Mtafiti na mgunduzi wa mbegu za Maharage katika kituo Cha utafiti wa kilimo Tari -Selian, Nestory Shida akionyesha unga wa maharage aina ya Jesca wenye virutubisho vya kutosha na unaoongeza nguvu za kiume .(Happy Lazaro)
………………………………………..
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha.Kituo cha utafiti wa kilimo Tanzania Tari -Selian kimefanya utafiti na kugundua aina mbalimbali ya maharage,yakiwemo Maharage aina ya Jesca ambayo yameongezewa viini lishe na yanatumika maalumu kwa ajili ya watoto ,wazee na wagonjwa wanaoishi na VVU.
Hayo yamesemwa na Mtafiti na mgunduzi wa mbegu za Maharage kutoka kituo hicho,Nestory Shida wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja na watafiti kutoka Kanda ya kaskazini ikiwa ni sehemu ya mafunzo kwa vitendo baada ya kupatiwa mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania (COSTECH).
Shida amesema kuwa, Maharage hayo aina ya Jesca ni maarufu Sana kutokana na kiwango kikubwa yaliyonayo kwani yana uwezo mkubwa wa kumwongezea mtoto uwezo mkubwa wa kufikiri huku yakielezwa kuongeza nguvu za kiume kutokana na kiwango kikubwa cha viini lishe kilichopo.
“Unga wa maharage haya yanatumika kwa shughuli nyingi ikiwemo kutengeneza keki,maandazi,na pia unatumika kwa wakina mama wajawazito kwani inawasaidia Sana hasa katika upande wa kuongeza damu ,hivyo nawaomba watumie unga huu kwani una virutubisho vingi Sana kwa afya ya mwili.”amesema.
Amesema kuwa, maharage hayo ya Jesca yana uwezo wa kukomaa kwa muda mfupi tofauti na maharage mengine ambapo yamepata umaarufu mkubwa kutokana na unga wake kuwa na virutubisho vingi ambavyo vina faida kubwa katika mwili wa binadamu.
Amesema kuwa ,mbali na kutoa elimu ya matumizi hayo ya unga wa maharage, wamekuwa wakiwaunganisha wakulima waliopo kwenye vikundi na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wakubwa na kuweza kufanya biashara na kuwa na soko la uhakika ambalo limewezesha kuinua kipato chao.
Shida amesema kuwa,kituo kimekuwa kiungo muhimu katika kubuni, kuendeleza na kuzalisha mazao yenye viini lishe muhimu mfano ,mahindi yenye kiwango kikubwa cha protini ,lishe 1,Lishe 2,na lishe K1,huku kwa upande wa maharagwe yenye kiwango kikubwa Cha madini ya chuma na Zinki-Jescica,Selian 14 na Selian 15.
Amesema kuwa, kituo hicho kimekuwa kikiendesha maonesho ya kilimo biashara kila mwaka kwa kushirikiana na Baraza la Nafaka Afrika Mashariki ambapo kupitia maonesho hayo idadi kubwa ya wakulima wameweza kupata elimu ya kutosha kuhusu kilimo bora za Maharage hayo yenye tija na yanayokomaa ndani ya muda mfupi.
“Kwa kweli kituo hiki kimekuwa msaada mkubwa Sana kwa wakulima kwani wengi wao wameweza kuzifahamu mbegu bora za kutumia ambazo zinazaa kwa wingi na wameweza kupata manufaa makubwa Sana na kuboresha maisha yao.”amesema.