Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nakapanya wilayani Tunduru wakiwa katika mistari kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kutoka kwa wataalam wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma wilaya ya Tunduru.
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole akitoa elimu kwa wakazi wa kijiji cha Namiungo wilayani humo kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu wakati wa kampeni za uhamasishaji na uchunguzi wa ugonjwa huo zinazoendelea katika vijiji mbalimbali chini ya ufadhili wa Shirika lisilo la Kiserikali la MDH.
Wakazi wa kijiji cha Mkowela kata ya Namakambale wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakisubiri kupata huduma ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu wakati wa kampeni dhidi ya mapambano ya ugonjwa huo zinazoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali mkoani Ruvuma.
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole akizungumza na baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Mchangani wakati wa kampeni ya dhidi ya mapambano ya ugonjwa wa kifua kikuu inayoendelea wlilayani humo chini ya ufadhili wa Shirika lisilo la Kiserikali la MDH
………………………………………..
Na Muhidin Amri,Tunduru
JUMLA ya watu 87 kati ya 452 waliofanyiwa uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu katika vijiji vinne wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wamebainika kuwa na maambukizo ya ugonjwa huo.
Hayo yamesemwa jana na Mratibu wa kifua kikuu na ukoma mkoa wa Ruvuma Dkt Xavier Mbawala, wakati akitoa taarifa ya kampeni dhidi ya mapambano ya ugonjwa wa kifua kikuu iliyofanyika katika vijiji vinavyozungukwa na machimbo ya madini.
Dkt Mbawala alisema,kubainika kwa watu hao kunatokana na kampeni kabambe ya kuwaibua wagonjwa wa TB iliyofanyika kwa siku nne katika vijiji vya Mkowela,Namiungo,Nakapanya na Majimaji wilayani humo.
Alisema,Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ikiwamo Shirika lisilo la kiserikali la MDH limeanza kampeni hiyo ambapo mwaka huu wamenza kwenye machimbo na vijiji vinavyozungukwa na migodi ya madini.
Kwa mujibu wake,lengo ni kuhakikisha wananchi wote wenye ugonjwa wa kifua kikuu wanafikiwa na kuanzishiwa matibabu yanayotolewa bure katika vituo vya kutolea huduma vya serikali na binafsi na hatimaye waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Amewataka wananchi,kujitokeza kwa wingi katika kampeni hizo ili kupata fursa ya kuchunguzwa afya zao hususani maradhi ya kifua kikuu ambayo yanatajwa kuwa miongoni mwa magonjwa kumi yanayoongoza kupoteza maisha ya watu wengi Duniani.
Kwa upande wake mratibu wa kifua kikuu na ukoma wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema,katika kampeni hiyo iliyofanyika kwa siku nne mfululizo kwa kutumia kliniki tembezi wamegundua idadi kubwa ya watu waliojitokeza wana dalili zote za kifua kikuu.
Alisema,kampeni ya uchunguzi wa kifua kikuu inafanyika mara kwa mara katika wilaya hiyo kutokana na hali halisi ya ukubwa wa ugonjwa huo.
Alisema,mkakati wa mwaka huu ni kuhakikisha wanakwenda katika maeneo yote ya machimbo na vijiji vinavyozungukwa na shughuli za uchimbaji madini ambako ni rahisi watu kupata kifua kikuu kutokana na mazingira wanayoishi na aina ya kazi wanayofanya.
Alisema, katika maeneo ya vijijini kuna idadi kubwa ya watu wenye viashiria vya ugonjwa huo, lakini kutokana na kukosa nafasi ya kufika kwenye vituo vya kutolea huduma wameshindwa kujua hali ya afya zao,badala yake wanaendelea kuteseka wakiwa majumbani jambo lilinalosababisha kushindwa kushiriki katika mbalimbali za maendeleo.
Alisema,kutokana na changamoto hiyo wizara ya afya kwa kushirikiana na Hospitali ya wilaya kupitia kitengo cha kifua kikuu imeona ni vyema wataalam wake kufika maeneo ya pembezoni ili kuwafanyia uchunguzi na kuwaanzishia matibabu wale wanaobainika kupata ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Mkasange, tatizo la umaskini kwa baadhi ya familia limesababisha kuongezeka kwa ugonjwa huo, kwa sababu baadhi ya watu hawapati fursa ya kwenda kufanya uchunguzi wa afya zao,lakini serikali kwa kushirikiana na shirika la MDH itahakikisha wananchi wa maeneo hayo wanafikiwa na kupata matibabu.
Paroko wa Parokia ya Mama Mwakozi Nakapanya Padri Severianus Mutembei, ameishukuru Serikali kupitia wizara ya afya na wadau wa maendeleo MDH kwa kupeleka huduma za uchunguzi na matibabu ya kifua kikuu vijijini, kwa kuwa itaokoa watu wengi wanaougua ugonjwa huo hasa wanaoishi vijijini.
Alisema,tatizo la kifua kikuu linalosumbua sana katika jamii yetu kwani wapo watu wengi wanaougua kifua kikuu, hata hivyo hawapati matibabu ya uhakika kutokana na kukosa uwezo wa fedha kwenda katika vituo vya kutolea huduma kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.
Ameipongeza serikali kuendelea kuwafuata wananchi wanaoishi maeneo ya vijiji kwa ajili ya kuwapa huduma na kuomba huduma hiyo kuwa endelevu ili kuokoa maisha ya wananchi ambao wataweza kushiriki ujenzi wa Taif ana kukuza uchumi.
Mkazi wa kitongoji cha Mchangani kijiji cha Mkowela Ahmadi Halfan bado kuna watu wengi wako majumbani wanaougua kifua kikuu ambao wameshindwa kwenda katika vituo vya afya na Hospitali kupata matibabu.
Ameiomba Serikali kupitia wataalam wa kitengo cha kifua kikuu kutembelea vijijini mara kwa mara kwa ajili ya kuwafanyia wananchi uchunguzi wa afya zao.