Mwakilishi kutoka Ofisi ya waziri Mkuu Oliver Njogopa (katikati) akizungumza alipokuwa akisoma hotuba ya Ufunguzi wa Mkutano huo katika ukumbi wa Millenium Tower Jijini Dar es Salaam.
Katibu wa Jumuiya ya wanawake na watoto wa SHIVYAWATA Maria Charles akiwa kwenye mahojiano na waandishi wa habari
Wadau mbalimbali waliokuwa wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi. (PICHA NA: HUGHES DUGILO)
*************
Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.
Foundation for Civil Society kwa kushirikiana na Her – Ability Foundation na Shirikisho la watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) kwa pamoja wameandaa mkutano rasmi kwaajili ya kufanya tathimini ya mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika maswala ya jinsia na ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu hapa nchini.
Katika Mkutano huo uliofanyika leo Machi 23-2022 Jijini Dar es Salamaam uliwakutanisha wadau kutoka katika makundi ya watu mbalimbali wenye ulemavu ambapo waliweza kujadili kwa pamoja maendeleo yao yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wa Rais samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari Meneja Idara ya Kujenga Uwezo wa FCS Edna Chilimo amesema kuwa mkutano huo ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani ambapo kila mwaka huwa wanashirikiana na SHIVYAWATA kupitia idara yao ya wanawake na watoto, na kwamba kwa mwaka huu wameona ni vema kukutana ili kufanya tathimini na kupongeza mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo.
“Leo tumekusanyika hapa kwaajili ya kufanya tathimini ya mwaka mmoja wa Mama Samia na hii ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani, tumekuwa tukifanyakazi kwa karibu na SHIVYAWATA kupitia idara yao ya wanawake na watoto na Shirika la Her – Ability Foundation, huu ni mwaka wa nne tumekuwa tukifanya maadhimisho haya, lakini kwa mwaka huu tukasema tayari kuna mambo makubwa yametokea serikalini, Mama amefanya mambo makubwa katika Sekta hii ya watu wenye ulemavu tukasema tukae na kufanya tathimini pana katika yale mazuri, changamoto na pia kuishauri Serikali katika Sekta hii” Amesema Chilimo.
Aidha ameongeza kuwa FCS wameshiriki katika mkutano huo kama wawezeshaji ambao wamekuwa wakitoa ufadhili na ruzuku pamoja na kuzijengea uwezo Asasi za Kiraia na kuhakikisha kuwa yale yote yanayojadiliwa katika mkutano huo yanafika Serikalini na kufanyiwa kazi.
Kwa Upande wake Katibu wa Jumuiya ya wanawake na watoto wa SHIVYAWATA Maria Charles amesema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja cha Rais Samia kumekuwa na mabadiliko makubwa katika sekta zinazoshughulika na watu wenye ulemavu na kwamba wanampongeza Rais kwa kuweza kufanya mabadiliko katika Sekta hiyo na kwamba anaamini changamoto zote zinazowakabili walemavu zitakwenda kufanyiwa kazi.
“Kwakweli Tunampngezaa sana Rais wetu samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa na mafanikio aliyopata katika Sekta hii ya watu wenye ulemavu, tunafahamu zipo changamoto tunazokabiliana nazo zikiwemo vifaa mbalimbali ukizingatia walemavu tupo katika maeneo tofauti lakini kwa ujumla tuna imani kubwa Mheshimiwa Rais ataendelea kuzifanyia kazi changamoto hizo” ameeleza Maria.
Naye Mwakilishi kutoka Ofisi ya waziri Mkuu Oliver Njogopa ameipongeza FCS kwa kuendelea kutoa ufadhili na ruzuku kwa Taasisi za Watu wenye Ulemavu ikiwemo SHIVYAWATA na kwamba ufadhili wao umewezesha Taasisi hizo kutekeleza majukumu yake na kuendelea kuimarishana baina yao na kushughulikia changamoto zao
“Pia niendee kuipongeza FCS kwa elimu mnayoitoa ya kuwajengea uwezo wadau hawa muhimu kaika jamii yetu kwani kwa kufanya hivyo mmekuwa muhimili mkubwa kwa Asasi za Kiraia hapa nchini, pia nawapongeza sana jinsi mnavyofanyakazi na Seikali Hususani Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna ambavyo mnavyosaidia shughuli za watu wenye Ulemavu” amesema Njogopa.