Mkurugenzi mkuu wa TEMDO , Injinia Prof.Frederick Kahimba akionyesha moja ya teknolojia inayotengenezwa katika taasisi hiyo iliyopo eneo la Njiro mkoani Arusha.(Happy Lazaro)
*********************
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha.Taasisi ya uhandisi na usanifu mitambo Tanzania (TEMDO )imebuni teknolojia mbalimbali ikiwemo majokofu ya kuhifadhia miili,vitanda vya kujifungulia wakinamama ,pamoja na viteketeza taka katika hospitali, ambapo watanzania wametakiwa kuchangamkia fursa ya kununua teknolojia hizo zinazozalishwa hapa nchini badala ya kuagiza nje ya nchi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi mkuu wa TEMDO,Injinia Prof. Frederick Kahimba wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kwa lengo la kujionea teknolojia mbalimbali zinazotengenezwa ikiwa ni sehemu ya mafunzo kwa vitendo kwa waandishi waliopatiwa elimu namna ya kuandika habari za Sayansi na teknolojia yaliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH).
Injinia Kahimba amesema kuwa, wamekuwa wakitengeneza teknolojia mbalimbali kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi huku wakisaidia kuondoa gharama ya kwenda nje kuagiza teknolojia hizo nje ya nchi kwani asilimia 80 ya vifaa vya hospitali vinatoka nje ya nchi .
“Kuna teknolojia nyingi zinaagizwa nje ya nchi ambapo uwepo wa Taasisi hii umeleta fursa kubwa kwa watanzania kuagiza teknolojia hapa nchini na kuondoa gharama za kuagiza nje ya nchi kama ilivyokuwa hapo awali,ambapo imeweza kuongeza chachu ya wengi wao kuanzisha viwanda vidogo vidogo na kuweza kujiajiri.”amesema.
Ameongeza kuwa,wameweza kuja na teknolojia hizo za majokofu ya kuhifadhia miili ,pamoja na vitanda vya kujifungulia wanawake ambapo tayari wameshapata oda kutoka hospitali mbalimbali ambao wapo tayari kuchukua vitanda hivyo ambavyo vimetengenezwa katika ubora wa hali ya juu.
“Tumekuwa tukifanya utafiti na usanifu kabla ya kutengeneza teknolojia hizo sambamba na kutoa elimu na msaada wa kitaalamu katika sehemu katika viwanda vinavyoendelea ili waweze kupata elimu zaidi namna ya kutumia teknolojia hizo na kuweza kuzalisha kwa wingi “amesema Injinia Kahimba.
Ameongeza kuwa,wameweza kubuni teknolojia kwa ajili ya kukamua alizeti ,zabibu,chikichi ,na kiteketeza taka katika mahospital ambacho kinateketeza bila kutoa harufu na kuchafua mazingira .
“Tunashukuru Sana Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) kwa kutuwezesha fedha za kufanya utafiti kiasi cha shs 128 milioni ambapo Kati ya fedha hizo tumeweza kutumia kiasi cha shs 65 milioni kwa ajili ya kutengeneza mtambo wa kusafisha mafuta ya alizeti ambao una uwezo wa kusafisha Tani moja kwa siku.”amesema Injinia Kahimba.
Hata hivyo mbali na mtambo huo pia wameweza kutengeneza mtambo mdogo wa kuchakata miwa kwa ajili ya sukari kwa ajili ya wajasiriamali wadogo ambapo ina uwezo wa kuchakata Tani kumi ya miwa na kuweza kupata tani moja ya sukari ndani ya lisaa limoja.
Aidha Injinia Kahimba ametoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa na kuwa na tabia ya kununua teknolojia zinazozalishwa hapa nchini badala ya kuagiza nje ya nchi ili kuweza kuchangia pato la Taifa na kuongeza idadi ya ajira kwa wananchi wetu kwa kutumia teknolojia hizo.