………………………………………………………..
Mwaka mmoja wa utawala wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, umekuwa ni mfano mzuri wa uongozi imara na kielekezo cha mabadiliko chanya ya uchumi, vitu ambavyo vimepelekea kuchochea mageuzi ya kiuchumi nchini.
Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, sekta ya benki Tanzania imeendelea kuwa imara, salama, tulivu na yenye faida ya kutosha kutokana na mazingira wezeshi ya uchumi kiujumla.
Sekta ya benki ilishuhudia kukua kwa mizania kwa asilimia 24% ndani ya mwaka mmoja hadi kufikia jumla ya mali ya shilingi 38.7 Trillioni, kiasi ambacho ni rekodi kwenye sekta.
Kwa upande wa faida, kutokana na kasi madhubuti ya mapato, pamoja na kuimarika kwa ubora wa mikopo, benki zote nchini zilipata faida kabla ya Kodi ya Mapato ya jumla ya Shilingi 1.04 Trillioni.
Kama kinara wa huduma za kibenki nchini, Benki ya NMB imenufaika kwa kiasi kikubwa na mazingira mazuri ya kiutendaji yaliyowezeshwa na utawala wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Benki iliimarisha nafasi yake ya uongozi sokoni kwa kupata faida baada ya kodi ya TZS bilioni 289, ongezeko la asilimia 40 na kuweka rekodi mpya ya kisekta. Utendaji huu wa kipekee ni matokeo ya misingi rafiki ya uchumi kiujumla na Benki ya NMB kuzingatia wateja wake na kuhakikisha wateja na jamii kwa ujumla, wanahudumiwa kwa suluhisho bora za kifedha.
Akiutazama kwa kina mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi Ruth Zaipuna, anasema yafuatayo kuhusu jinsi benki hiyo ilivyonufaika na utawala wa kiongozi huyo mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anatimiza mwaka mmoja madarakani mwezi huu. Tupe mtazamo wako wa utendaji wa Benki ya NMB kwenye mwaka huu wa kwanza wa urais wa Mama Samia?
Mwaka wa kwanza wa urais wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni mfano halisi wa uongozi bora, na matumaini mapya, hasa wakati ambapo dunia inatoka kwenye mlipuko wa janga la Uviko-19 duniani.
Hatua za kisera zilichokuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita dhidi ya janga hilo pamoja na misingi imara ya uchumi kiujumla, kuliuwezesha uchumi wa Tanzania kukabiliana na athari za Uviko-19 mwaka 2021.
Kutokana na hali hiyo, ukiliganisha na majirani zake wa kikanda, uchumi wa Tanzania uliimarika vizuri katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Mheshimwa Samia Suluhu Hassan madarakani.
Kama benki kiongozi nchini, Benki ya NMB ina uhusiano wa karibu na uchumi wa taifa. Mabadiliko makubwa ya ukuaji wa uchumi yanayoendelea yanaonekana na kujitokeza moja kwa moja katika kukua kwa mizania yetu na mazingira chanya ya kimuundo yaliyopo yamesaidia kuchochea ukuaji wetu.
Matokeo yake ni kwamba, katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Mheshimiwa Rais Samia, benki iliweka rekodi ya kisekta ya utendaji kwa kupata faida ya TZS bilioni 420 kabla ya kodi (2020: 301 bln), sawa na ongezeko la asilimia 41. Ukuaji huu mkubwa, ulitokana na ukuaji thabiti wa mapato ya uendeshaji kwa asilimia 18 kulikotokana na ongezeko la mikopo, uwekezaji na ongezeko la wateja kuzitumia zaidi huduma zetu.
Mafanikio yetu kiutendaji mwaka 2021, yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na mazingira mazuri ya uendeshaji nchini ambayo yanachagiza ukuaji wa mikopo ya sekta binafsi, na hivyo kutoa msukumo stahiki kwa ajili ya mizania imara na kuongezeka kwa kasi ya mapato.
Udhibiti wa mlipuko wa Uviko-19 kwa kuchukuliwa hatua muhimu kama kuanzishwa kwa mpango wa chanjo wa taifa, umesaidia pia kuchangamsha matumizi binafsi, hivyo kuchochea shughuli za wateja na kupelekea kuongezeka kwa mikopo binafsi na hii iliongeza kasi ya ukuaji wa mapato yetu.
Soko pia limekuwa na ukwasi wa kutosha hasa kutokana na serikali kuendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati. Amana za wateja wetu zilikua kwa asilimia 25 hadi TZS trilioni 6.4 kufikia mwishoni mwa Disemba 2021 ukilinganisha na TZS trilioni 5.3 Disemba 2020.
Kwa mantiki hiyo, kuboreka kwa uchumi kiujumla chini ya Mheshimiwa Rais Samia kunaipa Benki ya NMB na sekta ya kibenki kwa ujumla matumaini ya kuendelea kufanya vizuri katika kipindi cha muda wa kati.
Mbali ya kutekeleza mpango mkakati wa Benki ya NMB, ni sababu kubwa nyingine zipi zilizochangia ufanisi mkubwa mlioupata katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita?
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Benki ya NMB na sekta ya benki ya Tanzania kwa ujumla iliendelea kuwa imara na yenye mtaji wa kutosha. Katika kipindi hicho, Benki ya NMB ilipata matokeo mazuri kiutendaji na iliendekea kuongoza sokoni, ikiwa na umiliki wa soko wa asilimia 40 kwa upande wa faida. Kwa ujumla sekta nzima ilikuwa na matokeo mazuri ya faida huku mabenki makubwa kwa pamoja yakipata faida ya TZS bilioni 715.
Utendaji madhubuti wa sekta nzima ni matokeo ya ukuaji thabiti wa mapato na kupungua kwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya mikopo isiyolipika yaani mikopo chechefu. Wigo wa huduma za kibenki za kidijitali unaendelea kupanuka ukichochewa na kuongezeka kwa huduma jumuishi za kifedha na kiwango cha matumizi ya mtandao.
Kufuatia janga la Uviko-19, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilichukua hatua kadhaa za kisera kuiimarisha sekta ya benki kwa kuboresha mazingira ya biashara na ufanisi katika utoaji wa huduma za fedha. Hatua hizo ni pamoja na kupunguza kiwango cha sehemu ya amana za mabenki kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu (SMR) na kurahisisha marejesho ya mikopo ili kuongeza ukwasi sokoni na kuchochea kukua kwa mikopo ya sekta binafsi.
Kwa muktadha huo, uhimilivu na kukua kwa sekta kunatokana na mchango wa utekelezaji wa sera wezeshi ya fedha pamoja na hatua madhubuti zilizochokuliwa na BoT kwa ajili ya kuboresha mazingira ya biashara na ufanisi wa kutoa huduma za kifedha. Kama mshiriki muhimu sokoni, tulizitumia baadhi ya hatua hizi wezeshi kuhakikisha tunaendelea kuwaunga mkono wateja wetu katika kipindi cha janga la Uviko-19.
Benki ya NMB pamoja na sekta nzima, inategemea kuendelea kukua kutokana na kuzidi kuchukuliwa kwa hatua wezeshi za kisera ambazo zinalenga ukuaji endelevu wa uchumi wa muda mrefu na kuongezeka kwa mikopo ya sekta binafsi.
Hivi karibuni Benki ya NMB ilitangaza kuanza kuwakopesha wadau wa sekta ya kilimo kwa riba isiyozidi asilimia 10. Je, hatua hii inahusiana kwa namna yoyote ile na sera elekezi ya hivi karibuni kuhusiana na kuwakopesha wakulima?
Katika kutambua majukumu yetu ya kuwa chombo cha ustawi endelevu wa kijamii na kiuchumi nchini, NMB imejijengea historia ya muda mrefu ya kukichangia kilimo na sekta zinazohusiana na shughuli za kilimo kukua. Na bado tunaendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta hizi kupitia huduma na bidhaa mbalimabli.
Katika mwaka huu mmoja, tuliendelea kukiangazia na kukichangia kilimo, ambapo mwezi Oktoba mwaka jana tulikuwa benki ya kwanza kutenga shilingi bilioni 100 kwa ajili ya mfuko maalum wa kuwakopesha wadau wa mnyororo wa thamani wa kilimo kwa riba isiyozidi asilimia 10.
Benki imechukua hatua hii ili kuimarisha zaidi upatikanaji wa mikopo, kupunguza pengo la mikopo kwenye kilimo, kukuza ukuaji endelevu wa sekta, kuongeza tija kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo na kuchochea upatikanaji wa ajira.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1997, Benki ya NMB imeshiriki kikamilifu kwenye ajenda ya maendeleo ya taifa na inaendelea kuunga mkono matarajio ya ukuaji wa uchumi wa nchi. NMB pia imekuwa mchangiaji mkubwa wa sekta muhimu za uchumi wa taifa pamoja na kuwa mshiriki mkubwa wa ajenda ya huduma shirikishi za kifedha.
Benki ya NMB imedhamiria kuendelea kuunga mkono juhudi za serikaki za kukiendeleza kilimo na ajenda nzima ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kupanua wigo wa mikopo.
Wapi unaiona Benki ya NMB miaka mitano ijayo kama mazingira mazuri ya biashara yaliyopo sasa hivi yatadumishwa na kuendelea kuwepo?
Tukizingalia siku za usoni, Benki ya NMB ina matumaini na safari iliyo mbele yetu na tutaendelea kujikita katika kuzifungua fursa lukuki zilizopo sokoni na kutumia misingi imara ya benki kutengeneza thamani zaidi na ustawi wa pamoja kwa wanahisa wetu.
Kipaumbele chetu ni kutekeleza mpango wetu wa muda wa kati (Medium-Term Plan – MTP). Pia tutaendelea kuitumia misingi yetu imara ambayo ni pamoja na mizania madhubuti, viwango bora vya mtaji, mtandao mpana wa matawi na uwezo wetu wa kidijitali ili kuendeleza matamanio yetu ya kibiashara.
Tutaendelea pia na ajenda ya huduma jumuiishi za kifedha na kuwapa wateja wetu suluhisho za kifedha za viwango vya juu kabisa. Tunapoelekea katika nusu ya pili ya mwaka 2022 na miaka ijayo, tumedhamiria pia kuendelea kuzalisha matokeo mazuri kwa wanahisa wetu na tunatarajia kuendelea kwa namna ya kipekee kuwahudumia wateja wetu na kuzisaidia jamii.