*************************
Na Selemani Msuya
ZAIDI ya viwanja 600,000 katika Mkoa wa Dar es Salaam vimetambuliwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi huku viwanja vilivyolipiwa gharama za urasimishaji vikiwa 171,000.
Aidha, imebainika kuwa baadhi ya kampuni zilizopewa kazi ya kurasimisha ardhi katika mitaa mbalimbali, yamekuwa yakichelewa kukamilisha kazi kwa wakati.
Hayo yamesemwa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa humo, Idrisa Kayera wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hilo ofisini kwake.
Kayera amesema mkoa umejitahidi kutambua viwanja zaidi ya 600,000 katika wilaya za Ubungo, Kinondoni, Temeke, Ilala na Kigamboni ila changamoto iliyopo ni wamiliki wa ardhi zilizotambulika kushindwa kulipia urasimishaji.
Kamishna msaidizi huyo amesema mkakati wao ni kuhakikisha ardhi yote ya mkoa wa Dar es Salaam irasimishwa na kupimwa ili waweze kutoa hati za kumiliki kwa wananchi.
Kayera amesema mchakato wa urasimishaji unaenda sambamba na utoaji wa hati ya kumiliki ardhi ambayo ni nyaraka muhimu kwa mtu yoyote ambaye atataka kumiliki ardhi.
“Sisi tunaendelea na utambuzi wa viwanja ambapo zaidi ya viwanja 600,000 vimetambuliwa, changamoto kubwa ipo kwa wenye kulipa Sh.150,000 ya urasimishaji, kwani hadi sasa viwanja ambavyo vimelipiwa ni 171,000, yaani hata nusu haijafika,” amesema.
Kamishna msaidizi huyo amewataka wamiliki wa viwanja katika jiji la Dar es Salaam kulipia Sh.150,000 kwa kampuni za kurasimisha ili mchakato wa kutoa hati uweze kukamilika kwa wakati.
Amesema ofisi yake inafanya kazi kwa njia za kiteknolojia hivyo iwapo mmiliki atafanikisha michakato yote muhimu kwa wakati wao hawatakuwa na sababu ya kuchelewa kutoa hati.
Aidha, Kayera amesema pamoja na kuwepo na mwamko mdogo wa baadhi ya wamiliki wa viwanja kulipa kwa wakati,fedha za urasimishaji, pia kuna baadhi ya kampuni za urasimishaji ambazo zinachelewesha mchakato wa kupatikana hati.
Amesema pia wamebaini katika baadhi ya maeneo zipo kamati ambazo zinatumika kuwakilisha wenzao katika mchakato wa urasimishaji ila zimeshindwa kwenda na kasi.
“Tunatumia kampuni mbalimbali za urasimishaji kwenye mitaa, ila bado wapo wachache ambao wanasuasua. Nitumie nafasi hii kuzitaka kampuni hizo ziongeze kasi ili kuhakikisha wananchi wanapata hati,” amesema.
Kamishna Kayera ametoa wito kwa watu wote wanaomiliki ardhi katika mkoa wa Dar es Salaam kuendeleza maeneo yao ili kuepuka uvamizi ambao umekuwa chanzo cha migogoro.
Amesema Serikali imepunguza gharama za kupata hati hadi kufikia asilimia 0.5, hivyo kila mtu ambaye anamiliki ardhi anaweza kupata hati bila usumbufu wowote.