************************
Na. John Mapepele
Mkurugenzi Mkuu wa Wasafi na Msanii maarufu ndani na nje ya Bara la Afrika, Diamond Platinum amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuwaunganisha wasanii ili sekta ya Sanaa iweze kuwanufaisha.
Diamond amesema haya leo Machi 25, 2022 mbele ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa alipotembelea Kampuni ya Wasafi inayomiliki rebo ya Wasafi, Wasafi TV na Wasafi FM redio kwa lengo la kukagua kazi za Sanaa.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni imefanya mapinduzi makubwa katika sanaa kwa kubuni mikakati mbalimbali ya kuwaunganisha na kuwanufaisha wasanii.
Miongoni mwa mikakati ameitaja mizuri ya Serikali kuwa ni pamoja na kurejesha tuzo za muziki.
Kwa upande wake Mhe. Mchengerwa amesema Serikali imeshatenga fedha nyingi kwa ajili ya kuwekeza kwenye Sanaa ili wasanii waweze kunufaika.
“Nimekuja hapa leo ikiwa ni mwendelezo wa ziara yangu ya kukutana na wadau wa sekta ninazozisimamia ili kuwaunganisha na Serikali yao, nimefurahi kuona wasafi mnaibua vipaji na kutoa ajira kwa wasanii nchini” amepongeza Mhe Mchengerwa
Amesema Serikali itaendelea kuwasaidia wasanii wote bila kuwabagua na kwamba Serikali inathamini mchango mkubwa unaotolewa na wasanii nchini.
Akielezea kuhusu utoaji wa burudani wa vituo vyake Diamond amefafanu kuww vinajitahidi kwenda na teknolojia ya kisasa katika kuendesha vipindi vyenye maudhui ya kuelimisha na kuburudisha jamii.
Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri amepata fursa ya kutembelea na kukagua shughuli za kampuni hiyo na kujionea uandaaji wa vipindi mbalimbali vya michezo na burudani vinavyotangazwa na vituo hivyo.
Mkurugenzi wa vipindi wa Wasafi Nelson Kisanga amesema Wasafi FM imekuwa na vipindi maarufu vya michezo vya Sports Arena na Sports court ambavyo vimekuwa na wasikilizaji wengi.