Afisa Uhusiano wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF), Usia Nkoma akizungumza wakati wa warsha ya uhamasishaji kwa Kamati za Kudumu za Bunge kuhusu masuala ya watoto na Bajeti iliyofanyika jijini Dodoma.
Mtaalam wa uchambuzi wa Bajeti,UNICEF Hayrullo Malikov,akitoa mada wakati wa warsha ya uhamasishaji kwa Kamati za Kudumu za Bunge kuhusu masuala ya watoto na Bajeti iliyofanyika jijini Dodoma.
Mtaalam wa Sera za Kijamii UNICEF,Zena Amury,akizungumzia umuhimu wa bajeti wa warsha ya uhamasishaji kwa Kamati za Kudumu za Bunge kuhusu masuala ya watoto na Bajeti iliyofanyika jijini Dodoma.
BAADHI ya wabunge wa Kamati za Kudumu za Bunge wakichangia mada mbalimbali wakati wa semina ya wabunge ya umuhimu wa kuongeza bajeti katika huduma za watoto na jamii iliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) iliyofanyika jijini Dodoma.
SEHEMU ya wabunge wa Kamati za Kudumu za Bunge wakifatilia mada mbalimbali wakati wa semina ya wabunge ya umuhimu wa kuongeza bajeti katika huduma za watoto na jamii iliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) iliyofanyika jijini Dodoma.
………………………………………………….
Na Bolgas Odilo, Dodoma.
MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (Usemi) Mhe.Dennis Londo ameishauri Serikali kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi nchini ili kutatua changamoto mbalimbali.
Kauli hiyo ameitoa wakati akichangia katika semina ya wabunge ya umuhimu wa kuongeza bajeti katika huduma za watoto na jamii iliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) iliyofanyika jijini Dodoma.
Mhe.Londo amesema kuwa miongoni mwa mambo ambayo waliishauri wakati wakijadili bajeti ya 2022/2023 kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na halmashauri ni kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi.
Aidha amesema kuwa walishauri Serikali kuweka mazingira rafiki katika ulinzi wa kisheria na pamoja na kuibua hoja za bajeti katika shule kwa ajili ya chakula shuleni.
“Kwa kweli tumekuwa wakali lakini tunaamini kuwa kabisa bajeti hii inakwenda kulenga maeneo muhimu ya kusoma katika mazingira mazuri,”amesema.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Shally Raymond alisema hakuna bajeti kwa ajili ya mama wajawazito na masuala ya ulemavu yamekuwa yakianzia tangu tumboni.
“Unazaa Katoto kamenyong’onyea tu nilikuwa naomba kwasababu ni elimu na tunataka kuweka vizuri bajeti zetu wazazi walio katika kaya masikini wasaidie,”alisema.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Stanslaus Nyongo alisema taarifa walizozipata kutoka katika shirika hilo ni muhimu kwa wabunge kwenye kijenga hoja na kutetea bajeti na kuhakikisha Serikali inafanya majukumu yake ipasavyo.
“Uwekezaji kwa watoto ni jambo muhimu sana kwasababu ndio Taifa la kesho na hakuna nchi nyingine itakayokuja kuweka mazingira mazuri kwa watoto wetu isipokuwa ni sisi wenyewe,”alisema.
Awali Ofisa Mawasiliano wa Unicef, Usia Nkoma alisema kuwa watoto wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili majumbani na shuleni kwa kulawitiwa na kubakwa hivyo wanashauri wabunge wajielekeze katika kuweka mazingira mazuri kwa watoto kwa kukomesha ukatili.
“Tujenge mazingira ya kuhakikisha watoto wetu wanakuwa salama na kuwajengea uwezo wa kusema wanayokabiliana nayo. Tuujenge jamii ya watu wanaokataa ukatili, ”alisema.