KAIMU Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Mhandisi Samweli Tanguye,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo SApril 6,2022 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia.
KAIMU Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Mhandisi Samweli Tanguye,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo SApril 6,2022 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia.
………………………………………………
Na Bolgas Odilo-DODOMA
MENEJIMENTI ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetaja mafanikio matano ambayo imeyapata katika kipindi cha awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Akiyataja mafanikio hayo leo April 6,2022,mbele ya Waandishi wa Habari Jijini Dodoma,Kaimu Katibu wa Sekretarieti hiyo,Mhandisi Samweli Tanguye amesema katika kutekeleza majukumu yake Ofisi hiyo imepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuteuliwa Mwenyekiti wa Bodi,vibali,ujenzi wa ofisi,mfumo wa ajira pamoja na kusimamia kanuni sheria na taratibu.
MWENYEKITI WA BODI
Amesema Mhe. Rais alipoingia madarakani hakuisahau Taasisi hiyo ambapo alimteua Mwenyekiti wa Bodi ya Wajumbe wa Sekretarieti ya Ajira na baadaye akawapatia Wajumbe wa bodi ya Sekretarieti ya Ajira.
“Mwaka mmoja nyuma, tuliendesha shughuli zetu pasipo kuwa na chombo cha juu cha maamuzi baada ya Bodi ya awali kuwa imemaliza muda wake.
“Chombo hiki cha maamuzi ni muhimu sana kwenye utendaji kazi wa kila siku wa Taasisi yetu na kinaongozwa na Bi. Sophia Kaduma ambaye ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Wajumbe wa sekretarieti ya Ajira.
VIBALI
Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja cha kuanzia Machi, 2021 mpaka Machi, 2022, Mhe. Rais, ametoa idadi ya vibali vya ajira vyenye nafasi nyingi za ajira ukilinganisha na kipindi kama hicho nyuma. Mfano, tumepokea kibali cha kuajiri Watanzania 2100 kwa ajili ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.
“Hii ni rekodi ya aina yake, kibali cha ajira za wahandisi mia mbili sitini na nane (268) kwa ajili ya TAMISEMI na tayari wameshapangwa kazini. Nafasi 508 kwa ajili ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) ambao nao wamepangwa kazini,”amesema.
UJENZI WA OFISI
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan pia ametuwezesha kuanza ujenzi wa Ofisi za Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma h Dodoma ambapo amedai unatarajia kuanza kabla ya mwaka huu wa fedha kumalizika.
“Mhe. Rais Samia hakuishia hapo, katika kipindi hiki, ametuongezea Shilingi Milioni mia sita themanini na tisa nje ya bajeti iliyoidhinishwa mwaka jana na hivyo kutufanya kutekeleza majukumu yetu vizuri. Na sasa, ameiongeza bajeti ya Taasisi kutoka Shilingi 3,388,771,000 katika mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia Shilingi 8,721,849,000 kwa mwaka wa fedha ujao wa 2022/2023. Katika hili, nasi hatuna budi kusema mama anaupiga mwingi,”amesema.
MFUMO WA AJIRA PORTAL MOBILE APP
Amesema ili kuhakikisha watanzania wanapata taarifa za michakato ya ajira na hususan walioko vijijini na maeneo ya pembezoni.
“Mhe. Rais Samia, alitupatia fedha na tumejenga mfumo wa “Ajira Portal Mobile App” ambao umeanza kuwasaidia waombaji fursa za ajira kupata taarifa za ajira popote walipo kupitia simu zao za kiganjani,”amesema.
Aidha, kupitia mfumo huo, mwombaji kazi anaweza kuomba kazi na kupokea taarifa za mchakato wa ajira kupitia simu yake.
“Mhe. Rais, Samia Suluhu Hassan ametuwezesha na tumefanikiwa kununua magari matatu ya Ofisi ili kutoa huduma zilizo bora na kuwafikia Watanzania.
SHERIA KANUNI NA TARATIBU
Amesema Sekretarieti ya ajira itaendelea kutekeleza jukumu la kuendesha mchakato wa Ajira kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu pamoja na miongozo mbalimbali kwa weledi wa hali ya juu.
“Ili kuwezesha upatikanaji wa wataalam wenye sifa za kuajiriwa katika Utumishi wa Umma ili nchi yetu iweze kufikia malengo iliyojiwekea kwenye dira ya maendeleo ya Taifa 2025,”amesema.