Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Augustine Mwarija (kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Jarida la Mahakama ya Rufani (T). Hafla ya uzinduzi huo imefanyika jana tarehe 05 Aprili, 2022 katika Ukumbi wa ‘Mount Meru’ jijini Arusha ambapo kinafanyika Kikao kazi cha Mapitio ya Mpango Mkakati wa pili wa Mahakama wa mwaka 2020/2021-2024/2025 sambamba na kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Mahakama. Wanaoshuhudia, wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga, wa pili kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na wa kwanza kulia ni Mhe. Happiness Ndesamburo, Naibu Msajili Mwandamizi-Mahakama ya Rufani (T).
Nyuso za furaha mara baada ya uzinduzi wa Jarida la Mahakama ya Rufani (T) uliofanyika jana tarehe 05 Aprili, 2022 katika Ukumbi wa ‘Mount Meru’ jijini Arusha.
Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa Jarida la Mahakama ya Rufani (T).
Sehemu ya Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu na Washiriki wengineo walioshuhudia uzinduzi wa Jarida la Mahakama ya Rufani (Court of Appeal Journal).
…………………………………………
Na Mary Gwera, Mahakama-Arusha
Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Augustine Mwarija amezindua rasmi Jarida la Mahakama ya Rufani (Court of Appeal Journal) huku akisisitiza Wananchi kusoma Jarida hilo ambalo linapatikana pia kupitia tovuti ya Mahakama ya www.judiciary.go.tz.
“Kumekuwa na maswali mengi ya jinsi Mahakama ya Rufani inavyofanya kazi, mathalani wengi wamekuwa wakijiuliza katika jopo la Majaji Watatu wa Mahakama ya Rufani ni nani anayeandika hukumu na maswali mengineyo, hivyo ni vyema kulisoma Jarida hili ili kupata taarifa mbalimbali kuhusu Mahakama ya Rufani (T) ikiwa ni pamoja na kufahamu historia ya Mahakama ya Rufani na kadhalika,” amesema Jaji Mwarija.
Jaji Mwarija ameongeza kuwa Jarida hilo lililopo kwenye lugha ya Kiingereza linaeleza utendaji wa Mahakama ya Rufani na vilevile linaonyesha ufanisi pamoja na historia ya Mahakama hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka.
“Wengi pia watajiuliza kwanini Jarida hili lipo kwenye Lugha ya Kiingereza, tumefanya hivi kwa kuanzia lakini mpango tulionao katika toleo zijazo ni kutumia Lugha zote mbili katika Jarida hili ili kuwawezesha Wadau wote waweze kuelewa kilichoandikwa,” amesema Jaji huyo.
Kwa upande wake Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina amesema kuwa wazo la kuanzisha Jarida hilo la mwaka 2021 lilianzia kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
“Wazo la kuanzisha Jarida hili lilianzia kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma na tumelitekeleza, na Jarida hili ni la mwaka 2021 lina taarifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na takwimu mbalimbali zinazoonyesha utendaji wa Mahakama, historia ya kuanzishwa kwake, orodha ya Majaji wa Mahakama hiyo na mengineyo,” amesema Mhe. Mhina.
Aidha, Msajili huyo ameishukuru Timu nzima iliyowezesha kufanikisha upatikanaji wa Jarida hilo na kuomba ushirikiano zaidi.
Jarida hilo limezinduliwa leo ikiwa ni siku ya pili ya Kikao kazi cha Mapitio ya Mpango Mkakati wa pili wa Mahakama wa mwaka 2020/2021-2024/2025 kinachokwenda sambamba na kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Mahakama kinachoendelea kufanyika jijini Arusha.
Mahakama ya Tanzania inaendelea kuuhabarisha umma kwa njia mbalimbali mojawapo ikiwa ni kupitia Majarida yake ya ‘Haki Bulletin’ linalotolewa mara nne kwa mwaka pamoja na Jarida hilo la Mahakama ya Rufani lililozinduliwa ambalo litakuwa likitolewa mara moja kwa mwaka.