Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Mkoani Tabora (WETCU 2018 LTD) Samwel Jokeya Akiwa ofisini kwake mara baada ya kufanya mazungumzo na waandishi wahabari.
………………………………………………
Na Lucas Raphael,Tabora
WAKULIMA wa zao la tumbaku Mkoani Tabora wamehakikishiwa kuwa katika msimu huu wa kilimo tumbaku yao yote itanunuliwa kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na serikali kwa kushirikiana na Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku (WETCU).
Hayo yamebainishwa jana na Meneja Mkuu wa Chama hicho (WETCU 2018 LTD) Samwel Jokeya alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo alieleza kuwa makampuni yanayonunua zao hilo yameongezeka.
Alisema baadhi ya makampuni yanayotarajiwa kushiriki kwenye ununuzi wa zao hilo msimu huu ni Alliance One Tobacco Tanzania Ltd (AOTTL), Japan Tobacco International Leaf Services (JTILS) na Magefa Tobacco Growers.
Makampuni mengine ni Pachtec Company Ltd (PCL), Naile Leaf na ENV services na kuongeza kuwa serikali imeendelea kuhamasisha wanunuzi wengi zaidi kujitokeza msimu huu ili tumbaku yote itakayozalishwa inunuliwe kwa bei nzuri.
Meneja huyo alieleza kuwa mwanzoni mwa msimu wakulima walielekezwa kuzingatia uwekaji sahihi wa mbolea, matumizi ya viuatilifu, matumizi ya manailoni, upandaji na utunzaji miti ikiwemo ya asili, matumizi ya vifaa kinga, uboreshaji majiko na ujenzi wa mabani ya kisasa ili kuongeza uzalishaji wa tumbaku bora.
“Msimu huu tumepata ongezeko la uzalishaji kutoka makampuni 6 ambayo yamesaini mikataba ya uzalishaji na vyama vya msingi 101ambapo makisio ya uzalishaji sasa yamefikia kilo million 16.2, hii ni neema kwa wakulima”, alisema.
Jokeya alibainisha kuwa katika msimu uliopita wa 2020/2021 walikisia kuzalisha kilo mililioni 14.5 lakini wakazalisha kilo mililion 12 za tumbaku ambazo ziliingizia wakulima kiasi cha sh bililon 42 kwa bei ya dola 1.54 kwa kilo.
Nakuongeza kuwa kwa mwaka huu katika makisio ya kilo mililion 16.2 zitakazozalishwa na vyama wanachama wa WETCU wanatarajia kupata zaidi ya sh bilion 61.5 kwa bei ya dola 1.62 kwa kilo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chama hicho Kikuu cha Ushirika wa Wakulima, Hamza Rajabu alipongeza serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujali wakulima na kusimamia ipasavyo maslahi yao.
Alibainisha kuwa hatua ya hivi karibuni ya Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kumwalika Rais kugawa vitendea kazi kwa Maofisa Ugani wote ni ishara njema ya kuboresha utendaji wao ili kilimo kilete tija kwa wakulima hapa nchini.
Alisisitiza kuwa watawatumia ipasavyo ili kuongeza uzalishaji wa mazao yote ya kimkakati ambayo yanalimwa na wakulima wa Mkoa huo ambayo ni korosho, pamba, tumbaku, alizeti, mpunga na mahindi huku akiwataka kutoka maofisini.
Aidha katika kuhakikisha wananufaika na jasho lao, aliwataka kuongeza umakini katika ufungashaji wa tumbaku yao katika msimu huu wa masoko ikiwemo kutochanganya madaraja ili iuzwe kwa bei nzuri.