Na Silvia Mchuruza-BUKOBA,KAGERA.
Wazazi wametakiwa kuacha tabia ya kuwalea watoto kama kuku wa kizungu aina ya (Broira), jambo linalosababisha Taifa kuwa na watu wasioweza kulihudumia na kuwa wazalendo.
Onyo hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Moses Machali ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe ya mahafali ya sita ya kidato cha sita ya shule za sekondari ya Kaizilege na ya tano kwa Kemibosi.
Machali amesema wapo wazazi wanaowadekeza watoto wao kwa kutaka wasiadhibiwe wanapokosea kwa madai kuwa watoto hao wamenyimwa haki za binadamu, jambo linalotengeneza kizazi cha watu ambao hawawezi kulijenga Taifa kutokana na kukosa maadili na kuvunja mila na desturi za kiafrika.
Naye Karibu Tawala Wilaya ya Bukoba, Kadole Kirungala amesema ajira zinazotolewa na serikali na Taasisi binafsi hazitoshi kutolewa kwa wahitimu wote wa vyuo vikuu na kidato cha sita hivyo watumie muda watakaokaa mtaani kutafakari, kujitathimini na kujifunza ndani yao vipaji walivyonavyo ambavyo vinaweza kuwaingizaia kipato.
Amesema imekuwa kawaida kwa wahitimu wengi pamoja na wazazi kutegemea ajira zinazotolewa na serikali ili kupata fedha ya kuendesha maisha yao badala ya kutumia vipaji walivyonavyo kujiingizia kipato cha kuendesha maisha yao.
Wakati huo, Meneja wa shule hizo, Eurigius Katiti amesema Taasisi hiyo ina mpango wa kuanzisha chuo cha kuwasaidia vijana wanaohitimu kidato cha nne na sita kusoma na kupata taaluma ya kazi, ambacho kitajengwa katika Wilaya ya Bukoba ili kuchochea maendeleo ya wilaya hiyo, Mkoa wa Kagera na Taifa kwa ujumla.
Pia amesema taasisi hiyo imetoa ajira kwa watanzania wengi, imekuza mitaji ya wafanyabiashara, imepandisha pato la Taifa kwa kulipa kodi mbalimbali na kuboresha miundombinu ambayo imeweze kutumika katika kipindi chote cha mwaka ikiwemo barabara, afya na kuwa na wataalam waliobobea katika kazi zao kwa kada mbalimbali.