Kaimu afisa Maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya ya Igunga Gidfrey Chezue akitoa elimu kwa wajasiliamali wa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wakati wa utoaji wa mikopo uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Igunga mkoani Tabora.
……………………………………………….
Na Lucas Raphael Igunga
Halmashauri ya wilaya ya Igunga mkoani Tabora imefanikiwa kutoa mikopo ya fedha kwa wajasiliamali kwa makundi ya wanawake vijana na watu wenye ulemavu kupitia mapato yake ya ndani ya asilimia 10 ambayo halmashauri imekuwa ikikusanya na kutenga fedha hizo.
Hayo yamebainishwa na kaimu afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya wilaya ya Igunga Godfrey Chezue wakati wa utoaji wa mikopo ya fedha ya Mil. 88,204,678.01 kwa vikundi 14 vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Igunga.
Chezue alisema idara ya maendeleo ya jamii ya halmashauri ya wilaya ya Igunga imeendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake vijana na watu wenye ulemavu ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya fedha ya serikali za mitaa sura 290 ya kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake vijana na watu wenye ulemavu ya mwaka 2019 kama ilivyofanyiwa marekebisho februari mwaka 2021.
Aidha Chezue alisema katika mwaka wa 2021/2022 halmashauri ya wilaya ya Igunga imeweza kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia utengaji wa asilimia kumi ya makusanyo ya mapato ya ndani kwenda mfuko wa maendeleo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu imeweza kukopesha vikundi hivyo kiasi cha Mil. 228,700,00.00
Alisema katika kipindi cha robo ya julai – septemba 2021/2022 ilitolewa mikopo yenye thamani ya Mil. 113,980,600 huku akiongeza kuwa hii mikopo ya vikundi 14 ni ya robo ya oktoba desemba 2021/2022 yenye thamani ya Mil. 88,204,678 isiyo na riba yoyote.
Alisema katika fedha hizo za robo ya oktoba desemba 2021/2022 vikundi 7 vya wanawake vimepewa Mil. 41,902,339 ambapo vijana vikundi 6 vimepewa Mil. 41,302,339 na kikundi kimoja cha walemavu kimepewa Mil. 5 na kusema kuwa vikundi hivyo vimepewa mikopo hiyo baada ya kukidhi vigezo vyote vya mikopo.
Wakitoa shukrani kwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassani baada ya kupokea mikopo hiyo ya fedha baadhi ya wajasiliamali wa makundi hayo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu Magreth Benjamin, Wakulu Juma, Hamisi Kafumu na Kimali Busagara.
Kwa nyakati tofauti walisema wanaishukuru serikali kwa kutoa mikopo hiyo isiyo na riba ambapo walisema itasaidia wao kufanya biashara bila misukosuko yoyote na kuongeza kuwa kuwa mikopo hiyo imesaidia kupunguza wimbi la ajira kwa vijana kwani wao tayari wanaenda kujiajiri kupitia biashara zao.
Aidha walimpongeza mkurugenzi wa halmashauri ya Igunga Fatuma Omari na timu yake kwa kusimamia vizuri mapato ya halmashauri ya Igunga na kutenga fedha hizo za makundi hayo ambapo wamefanikiwa wao kukopeshwa huku wakiahidi kurejesha fedha hizo kwa muda waliopewa na halmashauri.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Igunga Joseph Elias aliwataka wanavikundi hao kuzitumia fedha kwa kazi walizoziainisha katika maombi yao ya mikopo huku akiwahakikishia kuwa halmashauri itaendelea kutenga fedha kupitia mapato yake ya ndani na kuongeza kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha inawainua kiuchumi wananchi wake.
Mwisho.
MAELEZO YA PICHA
Kaimu afisa Maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya ya Igunga Gidfrey Chezue akitoa elimu kwa wajasiliamali wa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wakati wa utoaji wa mikopo uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Igunga mkoani Tabora.