NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu,imeipongeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa usimamizi mzuri wa mradi wa Daraja la J P.Magufuli na kuishauri serikali kuweka vipengele vitakavyowabana wakandarasi pindi inapoingia mikataba ya miradi mipya,ili kuwasaidia wananchi wa eneo husika kunufaika.
Pia ihakikishe inamsimamia kwa umakini mkubwa mkandarasi wa mradi huo unaojengwa na kukatisha juu ya maji ya Ziwa Victoria,kati ya vijiji vya Kigongo wilayani Misungwi na Busisi wilayani Sengerema,mkoani Mwanza,ukamilike kwa wakati wananchi wanufaike na kuiepusha serikali kuingia gharama nyingine.
Kamati hiyo ya Bunge ya Miundombinu jana ilitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa km 3,linalojengwa na mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) akishirikiana na China Railway 15 Bureau Group Corporation (CR15G JV)kwa gharama ya sh.bilioni 716.33.
Mwenyekiti wa kamati hiyo,Selemani Kakoso,akizungumza kwa niaba ya wajumbe,alisema serikali inapoingia mikataba ya miradi mipya iwabane wakandarasi watenge fedha kwa ajili ya jamii ili miradi inapokamilika wananchi wabaki na alama ya vitu vya kumbukumbu vitakavyowasaidia.
“Mh.Naibu Waziri,wakikutajia fedha inayokuja kuachwa kwa wananchi hapa ni aibu,kaeni nao wawajengee vitu vya kukumbukwa vitakavyo acha alama, tatukuridhishwa na maelezo ya mkandarasi kuwa hapa Misungwi wanaacha kama milioni 50 tu kwa mradi mkubwa kama huu,” alisema Kakoso.
Alisema hawataki kufanya makosa,miradi yoyote mipya lazima iwekwe mikataba itakayowabana wakandarasi ili waache fedha za miradi ya huduma za jamii,kwenye maeneo husika na wasitengeneze faida yao tu.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu,alisema wamejiridhisha mradi huo wa daraja la J P Magufuli unaendeshwa vizuri kasoro zilizopo ni ndogo ndogo,wakizisimamia utakuwa na tija.
“Tunampongeza Mh.Rais Samia Suluhu Hassan,ameonyesha njia ya kuhitaji kuona miundombinu hii inakamilika kwa wakati kama alivyoahidi,sisi wabunge tunakuja kuona na kuangalia jitihada zinazofanywa na serikali,wizara kwa usimamizi wa kuisimamia TANROADS nayo ikawasimamia wakandarasi,”alisema.
Kakoso aliomba mambo ya kuzingatiwa kwenye mradi huo,ili serikali isiingie kwenye gharama za mara kwa mara,wizara iwasimamie wakandarasi waukamilishe ndani ya muda wa mkataba sababu wengi wanachelewesha kazi wanapoona kuna nyongeza ya mkataba hasa kwenye fedha wanazokuwa wakidai.
Mbunge huyo wa Mpanda Vijijini (CCM)alieleza kuwa serikali imeonyesha utashi na kuwasistiza watendaji wawasimamie wakandarasi wamalize kazi kama walivyokubaliana kwenye mkataba.
Aidha kamati hiyo imefurahishwa kuona Watanzania wanashirikishwa kwenye mradi huo wa Daraja la J P. Magufuli na kuiagiza serikali iangalie maslahi yao walipwe kwa mujibu wa sheria za nchi,usalama na mazingira yao yaboreshwe kulingana na ukubwa wa mradi.
Kakoso aliongeza katika eneo hilo ili kazi iwe endelevu,wazawa hao watambuliwe na waandaliwe mazingira ya kufanya kazi maeneo mengine,wapewe elimu waje kutusaidia kwenye miradi mingine baada ya huu kukamilika.
Awali Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Rogatus Mativila,alisema mradi huo ni moja ya miradi ya kimkakati ya serikali ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii,utakuwa kichocheo cha kupunguza umasikini,utaharakisha ukuaji wa uchumi wa Kanda ya Ziwa na nchi za Maziwa Makuu.
Pia ni kiungo muhimu kati ya mikoa ya Mwanza na Kanda ya Ziwa,nchi za Maziwa Makuu (Uganda,Burundi, Rwanda na DRC) na umefikia asilimia 42 ambapo mkandarasi amelipwa sh. bilioni 194.46,mhandisi mshauri sh.bilioni 87.5 na bilioni 3.1 za fidia ya wananchi 165 zimelipwa.