WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Jenista Mhagama,akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo wa kielektroniki wa tathmini ya hali ya watumishi katika utumishi wa umma unaolenga kubaini mahitaji halisi ya watumishi kwenye Wizara na Taasisi za Umma uliofanyika leo Machi 24,2022 jijini Dodoma.
SEHEMU ya washiriki wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa mfumo wa kielektroniki wa tathmini ya hali ya watumishi katika utumishi wa umma unaolenga kubaini mahitaji halisi ya watumishi kwenye Wizara na Taasisi za Umma uliofanyika leo Machi 24,2022 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Jenista Mhagama,akizindua mfumo wa kielektroniki wa tathmini ya hali ya watumishi katika utumishi wa umma unaolenga kubaini mahitaji halisi ya watumishi kwenye Wizara na Taasisi za Umma uliofanyika leo Machi 24,2022 jijini Dodoma.
………………………………………………
Na Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Jenista Mhagama,amezindua mfumo wa kielektroniki wa tathmini ya hali ya watumishi katika utumishi wa umma unaolenga kubaini mahitaji halisi ya watumishi kwenye Wizara na Taasisi za Umma.
Akizindua leo Machi 24,2022 jijini Dodoma Waziri Mhagama,amesema kuwa mfumo huo utawezesha ukusanyaji, uchakataji na uchambuzi wa taarifa za Watumishi kwa njia ya kisayansi ili kubaini mahitaji halisi ya Watumishi katika Wizara na Taasisi za Umma.
Waziri Mhagama amesema kuwa mfumo huo utasaidia kutathmini hali halisi ya Watumishi waliopo na wanaohitajika katika taasisi zote za umma ili kuwapanga kwa kuzingatia mahitaji halisi ya kila taasisi.
“Kwa kufanya hivyo, serikali itakuwa na taarifa na takwimu sahihi kuhusu watumishi waliopo, mahitaji ya watumishi wanaohitajika katika kutekeleza majukumu ya kuwahudumia wananchi,”amesema Mhagama
Amesema kuwa tathmini hiyo ilianza Januari mwaka huu na lilitakiwa likamilike katikati ya mwezi Februari, 2022, na hadi sasa inaonesha bado Wizara na Taasisi nyingi hazijakamilisha.
“Kwa taarifa tulizonazo mpaka leo kati ya Wizara na Taasisi 427 zilizo kwenye Mfumo wa HCMIS, zote zimeshaanza kutumia Mfumo na zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa zoezi hili na zipo kati ya asilimia 13 hadi 97. “amesema Mhagama
Hata hivyo amesema kuwa taasisi 41 kati ya taasisi 70 zilizo nje ya Mfumo wa HCMIS zimeshawasilisha taarifa zao na sasa wataalam wanachakata taarifa hizo kwa ajili ya kuziweka kwenye Mfumo.
Waziri Mhagama amezitaja Taasisi 10 bora zilizofanya vizuri katika kuingiza taarifa za watumishi wao kwenye mfumo huo kuwa ni pamoja na Shule ya Sheria Tanzania (97%), Tume ya Ushindani (97%), Chuo cha Ardhi Morogoro (97%), Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala (96%) na Ofisi ya Rais Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa (95%).
Ofisi nyingine ni Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa (95%), Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (95%), Mamlaka ya Serikali Mtandao (95%),Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Pori (95%) na Wakala ya Mafunzo ya Menejimenti ya Elimu (94%).
Aidha Waziri Mhagama amewaagiza waajiri wote wawasimamie Wakurugenzi au Wakuu wa Idara/Sehemu zinazosimamia Rasilimaliwatu katika taasisi zao ili wakamilishe zoezi hilo kabla au ifikapo tarehe 31 Machi, 2022.
Amesema kuwa Taasisi ambazo hazitakamilisha zoezi hilo kwa muda uliowekwa zitakuwa zimekiuka maelekezo ya Serikali na hatua stahiki zitachuliwa dhidi yao.
“ Ni imani yangu kuwa, Wakuu wa Taasisi za Umma na watumishi watazingatia maelekezo niliyotoa na yale ambayo yamekuwa yakitolewa kwa ajili ya kulifanya zoezi hili liwe na tija. “ameeleza
Kwa mujibu wa Mhagama, matarajio ya zoezi hilo ni kuweka msawazisho wa Watumishi wa Umma katika taasisi za Umma huku akisema,kwa tathmini iliyopo inabainisha kuwa utoshelevu wa mahitaji ya watumishi kwa taasisi za Umma upo kati ya asilimia 52 hadi 90.