Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza wakati wa majadiliano katika Jukwaa la 8 la Wakuu wa Nchi na Serikali Duniani linalofanyika Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu leo tarehe 30 Machi 2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abudhabi Mohamed Seif Al Suwaidi walipokutana leo tarehe 30 Machi 2022 Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akikabidhi zawadi Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abudhabi Mohamed Seif Al Suwaidi mara baada ya mazungumzo yao leo tarehe 30 Machi 2022 Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu.
********************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amesema bara la Afrika linapaswa kuwa na ushirikiano mkubwa kupitia mkataba wa eneo huru la kibiashara la Afrika ili kufikia maendeleo ya pamoja na haraka wakati huu wa ufufuaji uchumi baada ya madhara ya Uviko 19.
Makamu Rais amesema hayo leo tarehe 30 Machi 2022 wakati wa majadiliano katika Jukwaa la 8 la Wakuu wa Nchi na Serikali Duniani linalofanyika Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Amesema kutoka na Afrika kujaaliwa rasilimali nyingi nchi za Afrika zinapaswa kushirikiana katika miradi itakayoinua uchumi wa bara hilo ikiwemo miradi ya nishati na miundombinu. Aidha ameongeza kwamba bara la Afrika kabla ya Uviko 19 uchumi wake ulikua ukipanda kwa asilimia 3.3 hadi 3.5 pamoja na kupungua kwa kiwango cha umasikini. Ameongeza kwamba nchi za Afrika zitaendelea kuimarisha kilimo cha kisasa ili kupata mazao ya kutosha kufanya biashara ndani na nje ya bara hilo.
Akizungumzia nchi ya Tanzania, Makamu wa Rais amesema serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha uchumi ikiwemo kuchukua hatua za kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi kwa manufaa ya pande zote mbili.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amesema licha ya Afrika kutochagua upande wowote katika migogoro ya siasa za kimataifa bado Afrika inapaswa kuendelea kushirikiana na mataifa nje ya bara hili kwa manufaa ya pande zote husika pamoja na kuheshimiana. Katika nchi za Afrika, Makamu wa Rais amesema migogoro yeyote ya uvunjaji katiba inapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo ili kuepusha madhara zaidi.
Makamu wa Rais amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika jukwaa hilo ambapo
Pamoja na mambo mengine lina lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kubadilishana mbinu za kuimarisha utendaji wa serikali.
Halikadhalika Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa maendeleo wa Abudhabi Mohamed Seif Al Suwaidi ambapo wamezungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano katika miradi inayotekelezwa na mfuko huo nchini Tanzania.