*************************
Mnamo tarehe 27.03.2022 majira ya saa 21:18 usiku huko katika Barabara ya Mbeya – Tunduma, Kata ya Utengule Usongwe, Tarafa ya Usongwe, Wilaya na Mkoa wa Mbeya. Gari yenye namba za usajili T. 909 DQC na tela namba T.205 DSF aina ya Scania likiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina la ABDULRAZACK HASSAN alishindwa kulimudu gari hilo akiwa anashuka mlima Iwambi baada ya kufeli break na kwenda kugonga Bajaji yenye namba ya usajili MC.999 CUD aina ya TVS King iliyokuwa uelekeo mmoja ikiendeshwa na SHUKRANI PAUL na kusababishia majeruhi na kugonga Gari yenye namba ya usajili T.128 ALE aina ya Nissan Double Cabin ikiendeshwa na EMMANUEL MAKONGANYA na kusababisha kifo kwa JEREMIAH MWASENGA ambae alikuwa abiria kwenye gari hiyo, kisha kugonga Gari yenye namba ya usajili T.387 DBD aina ya Toyota Noah iliyokuwa ikiendeshwa na dereva ANYENGULILE MWAMULUKI na mwisho kugonga Pikipiki yenye namba ya usajili MC.205 ARK aina ya T-Better iliyokuwa ikiendeshwa SUSA MBWIGA na kumsababishia kifo.
Katika ajali hiyo watu wawili wamejeruhiwa na wanaendelea na matibabu Hospitali Teule ya Ifisi – Mbalizi. Aidha vyombo vyote vilivyohusika katika ajali hiyo vimeharibika. Chanzo cha ajali ni kufeli breki ya Gari Lori yenye namba ya usajili T.909 DQC/T.205 DSF Scania na kusababisha dereva kushindwa kulimudu Gari hilo. Jeshi la Polisi mkoani hapa nilimshikilia Dereva wa Gari T.909 DQC/T.205 DSF Scania kwa hatua zaidi za kisheria.
KUKAMATA SILAHA NA RISASI KUMI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya mnamo tarehe 28.03.2022 majira ya saa 06:30 asubuhi huko maeneo ya uhindini, Kata na Tarafa ya Sisimba, Jijini Mbeya lilifanikiwa kukamata silaha aina ya Pistol – Liger M80, CAL.9×9 yenye Maker namba B.94554 rangi nyeusi ikiwa na risasi kumi ndani ya magazine na mkasi mmoja mkubwa.
Silaha hiyo ilikamatwa wakati askari wakirudi nyumbani kutokea kazini ndipo walipofika maeneo ya uhindini jirani na duka la wakala mkuu wa M-PESA aitwaye IRENE KAHEMELE waliwaona watu wawili huku mmoja akiwa amebeba begi dogo jeusi mgongoni na kuwatilia mashaka na walipojaribu kuwasogelea walianza kukimbia hali iliyopelekea askari kuanza kuwakimbiza huku akipuliza filimbi kuomba msaada ndipo watu hao walitupa begi hilo na kutokomea.
Katika upekuzi ndani ya begi hilo ndipo ilikutwa silaha moja na risasi 10 ndani ya magazine na mkasi mkubwa mmoja. Jeshi la Polisi mkoani hapa linaendelea na msako wa kuwatafuta watuhumiwa unaendelea.
KUPATIKANA NA NOTI ZIDHANIWAZO KUWA NI BANDIA.
Mnamo tarehe 26.03.2022 majira ya saa 13:30 mchana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko kijiji cha Nsongwi Mantanji, Kata ya Ijombe, Tarafa ya Tembela, Wilaya na Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata FIDELIS KOMBA [42] Mganga wa tiba asilia, Mkazi wa Nsongwi – Mantanji akiwa na noti 219 za Tshs 10,000/= zote zikiwa na namba KL 4105891 na noti 230 za Tshs.5,000/= zote zikiwa na namba HF 4424893 zinazodhaniwa kuwa ni noti za bandia.
Mtuhumiwa kabla ya kukamatwa alitajwa na mtuhumiwa mwenzake aitwaye FERUZ SELEMAN [35] Fundi ujenzi na Mkazi wa majengo mapya Nsalaga ambaye alikamatwa tarehe 25.03.2022 majira ya saa 20:45 usiku huko maeneo ya Isyesye -Madukani, Kata ya Isyesye, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya akiwa na noti bandia 69 za Tshs 5,000 zote zikiwa na namba HF 4424893 hivyo kufanya jumla ya noti 299 za Tshs.5,000/= akiwa katika harakati za kutaka kuziingiza kwa wakala wa mitandao ya fedha kwa nia ya kuzihalalisha fedha hizo na baada ya kuhojiwa kwa kina ndipo alimtaja FIDELIS KOMBA kuwa ndio aliyempa noti hizo. Upelelezi wa shauri hili unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa watu wanaojihusisha na utengenezaji na usambazaji wa noti bandia.