***********************
Jumatatu ya tarehe 21 Machi 2022 Miladia inayosadifiana na tarehe ( Mosi / Farvardin 1401) ni siku ya kuanza mwaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsia. Siku hii ambayo hujulikana kama Nairuzi, ni mwanzo wa sherehe za kale na za muda mrefu na matawi yake yameenea katika kona mbalimbali za dunia hadi Afrika Mashariki. Asili ya sherehe za Mwaka Kogwa huko Makunduchi visiwani Zanzibar, ni sherehe hizo za Nowruzi za nchini Iran.
Mbali na Iran, sherehe za Nowruzi hufanyika pia katika Jamhuri ya Azerbaijan, Tajikistan, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Turkmenistan, Albania, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar . Makala yetu itaangazia juu ya kushabihiana kwa sherehe ya Nowruzi nchini Iran na ile ya Mwaka Kogwa inayofanyika visiwani Zanzibar, na hasa katika eneo la Makunduchi, kusini mashariki mwa kisiwa cha Unguja.
Nowruz ni sherehe ambayo imedumu toka zama za kale na ingali inaendelea kuadhimishwa katika nchi mbalimbali duniani. Kwa mujibu wa aghalabu ya ngano za kale na riwaya za kihistoria kuhusu Nairuzi, sikukuu hii ilianzishwa na mfalme Jamshid katika silisila ya tawala za Pishdadi. Jamshid alikuwa mfalme wa nne katika silisila ya watawala wa Pishdadi na anatambuliwa kama muasisi wa sikukuu ya Nairuzi. Jamshid alikuwa mfalme aliyependwa sana na wananchi wake. Inasimuliwa kuwa katika siku zake za utawala, nchi ilifika katika kilele cha utajiri wa mali. Ferdowsi mshairi na malenga wa tungo za hamasa wa Iran katika simulizi yake kuhusu kuibuka Nowruz anasema: “Wakati neema zilipokuwa nyingi katika nchi, Jamshid aliwakusanya maafisa wote wa serikali na kuwashukuru. Mfalme Jamshid aliwashukuru na kuwaenzi waliofanya kazi vizuri tarehe Mosi Farvardin ambayo ilikuwa siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa Hijria Shamsia. Aliitaja siku hiyo kuwa ni siku ya Nowruzi yaani siku mpya ya sherehe”.
Pamoja na kuwa hakuna nyaraka kamili kuhusu historia ya Nairuzi, lakini ni jambo lisilo na shaka kuwa Nowruzi ni sherehe ya kale na ilikuwa ikisherehekewa katika ardhi ya Iran hata kabla ya kuwasili kaumu ya Arya.
Kwa mujibu wa mtafiti Muirani Mehrdad Bahar, Nowruz ni mila na desturi ya kale ambayo ilikuwepo millennia ya tatu kabla ya Miladia (Kuzaliwa Nabii Issa AS). Anaandika hivi: ‘Sherehe hizo zilikuwa zikiadhimishwa na makabila ya asili ya wenye kuhamahama Iran.’ Baadhi ya riwaya za kihistoria zinasema Nowruz iliingia Iran mwaka 538 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa ( AS) baada ya Kourosh kuliteka eneo la Babel. Riwaya hizo zinasema kuwa katika kukaribisha Nairuzi, Kourosh wa Pili alikuwa na mpango maalumu wa kuboresha maisha ya askari wake, kusafisha na kudumisha usafi katika maeneo ya umma na nyumba binafsi sambamba na kuwaachilia huru wafungwa.
Baada ya kuingia Uislamu katika ardhi ya Iran, Wairani Waislamu waliendelea kuadhimisha sikukuu ya Nairuzi lakini kwa kuzingatia mafundisho, mila na desturi za Kiislamu. Katika zama za utawala wa Waseljuki walioanza kutawala Iran katika karne ya 10 Miladia, kulifanyika mabadiliko katika kalenda kuhusu mwaka unaofuata jua yaani mwaka wa Shamsia. Mnamo mwaka 467 Hijria Qamaria sawa na mwaka 1,074 Miladia, Jalaluddin Malik Shah Seljuki aliwataka wanahisabati na wataalamu wa falaki yaani elimu ya nyota akiwemo Omar Khayyam Nishaburi wafanye utafiti juu ya namna ya kuifanyia marekebisho kalenda iliyokuwepo wakati huo. Wataalamu hao waliamua siku ya kwanza ya Nowruz isadifiane na siku ya kwanza ya msimu wa machipuo na ndio maana kalenda ya Iran ikapewa pia jina la ‘Kalenda ya Jalali’ au ‘Maliki’. Kimsingi ni kuwa kalenda hii ilienda sambamba na kalenda ya kimaumbile kikamilifu. Kwa hivyo si tu kuwa Nowruz iko katika siku ya awali ya msimu wa machipuo, bali pia kalenda ya Jalali au Hijria Shamsia inaenda sambamba na misimu yote ya kimaumbile katika eneo hili. Mwaka wa kalenda ya Jalali haurudi nyuma hata siku moja na hii ni kinyume na Kalenda ya Miladia (Gregorian) ambayo baada ya kila miaka elfu 10 huwa na hitilafu ya takribani siku tatu.
Katika msimu huu ambao ndio kwanza umeingia nchini Iran hivi sasa, mimea huonekana ikiwa imechangamka na kunawiri ikiwa ni ishara ya kuwa na nishati na uchangamfu wa hali ya juu ikilinganishwa na vipindi vingine vya misimu ya mwaka. Kwa ufupi mandhari huwa ni ya kijani kibichi hali inayoashiria kufufuka maumbile na kuingia katika uhai mpya baada miti na mimea kukauka katika kipindi cha kipupwe na cha baridi kali. Katika msimu huu, bustani hunawiri kwa maua yaliyochanua kwa rangi tofauti yenye harufu nzuri.
Kwa hakika historia ya Wairani imejaa mafundisho ya kimaanawi ambayo mengi yake yametokana na mfungamano wa kidini wa jamii ya Iran ambao umejaa misingi ya maarifa na kutambua vyema maumbile ya mwanadamu.
Ada nyingine iliyozoeleka baina ya Wairani ambayo hufanywa katika siku za mwishoni mwa mwaka ni usafi wa jumla ambao unajulikana kama “Khane Tekoni”. Katika siku za mwisho wa msimu wa baridi, Iran hutawaliwa na harakati na hali maalumu ambapo watu wote hufanya hima zaidi ya usafi jumla wa nyumba, maeneo ya ibada kama misikitini, vifaa vya nyumbani na hata maeneo ya umma katika bustani, barabara na mitaa ya miji. Usafi huu huwa wa aina yake na hutofautiana na ule usafi wa kawaida na wa kila siku. Bali usafi huu huambatana hata na kubadilisha upangaji wa vitu nyumbani, au hata kuweka mabusati na mazulia mapya na kubadilisha vitu vya ndani ya nyumba kama sofa na mapazia, kununua vitu vipya na kadhalika.
Kwa msingi huo Waislamu wa Iran wanaitambua Nowruz kama siku yenye furaha na baraka na wameiambatanisha na utamaduni wa Kiislamu.
Wakati wa kuingia mwaka mpya wa Kiirani, wananchi wa Iran huomba dua maalumu kwa unyenyekevu mkubwa. Katika lahadha hiyo ya kuukaribia mwaka mpya, Wairani wakiwa wamejikusanya pamoja na familia na jamaa zao, hunyanua mikono na kumuomba Mola Mlezi kwa kusema:
“Ewe unayebadilisha nyoyo na macho ya watu. Ewe Mpangiliaji wa Usiku na Mchana! Ewe Mbadilishaji wa mwaka na hali! Badilisha hali zetu kuwa bora ya hali”.
Moja ya harakati muhimu na yenye ushawishi mkubwa zaidi iliyofanywa na Wairani nje ya mipaka ya taifa hilo katika zama za kale, hasa kwa mtazamo wa kitamaduni wa kiustaarabu, ilikuwa safari ya kihistoria ya kundi la Wairani waliofanya safari kutoka Uajemi hadi eneo la Pwani ya Afrika Mashariki mwishoni mwa karne ya nne Hijiria.
Wairani hao walifanya safari yao hiyo iliyojaa hatari wakati wa utawala wa Al-Buwayh kwa kuanzia Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Hindi, hatimaye kuingia Pwani ya Afrika Mashariki na kufanikiwa kuacha athari zao kubwa katika kukuza mila,utamaduni na ustaarabu kwa wakazi wa maeneo hayo.
Uhamiaji wa Wairani na makazi yao katika maeneo makubwa ya mwambao na visiwa vya Afrika Mashariki, ulipelekea kuanzishwa ufalme unaoitwa Washirazi, uliokuwa na taathira kubwa ya kijamii na kitamaduni, hadi leo hii, licha ya kuporomoka kwa karne nyingi za ufalme huu, mabaki ya athari za kihistoria na kiutamaduni ya Washirazi hao yangali bado yanaonekana katika sehemu mbalimbali za eneo la Afrika Mashariki, na hasa Zanzibar.
Kuwepo kwa maneno mengi ya lugha ya Kifarsi (Kiajemi) katika lugha ya Kiswahili, kuenea kwa usanifu wa majengo wa Kiirani, kama vile Misikiti na majumba mengi ya kale yaliyoachwa na utawala wa Shiraz, kuibuka kwa jamii inayoitwa kabila la Shirazi, ni baadhi ya vipengele hivi vya kitamaduni vya ustaarabu wa Washirazi vinavyoshuhudiwa hadi leo hii visiwani Zanzibar.
SHEREHE ZA MWAKA KOGWA MAKUNDUCHI, ZANZIBAR
Mwaka Kogwa ni mojawapo ya sherehe za mila ya watu wa kale katika visiwa vya Unguja na Pemba, aghalabu sherehe hizi hufanyika mwezi Julai ya kila mwaka. Wenyeji wa visiwa hivyo hupenda kusema sherehe hizi zilianzishwa katika visiwa vya Zanzibar kutokana na mwingiliano wa kitamaduni kati ya wenyeji wa visiwa vya Zanzibar na “Washirazi” watu waliotokea nchini Iran, ambao walihamia, waliishi na kuingiliana na wenyeji wa visiwa hivi.
Mwaka Kogwa ni sherehe ambazo, pamoja na mambo mengine, zinaashiria kuingia mwaka mpya wa Kiswahili. Tarehe hasa ya kuanzishwa kwa sherehe hizi haijulikani. Ila ni sherehe ambazo zimeshakuwepo kama sehemu ya utamaduni na mila za kale za wenyeji wa Zanzibar kwa zaidi ya mamia ya miaka sasa.
Hivi sasa sehemu pekee ambazo sherehe hizi bado zinaendelezwa ni maeneo ya Kisiwa cha Jibondo huko Mafia, Kisiwa cha Kojani kilichoko Pemba pamoja na maeneo ya Makunduchi, kusini mashariki mwa Kisiwa cha Unguja.
Desturi za kusherehekea Mwaka Kogwa kama vile kusafisha nyumba na kutoa vumbi la mwaka jana na kuwasha moto ni mambo yanayolingana na kushabihiana na sherehe ya Nowruz ya Iran, lakini wakati huo huo zimeongezwa baadhi ya mila na desturi za watu wa asili wa Afrika Mashariki.
Sherehe ya Mwaka Kogwa huko Makunduchi imegawanywa katika sehemu mbili, sehemu moja ni ya faragha na sehemu nyingine inafanywa mbele ya umati wa watu. Sherehe ya faragha inafanyika katika sehemu iitwayo “Kae Kuu” yenye maana ya sehemu inayoishi watu, ambapo imeelezwa kuwa watu wa zamani wa eneo hilo waliamini kuwa kuna pango la Mizimu.
Kwa mila na desturi za wananchi wa Zanzibar, shughuli ya faragha hufanyika wiki moja kabla ya kuanza kwa sherehe za hadhara, maovu yote yanayohusiana na mambo ya nyuma yanaondolewa kwa wakaazi wa eneo hilo.
Kama tulivyoeleza hapo awali, Nowruz nchini Iran ni sikukuu yenye historia ya kale mno katika mwambao wa Afrika Mashariki na desturi zake zinafanana kwa kiasi fulani na sherehe zinazofanyika Zanzibar. Hata hivyo, pamoja na kupita kwa mamia ya miaka, Nowruz bado inashikilia nafasi yake kama moja ya sherehe zilizokita mizizi katika visiwa vya Zanzibar na wenyeji wa maeneo haya wanaichukulia kama moja ya mila, utamaduni na desturi zao muhimu.
Hayo yote yanatokana na historia ya kuwepo Washirazi wa Iran katika maeneo ya Pwani ya Afrika Mashariki na uhusiano mwema waliouanzisha kwa kuzingatia udugu,urafiki na usawa, mambo ambayo bado yamebakia ndani ya nyoyo za wenyeji na katika kumbukumbu ya kihistoria visiwani humo na kuendelea kurithishwa kizazi hadi kizazi.
Sherehe za jadi za Mwaka Kogwa kwa kawaida zinaanza asubuhi baada ya kuchomoza jua, wanaume kwa wanawake, huosha miili yao katika maji ya Bahari ya Hindi na kujisafisha na uchafuzi wowote ule. Wanafunzi pia hushiriki katika kuandaa chakula cha sikukuu kuanzia usiku wa kuamkia siku ya sherehe wakiwa na walimu wao mashuleni, na wenyeji hula chakula cha mchana nje ya nyumba zao, ili kuwakaribisha wageni watakaopita karibu na makaazi yao, pia husomwa Qur-ani katika sherehe hizo.
Sherehe hizo zinaendelea kwa kuwashwa moto mkubwa, kuwepo mapigano kati ya watu wa kusini na kaskazini mwa Makunduchi, mapigano hayo yasiyokuwa ya kiadui wala uhasama hutumia makoa ya migomba, lengo ni kuondoa chuki na uhasama wa mwaka uliopita, na kufungua ukurasa mpya wa upendo, umoja mshikamano na amani, na kusahau yote yaliyopita mwaka uliopita. Hali kadhalika, wanawake wa Makunduchi pia hucheza ngoma huku wakiwa wamevaa nguo zao maridadi, hushikilia pembe ya ng’ombe kwa mkono wao wa kushoto, na huvaa kengele ndogo kwenye vifundo vyao vya miguuni. Kwa mila na desturi za wakaazi wa eneo hilo, wanaume hawaruhusiwi kuhudhuria wala kuangalia ngoma hiyo inayochezwa na wanawake pekee.
Sherehe hizi za kusisimua, licha ya kuhudhuriwa na wakaazi wa visiwa vya Unguja na Pemba, hutambuliwa kuwa ni sherehe ya kitaifa, kwani viongozi wa ngazi za juu serikalini hupata fursa ya kuhudhuria kwenye sherehe hizo. Wageni kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania na hata nje ya nchi hualikwa na kushiriki kwenye sherehe hizo za jadi na za kale, ambazo kwa kawaida hufanyika kila unapowadia mwezi Julai.
Hatimaye, mwaka 2009 Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni UNESCO lilitangaza na kuisajili Nowruz kama turathi ya kimaanawi duniani. Aidha Mwaka 2010 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza rasmi tarehe Mosi Farvardin yaani Machi 21 kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nowruz. Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama sikukuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena maumbile. Kwa mujibu wa tovuti ya Umoja wa Mataifa, sikukuu ya Nowruz hueneza thamani za amani na mshikamano wa vizazi katika familia, sambamba na kuleta maelewano na ujirani mwema na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika kudumisha urafiki baina ya watu wa jamii mbali mbali. Katika matini ya kuidhinishwa Nairuzi katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imeandikwa kuwa: “Sherehe za Nowruz zina mizizi ya Kiirani ya zaidi ya miaka 3,000 iliyopita na leo zaidi ya watu milioni 300 huadhimisha siku hii.”