Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe akitoa elimu ya kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali alipohudhuria, zoezi la kumsimika kiongozi (Olaigwanani) wa familia ya Napaya ambae pia ni Diwani wa kata ya Ngabobo Mkoani Arusha.
*************************
Na WAF – NGABOBO, ARUSHA
MGANGA MKUU wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amewaelekeza viongozi wa jadi/mila nchini kuhakikisha wanapambana na tatizo la vifo vya Wajawazito ambalo kwa kiasi kikubwa linatokana na kuchelewa kwenda kliniki, mjamzito kutojifungulia katika vituo vya kutolea huduma au kuchelewa kufika katika vituo hivyo.
Ameyasema hayo alipofanya ziara ya kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa kwa jamii, shughuli iliyoambatana na zoezi la kumsimika kiongozi (Olaigwanani) wa familia ya Napaya ambae pia ni Diwani wa kata ya Ngabobo Mkoani Arusha Bw. Gabriel Kinwaa Mollel.
“Tunataka mtusaidie sana katika kuhamasisha na kuelimisha jamii kutumia miundombinu/uwekezaji ambao Serikali imeufanya kwa kuhakikisha wajawazito wanakwenda kliniki mapema lakini pia waweze kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma, hatutaki kuona mama anajifungulia nyumbani halafu akafariki.” Amesema.
Moja kati ya vipaumbele vya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Ally Mwalimu ni kuhakikisha suala la huduma bora za mama na mtoto zinaboreshwa ili kuondoa vifo vinavyotokana na uzazi vinavyoweza kuzuilika. Amesisitiza Dkt. Sichalwe.
Sambamba na hilo, Dkt. Sichalwe amewataka viongozi kuhakikisha wanahamasisha wananchi kujenga na kutumia vyoo ipasavyo ili kuepuka magonjwa ya mlipuko hasa kipindupindu na magonjwa mengine ya matumbo yanayoweza kuzuilika na kuipunguzia Serikali gharama za matibabu.
Pia, Dkt. Sichalwe amewaomba Olaigwanani kuendelea kuhamasisha na kusisitiza jamii zao juu ya umuhimu wa kupata Lishe bora, hususan kwa wamama wajawazito na Watoto ili kujenga Taifa la watu wenye afya bora na uwezo wa kufikiri katika kuleta Mapinduzi ya kimaendeleo katika ngazi ya jamii mpaka Taifa.
Mbali na hayo, amesema Serikali imetimiza wajibu wake wa kuleta maendeleo kwa Wananchi wake kwa kuboresha miundombinu ya afya, elimu, barabara, umeme na maji ambayo kwa kiasi kikubwa inachochea ukuaji wa shughuli za uchumi na kuwataka kuendelea kuitunza miundombinu hiyo ili iendelee kuleta tija katika maeneo yao.
Nae, Diwani wa kata ya Ngabobo na kiongozi wa familia ya Napaya Bw. Gabriel Kinwaa Mollel amemshukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa jitihada za kuboresha huduma kwa wananchi ikiwemo elimu ya kujikinga dhidi ya ugonjwa mbalimbali na elimu ya huduma za mama na mtoto.