*************************
ASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA ZA WIZI WA MAMILIONI YA FEDHA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia MOHAMED HAMIS ALLY [44] Mkazi wa Soweto Jijini Mbeya kwa tuhuma ya wizi wa fedha taslimu shilingi milioni ishirini na siti na laki nane [Milioni 26,800,000/=] kutoka kwa mwajiri wake kampuni ya “Farmers Centre (T) Ltd” inayojihusisha na uuzaji wa pembejeo za kilimo.
Ni kwamba mnamo tarehe 28.02.2022 majira ya saa 14:16 mchana huko maeneo ya mafiati Jirani na kituo cha mafuta cha Infinity Jijini Mbeya mtuhumiwa MOHAMED HAMIS ALLY [44] Mkazi wa Soweto akiwa kazini alikabidhiwa fedha taslimu milioni 26,800,000/= na mwajiri wake kampuni ya “Farmers Centre (T) Ltd” kwa ajili ya kuzipeleka benki akiwa na dereva.
Baada ya dereva kumfikisha benki na kuondoka, mtuhumiwa aliondoka na fedha hizo ambazo alitakiwa kuziweka benki kama alivyoelekezwa na mwajiri wake na kutokomea kusikojulikana.
Taarifa za tukio hili ziliripotiwa Polisi na mara moja Jeshi la Polisi mkoani hapa lilianza upelelezi na kubaini kuwa mtuhumiwa amekwenda jijini Dar es Salaam maeneo ya Ukonga – Mwembe Madafu.
Mnamo tarehe 16.03.2022 majira ya jioni, timu ya makachero ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya ilifanikiwa kumtia nguvuni mtuhumiwa na katika mahojiano alieleza kuwa fedha hizo amezificha nyumbani kwake jijini Mbeya ambapo askari walifika na kufanya upekuzi kwa mujibu wa sheria na ndipo kilipatikana kiasi cha fedha Tshs.Milioni ishirini zikiwa katika mabunda manne.
Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Nitoe wito kwa jamii kuacha tamaa ya kujipatia fedha kwa njia isiyo halali, hivyo tujenge tabia ya kuwa waaminifu kwa waajiri wetu ili kujiepusha na mkono wa sheria. Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya halitamvumilia mtu yeyote ambaye atajihusisha na uhalifu wa aina yoyote na kudhani akiiba au kutenda uhalifu na kukimbia hatapatikana, Jeshi la Polisi lina mkono mrefu, litafika popote na kuchukua hatua dhidi ya mhalifu yeyote.
KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA MAUAJI.
Mnamo tarehe 21.03.2022 majira ya saa 17:00 jioni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Polisi Mkoa wa Songwe lilifanya msako huko Kijiji cha Mwaka – Tunduma, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa EMMANUEL PATSON MWESA [22] Mkazi wa Mwaka – Tunduma aliyekuwa akitafutwa kwa kosa la mauaji ya bosi wake aitwaye ASUMWISYE LUFINGO @ MWAMBONIKE [37] Mkazi wa Isangawana tukio lililotokea mnamo tarehe 02.01.2022 wakiwa shambani.
Ni kwamba mnamo tarehe 02.01.2022 majira ya saa 16:00 mchana huko Kijiji cha Isangawana, Kata ya Matwiga, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, ASUMWISYE LUFINGO @ MWAMBONIKE [37] baada ya kufika shambani kwake kuwatembelea vibarua wake ambao ni mtuhumiwa EMMANUEL PATSON MWESA [22] na mwenzake aliuawa kwa kukatwa panga kichwani. Chanzo cha tukio ni madai ya fedha ya ujira ya kulima shamba. Aidha katika tukio hilo, watuhumiwa waliondoka na Pikipiki ya marehemu yenye namba za usajili MC.776 BES aina ya Fekon.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilianza msako na hatimaye kumkamata mtuhumiwa huko mkoani Songwe. Aidha Jeshi la Polisi mkoani hapa linaendelea na msako wa kumtafuta mtuhumiwa mwingine ambaye walishirikiana katika tukio hili. Aidha mahojiano na mtuhumiwa yanaendelea ili kubaini ilipo Pikipiki ya marehemu waliyoondoka nayo mara baada ya kufanya tukio hilo.
KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA MAUAJI.
Mnamo tarehe 20.03.2022 majira ya saa 13:30 mchana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko Kijiji cha Shitete, Kata ya Iwindi, Tarafa ya Usongwe, Wilaya na Mkoa wa Mbeya na katika msako huo tulifanikiwa kumkamata mtuhumiwa SAFARI ADMIN LUWOLE [43] Mkazi wa Kijiji cha Horongo aliyekuwa akitafutwa kwa kosa la mauaji ya mke wake aitwaye TUMAIN ANTHON [45] tukio lililotokea tarehe 04.02.2022.
Ni kwamba mnamo tarehe 04.02.2022 majira ya saa 07:00 asubuhi huko Kijiji cha Inolo, Kata ya Iwindi, Tarafa ya Usongwe, Wilaya na Mkoa wa Mbeya, TUMAINI ANTHON [45] Mkazi wa Inolo alikutwa ndani ya nyumba yake akiwa amefariki dunia baada ya kupigwa kitu Kizito kwenye paji la uso na mume wake aitwaye SAFARI ADMIN LUWOLE [43] Mkazi wa Kijiji cha Horongo. Chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa kifamilia kati ya marehemu na mumewe (mtuhumiwa).
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilianza msako mara moja na mnamo tarehe 20.03.2022 tulifanikiwa kumkamata mtuhumiwa. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA MATUKIO YA WIZI.
Mnamo tarehe 20.03.2022 majira ya saa 12:00 mchana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko Kijiji na Kata ya Ubaruku, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya na katika msako huo tulifanikiwa kumkamata LUCY ANTHONY MWALONGO [20] Mkazi wa Ubaruku akiwa na mali mbalimbali za wizi nyumbani kwake ambazo ni:-
- Vyombo vinavyotumika majumbani vya aina mbalimbali,
- Nguo aina mbalimbali,
- Kadi ya benki,
- TV aina ya Aborder inch 19,
- Radio aina ya aborder,
- Speaker 02,
- Simu Smartphone 02 aina ya Tecno,
- Plag socket 01, vyote vikiwa na jumla ya thamani ya 900,000/=. Mali zote zimetambuliwa na mhanga aitwaye RAPHAEL EDWARD [34] Mkazi wa Ubaruku. Upelelezi wa shauri hii unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
KUPATIKANA NA MALI YA WIZI.
Mnamo tarehe 22.03.2022 majira ya saa 12:00 mchana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko Kijiji na Kata ya Ubaruku, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa GEOFREY MALIATABU [18] Mkazi wa Ubaruku akiwa na mali ya wizi Pikipiki aina ya Kinglion yenye Chasis namba LZLP900KHH50839 ikiwa imetolewa namba ya usajili huku akiwa hana nyaraka zozote zinazoonyesha uhalali wa kumiliki pikipiki hiyo. Upelelezi wa shauri hili unaendelea ili kubaini mtandao mzima unaojihusisha na wizi, ununuzi na uuzaji wa pikipiki za wizi.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi mkoani Mbeya katika misako limekamata mali mbalimbali za wizi ambazo ni:-
- Pikipiki MC.458 BDY aina ya Boxer rangi nyeusi
- TV Flat Screen tatu aina ya Home Base inchi 43, Aborder mbili inchi 32 na Remote Control moja ya Home Base.
- Simu mbili Smartphone aina ya Samsung S8 na Galaxy A10.