


***********************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa(TAKUKURU) kwa kushirikiana na chama cha Skauti Mkoani Mwanza wametoa mafunzo kwa Walimu walezi,viongozi wa makundi ya skauti kwa lengo la kuwapatia elimu juu ya mapambano dhidi ya rushwa.
Mafunzo hayo yamefanyika leo hii Machi 30,2022 katika ukumbi wa mikutano uliopo kwenye jengo la Halimashauri ya Jiji la Mwanza.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo Kaimu Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Nyamagana, Innocent Shetui amesema kuwa kupitia mkakati wa Takukuru na skauti( TAKUSCA) wenye kauli mbiu isemayo “Tokomeza rushwa” wametoa elimu hiyo kwa walimu walezi ili wakawafundishe vijana namna bora na mbinu muhimu za kushiriki kwenye mapambano dhidi ya rushwa.
Amesema vijana walioko mashuleni wakiandaliwa vizuri familia,Jamii na Tanzania vitakuwa salama kutokana na kutengeneza kizazi kitakachokuja kutumikia Taifa lisilokubali rushwa.
Nae Kamishina wa skauti Mkoa wa Mwanza Wande Munkyala, amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwa walimu kwani wao ndio wanakundi kubwa la vijana ambao wanatakiwa kuelimishwa ili weweze kukua katika malezi bora ya kupinga rushwa.
Amesema mafunzo hayo ni mpango wa Taifa hivyo amewataka walimu wanaopatiwa mafunzo hayo kuendeleza mpango wa skauti mashuleni ili kuwafichua wanao toa na kupokea rushwa kwani vijana wakianza kufundishwa bado wadogo inakuwa ni chachu ya kuleta mabadiliko na kupandikiza roho ya kuchukia vitendo vya rushwa.
Awali akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala amesema kuwa mafunzo hayo yamekuja muda sahihi kabisa ambapo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu ameelekeza fedha nyingi katika miradi ya ujenzi, hivyo kupitia elimu watakayoipata anaimani watakuwa mabolozi wazuri wa kuielimisha jamii juu ya kuachana na vitendo vya rushwa.