Baadhi ya wadau wa afya wakiwa katika mkutano wa afya ya msingi ya mkoa wa katavi
********************
Na Zillipa Joseph, Katavi
Mdondoko wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika mkoa wa Katavi umeelezwa kuwa mojawapo ya chanzo cha mimba za utotoni kwa watoto wa kike ambao baadae unapelekea kuwa na watoto wenye udumavu
Kwa mwaka 2020 jumla ya wanafunzi wa shule za msingi 3,038 waliacha masomo huku idadi hiyo ikiongezeka kwa mwaka 2021 ambapo jumla ya wanafunzi 4362 nao walikatisha masomo na inaelezwa kuwa asilimia 30 ya watoto hao wanaangukia katika ndoa za utotoni
Akizungumza kwa niaba ya Afisa elimu mkoa katika kikao cha wadau wa Afya mkoa wa Katavi; Afisa Elimu manispaa ya Mpanda Godfrey Kalulu ametaja sababu za mdondoko huo kuwa ni pamoja na matatizo ya kiafya, ambapo mwanafunzi anaeugua mara kwa mara anashindwa kuhudhuria masomo vizuri na hatimaye kuamua kuacha kabisa kwenda shule na umaskini ndani ya kaya
Sababu nyingine ni kuhama hama kwa familia za wafugaji na kuacha kuchukua uhamisho wa wanafunzi na kaya kuishi umbali mrefu na shule hali inayowakatisha tama wanafunzi kuendelea na shule
Kalulu ameeleza kuwa kwa wanafunzi wa shule za msingi mwaka 2013 waliandikishwa wanafunzi 13,457 na mwaka 2019 waliosajiliwa kufanya mitihani ya darasa la saba ni 10,419
Aidha kwa mwaka 2014 walioandikishwa darasa la kwanza walikuwa 17395 na mwaka 2020 waliosajiliwa kufanya mitihani ya darasa la saba walikuwa 12,932
Kalulu ameishauri jamii kuwa na mwamko wa kuwasisitiza wananfunzi kwenda shule pamoja na kujenga shule za bweni katika maeneo yasiyofikika kiurahisi
Mratibu wa afya ya mama na mtoto mkoa wa Katavi Sista Elida Machungwa amesema kwa kipindi cha miezi sita iliyopita jumla ya wasichana 130 walio na umri wa chini ya miaka 18 walifika katika vituo vya kutolea huduma wakiwa wajawazito
‘Idadi hiyo ni kwa wale tu wanaofika katika vituo vyetu, sasa ukitathmini kwa mkoa mzima na wale ambao hawajajitokeza unafikiri hali ikoje?’ alisema Sista Machungwa
Ameeleza kuwa kutokana na wasichana wadogo kuanza majukumu ya kulea watoto kabla ya umri wao hali hiyo inazalisha udumavu kwa watoto wanaowazaa kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya malezi ya mtoto na lishe yake kwa ujumla
Ameongeza kuwa walio wengi wamekuwa wakitelekezwa na wanaume wanaowapa mimba na matokeo yake wamekuwa wakijishughulisha na biashara ndogondogo na hivyo kushindwa kuwalisha watoto wao ipasavyo
Dr. Omar Sukari ni mganga mkuu wa mkoa wa Katavi amewahimiza kinamama wanaohudhuria kliniki kutumia kadi maalum za mahudhurio ya mtoto badala ya daftari kwani kadi ina michoro maalum inayoweza kumtambulisha muhudumu na mama kwa haraka hali ya mtoto kiafya kama inashuka au inapanda
Mratibu wa lishe mkoa wa Katavi Asnath Mrema amewataka maafisa lishe ngazi ya kata kuboresha utoaji wa huduma za lishe kwa jamii, ikiwemo elimu na kutambua kwa mapema watoto wenye utapiamlo mkali
‘Silaha pekee ya kuondokana na tatizo la udumavu mkoani Katavi ni wadau viongozi kufanya kazi kwa pamoja kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa lishe.’ alisema
Magreth Chaya ni Mratibu wa asasi isiyo ya kiserikali ya Niache Nisome amethibitisha kuwepo kwa wasichana wadogo wanaobeba ujauzito na kufika ofisini kwake kwa kuhitaji misaada.
Dokta Justina Tizeba amesema katika vituo vya kutoa huduma ya mama na mtoto ni rahisi kuwabaini watoto wenye utapiamlo kwani wanaonekana kwa macho.
Ameongeza kuwa alifika katika kituo cha RCH cha Town Clinic ambapo aliwaona watoto mia mbili waliofika kwa ajili ya kupima uzito na kupata chanjo kwa siku hiyo na kati yao asilimia hamsini ya watoto walionekana kuwa na utapiamlo wa kawaida na asilimia tano walikuwa na utapiamli mkali
Aidha amesisistiza elimu ya lishe bora mashuleni, misikitini na makanisani na popote kwenye mikusanyiko ili kuondokana na changamoto ya watoto wenye udumavu
Matibabu ya watoto wa lishe yasitegemee tu lishe spesheli bali wazazi/walezi wafundishwe njia mbadala ya kupata lishe kwa watoto ambayo inajumuisha maziwa ya ng’ombe, sukari na mafuta ili kuwasaidia watoto wenye utapiamlo mkali
‘Ni heri kuwafundisha ili kuzuia watoto wasipate utapiamlo mkali kwani motto akifikia hali hiyo atalazimika kukaa naye hospitali kwa zaidi ya siku kumi na nne kabla ya kupata nafuu’ alisema Dk. Tizeba
Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesema mkoa wa Katavi unazalisha vyakula vya kutosha hadi kuuza katika mikoa ya kanda ya Ziwa Viktoria na nchini Kongo DRC hivyo mkoa kuwa na asilimia 33 ya watoto wenye ulumavu haikubaliki
Amewataka maafisa lishe kushirikiana na viongozi wengine katika kufikisha elimu kwa jamii ya lishe bora