Greyson Mwase na Mwanahamisi Msangi, Dodoma
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa Nchini kuweka utaratibu wa kukutana na wachimbaji wa madini na kutatua changamoto ili kurahisisha utendaji kazi wa Tume ili Sekta ya Madini iendelee kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa.
Prof.Kikula alitoa agizo hilo Machi 24, 2022 kwenye ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Madini kilichofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji za majukumu ya Tume pamoja na kutatua changamoto mbalimbali.
Profesa Kikula alisema kuwa wadau wengi wa madini pamoja na wananchi kwa ujumla wana matarajio makubwa kwenye Sekta ya Madini na kusisitiza kuwa Tume ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ya kuimarisha huduma zake ili wananchi wote waweze kunufaika na wingi wa rasilimali za madini zilizopo nchini.
Ili kuimarisha umoja ndani ya Taasisi, Profesa Kikula alishauri watumishi wa Tume ya Madini kuanzisha mfuko wa kusaidiana wa SACCOS na kuendelea kushirikiana kwa kubadilishana uzoefu kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini.
Aidha, aliwataka watumishi kujiendeleza kimasomo katika fani mbalimbali ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini, na kusisitiza kuwa Tume ya Madini itaendelea kutatua changamoto mbalimbali katika utendaji kazi.
Awali akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba alieleza mafanikio ya Tume ya Madini tangu kuanzishwa kwake mapema Aprili 2018 ikiwa ni pamoja na ongezeko la ukusanyaji wa maduhuli kutoka shilingi bilioni 164 mwaka 2017 hadi shilingi bilioni 528.24 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019-2020.
“Katika mwaka wa fedha 2021-2022 tulipangiwa lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 650 ambapo kuanzia kipindi cha mwezi Julai hadi Februari, 2022 tumekusanya kiasi cha shilingi bilioni 412.27; tumeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha tunavuka lengo lililowekwa ifikapo mwezi Juni mwaka huu,” alisema Mhandisi Samamba.
Alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini 42 na vituo vya ununuzi wa madini 75 ambayo yamerahisisha kwa kiasi kikubwa usimamizi wa biashara ya madini, ongezeko la kasi ya utoaji wa leseni pamoja na kaguzi za mara kwa mara kwenye migodi ya madini ambazo kwa kiasi kikubwa zimepunguza ajali zilizokuwa zinatokea mara kwa mara kwenye migodi.