Baadhi ya kinamama wajawazito wakisubiri huduma katika moja ya vituo vya afya
……………………………………………………
Na Zillipa Joseph, Katavi
Wanawake wametakiwa kuwa na maandalizi ya awali kabla ya kushika mimba kwa kuhakikisha wana afya bora ili mtoto atakayekuja kuzaliwa asiwe na mapungufu kama kuzaliwa na uzito mdogo ama utapiamlo.
Ushauri huo umetolewa na Mchungaji Peter Jerome wa kanisa la AICT Mpanda mjini wakati wa kongamano la wanawake lililoandaliwa na halmashauri ya Manispaa ya Mpanda.
Mch. Jerome amesema tatizo la udumavu linaanzia pale mama mjamzito anaposhindwa kuzingatia ulaji bora.
‘Mama unatakiwa kufanya maamuzi yaliyo haki ya mtoto wako unaetarajia kumleta duniani’ alisema
Akitoa mada ya lishe bora bwana Fikilio Gambi ambaye ni Mwakilishi kutoka mashirika mawili yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi pamoja MIIKO na RIKOTO amabyo yanajisughulisha na ulimaji wa mboga mboga na matunda amesema kinamama wanapaswa kula mlo kamili kabla na wakati wa ujauzito.
Amesema kufanya hivyo kutamwezesha mtoto aliye tumboni kuwa na afya bora.
Ameongeza kuwa mwanamke anahitaji kumeza vidonge vya kuongeza damu miezi mitatu kabla ya kushika mimba kwani vitamwezesha mtoto aliye tumboni kutopungukiwa damu.
Dk. Yustina Tizeba ni daktari bingwa wa magonjwa ya watoto anasema madhara ya kilishe yanayojitokeza yasiporekebishwa katika kipindi cha siku 1,000 za mwanzo za maisha ya mtoto huleta athari zisizoweza kurekebishwa tena katika ukuaji na maendeleo yake.
Amesema mtoto anayekuwa na lishe duni katika umri huo ambao ni sawa na kuanzia ujauzito mpaka miaka miwili ana uwezekano mkubwa wa kudumaa kimwili, kiakili, kuugua mara kwa mara na hata kufa.
Amesisitiza kwamba chakula bora ni kile kinachopatikana katika mazingira ya kawaida kama dagaa, maharage, mbogamboga na matunda cha msingi ni kuzingatia mtu ale mafungu ya aina tano ya vyakula.
Aidha ameongeza kuwa pindi mama awapo mjamzito ni vema akaanza kliniki mapema ili kupata ushauri wa kitaalamu kuhusiana na afya yake.
Kwa upande wao kinamama waliohudhuria kongamano hilo wengi wao walionyesha kutofahamu kama mama anapaswa kuanza maandalizi ya ulaji chakula bora kabla ya kupata ujauzito.
Mwanakombo Ali amesema yeye ndio kwanza anasikia kwa mara ya kwanza jambo hilo. ‘Mi najua ukiwa mjamzito ndio wanakushauri kula vizuri’ alisema
Nae Suzana Kilemeta amesema yeye huwa anahudhuria kliniki pale ujauzito wake unapokuwa na miezi sita au saba.