Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha amewataka Wadau wa Mahakama kubadilika kifikra na kuwa tayari kwenda sambamba na uboreshaji wa matumizi ya TEHAMA mahakamani.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya siku (3) kuhusu mifumo ya uendeshaji wa mashauri kwa njia ya mtandao kwa wadau na watumishi wa Mahakama Mkoa wa Kigoma, Jaji Mlacha alisema kuwa na fikra chanya kuhusu uboreshaji wa Matumizi ya TEHAMA unaoendelea mahakamani utawezesha mafanikio ya azma ya Mahakama ya kuwa Mahakama Mtandao (e-Judiciary).
“Mahakama ilishaanza safari ya kuelekea Mahakama Mtandao na leo hii katika mafunzo haya tunaiongezea mwendo tu ili tuweze kwenda pamoja,” alisema Jaji Mlacha.
Aliongeza kuwa usajili wa mashauri kwa njia ya mtandao pamoja na usikilizaji wake bado ni dhana mpya hivyo aliwataka Washiriki wa mafunzo hayo kutumia vyema ujuzi watakaoupata watakaporudi vituoni ili kuboresha utendaji kazi wa utoaji wa Haki kwa wakati. Alisema ni Muhimu washiriki kujua kuwa mageuzi katika dunia ya sasa yamejielekeza katika matumizi ya TEHAMA na mtandao na kwamba hayaepukiki.
“Mtakuwa mashahidi wa maendeleo makubwa ya matumizi ya akili bandia (Artificial intelligence), habari za roboti kufanya kazi kama au zaidi ya binadamu wa kawaida, Anuani za Makazi na ‘Postcode’ hivyo bila TEHAMA kwa sasa haiwezekani kushindana” alisisitiza Jaji Mlacha.
Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka alisema kuwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa uboreshaji wa huduma za Mahakama yaliyotafsiriwa katika Mpango Mkakati wa Mahakama wa miaka mitano ulioanza mwaka 2015/2016 hadi 2019/2020 kwa awamu ya kwanza na Mpango Mkakati awamu ya pili ya mwaka 2020/2021 hadi 2024/2025 ambao pamoja na mambo mengine umelenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki kwa wakati.
Mtendaji huyo alieleza kuwa mafunzo hayo yamepangwa pia ili kuwezesha wadau na Watumishi kutoka Mahakama Wilaya ya Kasulu kusajili na kuendesha kwa ufanisi mashauri yenye asili ya Kambi ya Wakimbizi Nyarugusu kwa njia ya mtandao.
Mwakilishi wa Shirika linalohudumia Wakimbizi Kituo cha Kigoma, Bw. Innocent Sangala aliupongeza Uongozi wa Mahakama kuzindua kituo cha kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao wilayani Kasulu katika Kambi ya wakimbizi Nyarugusu na kusema kuwa wataendelea kuunga mkono jitihada za kuboresha huduma hizo muhimu kwa wananchi.
“Tutajitahidi kwa kila linalowezekana kuhakikisha rasilimali chache zinazopatikana zinachangia maboresho ya Mahakama na wadau katika eneo la TEHAMA ili lengo la utoaji wa haki kwa wakimbizi na wananchi wengine liweze kufikiwa kwa wakati na kwa wote” alisema Bw. Sangala
Akitoa neno la Shukrani kwa niaba ya washiriki waliohudhuria mafunzo hayo, Inspekta wa Polisi, Bw. Dominic Mlolere ambaye pia ni Mwendesha Mashtaka wa Wilaya ya Kasulu aliupongeza Uongozi wa Shirika linalohudumia wakimbizi (UNHCR) na Kituo cha msaada wa kisheria kwa Wanawake, Watoto na Wakimbizi (WLAC), kwa kushirikiana na Uongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma kuandaa mafunzo hayo ambayo yamewaongezea ari na nguvu ya kufanya kazi hivyo kuendana na kasi ya Mahakama kuelekea Mahakama mtandao.
Washiriki wa mafunzo walijengewa uwezo kwa nadharia na vitendo kwa mafunzo yaliyowezeshwa na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mhe. Gadiel Mariki, Mtendaji wa Mahakama, Bw. Moses Mashaka na Afisa TEHAMA Bw. Prosper Bonaventura.
Mafunzo hayo yaliwashirikisha washiriki wapatao 45 kutoka Kituo cha Msaada wa kisheria kwa Wanawake, Watoto na Wakimbizi, kutoka shirika linalohudumia wakimbizi (UNHCR), Ofisi ya Waendesha Mashtaka Kigoma na Kasulu, Ofisi ya Huduma za Uangalizi Kigoma (Probation officers), Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi, Jeshi la Uhamiaji, Shirika la ‘IRC’ na watumishi wa Mahakama kutoka Kigoma na Kasulu.