******************
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewataka watanzania kuwa na utamaduni wa kupanda miti ili kutunza mazingira.
Ameyasema hayo katika Siku ya Upandaji Miti Kitaifa na Siku ya Misitu Duniani katika kijiji cha Sagani Wilayani Magu Mkoani Mwanza Machi 21,2022.
Amesema lengo la siku hiyo ni kuukumbusha umma wa watanzania juu ya umuhimu wa upandaji miti na pia kuendelea kutunza na kuhifadhi misitu kwa ajili ya faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Amesema kutokana na uharibifu wa maeneo mengi ya misitu ya hifadhi bidhaa za misitu zimekuwa adimu na kupelekea bidhaa hizo kupanda bei.
“Natoa wito kwa watanzania waishio Ukanda wa Ziwa Victoria na maeneo mengine kuendeleza kazi ya kupanda miti na kutunza mazingira kwa ustawi wa maisha yetu” Mhe. Masanja alisisitiza.
Ametaja faida za upandaji miti kuwa ni kupata hewa safi, kuhifadhi vyanzo vya maji, kuhifadhi ardhi yenye rutuba, kuzuia mmomonyoko wa udongo na kupata mahitaji kama kuni, mbao nk.
Jumla ya miti 6000 ilipandwa katika Shule ya Msingi Sagani Wilaya ya Magu na kuitaka halmashauri hiyo usimamie utunzaji wa miti hiyo kwa kuimwagilia maji.