Mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango akikata utepe ishara ya uzinduzi wa mradi wa kilimo endelevu iliofanyika Jijini Arusha
Meneja miradi wa shirika la kibelgiji la Island of Peace (IDP) ,Ayesiga Hiza akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi wa mradi wa kilimo endelevu uliofanyika Jijini Arusha .(Happy Lazaro).
…………………………………………………….
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha.Zaidi ya wakulima 250,000 kutoka halmashauri ya Arusha dc na jiji la Arusha wanatarajiwa kunufaika na mradi wa kilimo endelevu unaolenga kuongezea thamani mnyororo mzima wa kilimo kuanzia kwa mzalishaji hadi mlaji.
Akizungumza wakati wa kuzindua mradi huo Jijini Arusha,Meneja miradi kutoka shirika la Ubelgiji la Island of Peace (IDP),Ayesiga Hiza amesema kuwa, mradi huo ni wa miaka mitano kuanzia 2022 -2026 ambapo unafadhiliwa na Serikali ya Ubelgiji na Ufaransa.
Ayesiga amesema kuwa,mradi huo unalenga kumnufaisha mkulima katika maswala ya kilimo bora chenye tija na kuondokana na kilimo cha mazoea ,namna ya utunzaji wa mazao ili kupata chakula Safi na salama ,usafirishaji na kutatua changamoto ya soko inayowakabili wakulima wengi.
Amesema kuwa,kupitia mradi huo wakulima wataweza kupata mbinu bora ya utunzaji wa ardhi ili iwe bora na yenye rutuba na kutumia kilimo cha ikolojia kinachotunza mazingira kwa ustawi na uchumi wa mwananchi na kuweza kuzalisha mazao mengi zaidi na kuongeza kipato chao.
” zaidi ya asilimia 60 ya ardhi tunayoishi ipo hatarini kuwa jangwa kutokana na kilimo kisichozingatia kanuni bora kutokana na watu kutumia kemikali nyingi na hivyo kusababisha udongo kuchoka , ambapo watapata fursa ya kuweza kujifunza kilimo cha ikolojia ambacho kinazingatia na kuifanya ardhi iendelee kuwa mpya kila wakati na kuweza kutumika vizazi na vizazi.”amesema Ayesiga.
Amesema kuwa, kupitia mradi huo zaidi ya shule 20 zitafikiwa huku lengo likiwa ni kuhakikisha teknolojia hiyo inawafikia wanafunzi wakiwa tangu wadogo ili waweze kutunza mazingira na kulima kilimo chenye tija.
Mkuu wa wilaya ya Arumeru ,Mhandisi Richard Ruyango amesema kuwa, uzinduzi wa mradi huo ,unalenga kuangalia kilimo cha ikolojia kinacholenga kumwinua mkulima mdogo katika kulima kilimo chenye tija na kitakachomwongezea thamani katika mazao yake huku akitunza mazingira.
Amesema kuwa, mradi huo unalenga kuleta matokeo chanya katika upande wa chakula katika kaya zetu sambamba na kutatua changamoto ya kuimarisha mifumo endelevu ya chakula kuanzia kwa mzalishaji hadi kumfikia mlaji.
“Mradi huu ni suluhisho la kuzingatia matumizi bora ya kilimo kwani utasaidia Sana wakulima kuachana na kilimo cha mazoea na kulima kilimo chenye tija ambacho kitamkomboa mkulima katika mnyororo mzima wa thamani.”amesema .
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa shirika linalohusiana na kuweka daraja la teknolojia kwa wakulima wadogowadogo, Dominic Ringo amesema kuwa,mradi huo una manufaa makubwa kwa wakulima kwani unalenga kuangalia namna ya kuzalisha kwa tija hasa katika swala zima la mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema kuwa, kupitia mradi huu kilimo kitafanyika chenye tija kwa kutumia mfumo wa ikolojia ambao unatunza mazingira sambamba na kuendelea kuwepo kwa usalama wa chakula ,huku wakiongeza ubunifu na weledi katika kilimo chao na kuondokana na kilimo cha mazoea.