*********************
Na Mwandishi wetu, Busanda
MBUNGE wa Jimbo la Busanda Mkoani Geita, mhandisi Tumaini Bryceson Magessa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha maendeleo mengi Jimboni kwake Busanda kwa kipindi cha mwaka mmoja cha Urais wa Mama Samia.
“Mimi Eng. Tumaini Bryceson Magessa, Mbunge wa Jimbo la Busanda (Geita), kwa wimo wa moyo mkuu, unyenyekevu na heshima, ninayo furaha kubwa kuchukua nafasi hii kukupongeza kwa dhati, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (Chief Hangaya), kwa kutimiza mwaka mmoja tangu uingie madarakani,” amesema.
Pongezi zangu hizi kwako Rais Samia, zinaambatana na heko kwa mambo mengi makubwa uliyofanya katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wako!
Mhe. Rais Samia, ulianza kwa kuendeleza miradi iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano, ambayo wewe ulikuwa sehemu yake, hivyo miradi hiyo inakuhusu moja kwa moja kama mshauri mkuu wa aliyekuwa Rais wa Awamu hiyo, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Busanda, ninaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, chini yako wewe Jemedari mpambanaji, Rais Samia, kwa kutoa zaidi ya Shilingi Billioni 1, kugharamia miundombinu ya barabara, chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).
Fedha hizo, zimefanya kazi kubwa katika sekta hiyo, na hivyo kutatua kero za wananchi wengi wa Jimbo la Busanda, kwani ukweli ni kwamba bajeti ya fedha ya asilimia 30 kwa Tarura, haikuwa ikikidhi matengenezo ya barabara, hususan kwa majimbo makubwa kama Busanda, asante sana Mama, Rais Samia Suluhu Hassan. Najua kabisa, haupendi sifa za bei nafuu (Cheap Compliments), lakini kwa uhalisia huu, nivumilie tu nitoe ya moyoni!
Amesema kama mwakilishi na Msemaji Mkuu wa shida za wananchi wa Jimbo la Busanda, ninatoa shukrani za dhati kabisa kwa mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa, ambao ulikuwa wa kitaifa, hivyo kuwezesha wanafunzi wote walifaulu kujiunga na Kidato cha Kwanza kuripoti shuleni kwa wakati mmoja, bila kusubiri chaguo la pili (Second Selection).
Jambo ambalo halikuwahi kutokea kabla, pamoja na wale wa Darasa la Kwanza!
“Ipo pia miradi mingi mikubwa, tunayoendelea kuipokea wananchi wa Jimbo la Busanda, chini ya Serikali yako, katika kuwezesha sekta mbalimbali za huduma za kijamii. Asante sana Mama, Rais Samia Suluhu Hassan,”.
“Binafsi kama Mbunge mpenda maendeleo, ninakubaliana moja kwa moja na taarifa zilizowasilishwa na wizara mbalimbali, kupitia mawaziri husika juu ya mafanikio ya mwaka mmoja wa uongozi wako kwa kipindi cha mwaka mmoja, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhusiano na mataifa mengine, jambo ambalo linachochea maradufu ukuaji wa uchumi,”
Mwisho, anawasihi wananchi wenzake wa Jimbo la Busanda na Watanzania kwa ujumla kumuunga mkono Rais Samia katika jitihada zake za dhati ambazo amezionesha katika kuijenga Tanzania, kwa kufanya kazi kwa bidii, kuwa wazalendo na kulipa kodi kwa wakati.
Amesema mambo ambayo kwa pamoja yatatufikisha mbali kiuchumi na maendeleo ya mtu mmoja mmoja na kama Taifa kwa ujumla.
“Hongera sana Mama, Rais Samia kwa juhudi na jitihada kubwa ambazo umezionesha, tangu upokee rasmi kijiti, mnamo Machi 19, 2021 baada ya kula kiapo cha kulitumikia Taifa letu, kama Rais na Amiri Jeshi Mkuu,”.
Amesema wananchi wa Busanda wapo pamoja na yeye, katika utekelezaji wa maono ya Rais Samia ya kupaisha Tanzania kiuchumi.
“Mhe. Rais, hamasa ya kuendelea kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Uviko, inaendelea Jimboni Busanda kwa kutoa elimu ya umuhimu wa kuchanja na kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi hayo,” amesema.
Amesema pia, wananchi wanasisitizwa kutoa ushirikiano katika zoezi la Anwani za Makazi, kwa ajili ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, linalotarajiwa kufanyika kote nchini, Agosti 25, mwaka huu!
“Sisi wananchi wa Busanda, tunakuombea kwa Mungu afya njema na maisha marefu, ili uweze kutufikisha mahali ulipolenga kwa maono yako. Kila la kheri, Rais Samia, Chief Hangaya. ‘Unaupiga mwingi’ sana Mama!