Mkuu wa Wilaya ya Magu ya Magu, Salum Kalli,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)jana ofisini kwake kuhusu miradi ya maendeleo iliyotekelezwa ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan, madarakani.
…………………………………………………….
NA BALTAZAR MASHAKA,Magu
WILAYA ya Magu,imeanika mafanikio lukuki ya mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan, baada ya kutekeleza miradi ya maendeleo na kijamii inayolenga kuwanufaisha wananchi baada ya changamoto na kero zao kutatuliwa.
“Tumejipanga ndani ya mwaka mmoja kazi kubwa imefanyika Magu, Rais Samia,ametupatia fedha sh. 13.214,394.735.19 za miradi ya maendeleo ya sekta zote na hakuna iliyoachwa,tumeona maajabu haijapata kutokea,amewezesha ujenzi wa madarasa 123 kujengwa kwa sh.bilioni 2.4,Magu tusingeweza kwa makusanyo yetu sh.bilioni 2 kwa mwaka,”alisema Kalli.
Alisema iko miradi mingi ilikwama kwa miaka 14 bila kukamilika imekwamuliwa na kukamilika kwa sh.milioni 629 za mapato ya ndani na kuitaja miradi hiyo kuwa ni zahanati 14 na vituo vya afya Kahangara na Kabila,madarasa 37 ya shule za msingi 10, ujenzi wa shule sekondari tatu na ofisi mbili za walimu.
Mapato hayo ya ndani pia yametumika kujenga hosteli ya Ng’aya sekondari, matundu ya vyoo ya shule za msingi na Mwalo wa Nyakasenge,ukarabati wa uwanja wa Red Cross Kisesa,kulipa fidia na matengenezo ya stendi ya magari Kisesa ambapo sh.milioni 171.7 kati ya sh.milioni 629 za mapato hayo zimewezesha mikopo kwa vikundi 25 vya wajasiriamali wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.
Kalli alisema katika uendeshaji wa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari walipokea sh.bilioni 1.5 na pia walipokea kutoka Mfuko wa Jimbo fedha za kuchochea shughuli za maendeleo sh. milioni 60.8.
Alisema kuwa uwezeshaji wa utoaji wa huduma za afya katika Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo,walipata sh. milioni 19 kutoka Mfuko wa Pamoja wa Afya, kwa upande wa hospitali ya wilaya,ilipata sh.milioni 43.9,vituo vya afya sh. milioni 39.06 na zahanati sh.milioni 28.3.
Mkuu huyo wa wilaya alieleza kuwa wanajenga jingo la mama na mtoto kituo cha afya Kisesa kwa sh. milioni 400,nyumba ya mtumishi katika kituo cha kutolea huduma sh. milioni 90 na uhamasishaji chanjo ya corona sh.milioni 50.
Pia mafanikio mengine uwezeshaji wa kaya zenye maisha duni kupitia mpango wa TASAF walengwa 5,569 walilipwa sh. milioni 600.5 huku upande wa elimu ya sekondari kupitia miradi ya SEQUIP sh.bilioni 3 zitawezesha ujenzi wa shule moja ya kitaifa huku ujenzi wa shule mbili mpya za Kata za Magu Mjini na Buhumbi ukigharimu sh. milioni 940.
“Serikali kuu imetoa fedha sh. milioni 788.09 kukamilisha jengo la halmashauri na ununuzi wa gari,tozo ya mawasiliano sh. 300 kati ya hizo sh.milioni 250 zimekarabati na kuboresha miundombinu ya Kituo cha Afya Shishani na sh. milioni 50 zimekamilisha madarasa 4 ya shule ya Sekondari Misungwi,”alisema Kalli.
Alieleza kuwa miradi ya kijamii ya kuboresha huduma za afya,maji na usafi wa mazingira sh.milioni 532.5 zilitolewa na serikali kuu ambapo RUWASA umetumia sh.bilioni 1.9 kuboresha mitandao ya usambazaji wa maji vijijini,vijiji 4 havikuwa na huduma hiyo vimefikiwa na TARURA imeboresha miundombinu ya barabara kwa milioni 13.8.
Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Magu,Moza Alli Abdallah,alisema kinaridhishwa na miradi ya maendeleo kwenye sekta zote ili kuwanufaisha wananchi pia kwa namna Ilani ilivyotekelezwa na serikali iliyokabidhiwa ilani hiyo na kuwataka watendaji kusimamia miradi kwa weledi wananchi wanufaike zaidi.
Alisema CCM itaendelea kuisimamia serikali itekeleze miradi na kuhakikisha fedha zinazotolewa zinafanya kazi iliyokusudiwa na Chama kinazifuatilia zilete tija na kumpongeza Rais Samia kwa utendaji wake uliotukuta na kuwezesha miradi mingi kutekelezwa wilayani Magu.