*******************
Mwamvua Mwinyi,Pwani
March 28
WATU wawili wamefariki dunia pamoja na kujeruhi wengine wawili ,katika ajali iliyohusisha magari matatu kugongana huko maeneo ya Miwaleni, Halmashauri ya wilaya Kibaha Vijijini mkoani Pwani.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa polisi Mkoani Pwani,Pius Lutumo alieleza, ajali hiyo imetokea march 28 asubuhi.
Alieleza kuwa, gari namba T608 AGV likiwa na tela lenye namba T.317 AQM aina ya scania likiendeshwa na Raymond Kimaro (36) ,mkazi wa Ubungo likitokea nchini Kongo kwenda Dar es salaam ambapo lilihamia upande wake wa barabara na kugonga gari namba T.256 CMF aina ya Noah iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Morogoro.
Alieleza,hali hiyo ilisababisha kontena kuchomoka na kuangukia gari SU 38223 aina ya Toyota land cruiser iliyokuwa ikitokea Dar es salaam kwenda Morogoro ikiendeshwa na Innocent Gerson Mringo na kusababisha vifo na majeruhi hao.
Lutumo alitaja waliofariki dunia kuwa ni profesa Prosper Ngowi (55) mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Na Innocent Gerson (33) mkazi wa Dar es Salaam na dereva.
Majeruhi ni Raymond Kimaro (39) dereva wa lori T.608 AGV na Abdallah Mohammed (33)dereva wa Noah mkazi wa Dar es Salaam na kusababisha uharibifu wa magari.
Kamanda huyo alifafanua, chanzo Cha ajali bado kinachunguzwa hata hivyo uchunguzi wa awali unaonyesha Kuwa ni uzembe wa dereva wa gari aina ya scania kuhama upande wake wa barabara na kugonga gari aina ya Noah na kupelekea kontena kuchomoka na kuliangukia gari Toyota cruiser.
Lutumo alisema, mwili wa marehemu profesa Prosper Ngowi umehifadhiwa hospital ya rufaa Tumbi na mwili wa marehemu Innocent Gerson umehifadhiwa katika kituo cha afya Mlandizi.
Majeruhi wametibiwa na hali zao ni nzuri huku mtuhumiwa akishikiliwa na jeshi la polisi kwa hatua zaidi.
Lutumo aliwaasa madereva kuacha kuendesha pasipo kufuata Sheria za Usalama Barabarani,na wawe makini ili kujiepusha na ajali.