” alisisitiza Mhe. Siyani.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akifungua kikao kazi cha siku ya pili cha wajumbe wa mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama awamu ya pili na Mradi wa uboreshaji huduma za Mahakama awamu ya pili 2022/2023 – 2024/25 jana tarehe 4 Aprili 2022 Jijini Arusha.
Sehemu ya wajumbe wa kikao kazi cha mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama awamu ya pili na Mradi wa uboreshaji huduma za Mahakama awamu ya pili 2022/2023 – 2024/25 wakifuatilia hotuba ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (hayupo pichani)
Sehemu ya wajumbe wa kikao kazi cha mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama awamu ya pili na Mradi wa uboreshaji huduma za Mahakama awamu ya pili 2022/2023 – 2024/25 wakimsikiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (hayupo pichani)
Sehemu ya wajumbe wa kikao kazi cha mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama awamu ya pili na Mradi wa uboreshaji huduma za Mahakama awamu ya pili 2022/2023 – 2024/25 wakimsikiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (hayupo pichani)
Sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani walioshiriki kikao kazi cha mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama awamu ya pili na Mradi wa uboreshaji huduma za Mahakama awamu ya pili 2022/2023 – 2024/25 wakimsikiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (hayupo pichani)
Viongozi wakuu waandamizi wa Mahakama walioshiriki kikao kazi cha mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama awamu ya pili na Mradi wa uboreshaji huduma za Mahakama awamu ya pili 2022/2023 – 2024/25 wakimsikiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (hayupo pichani)
Picha na Innocent Kansha – Mahakama