Mkurugenzi na mwanzilishi wa kampuni ya Mvomero group Ltd,Jesse Oljange akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea ofisini kwakw kujionea fursa mbalimbali zinazopatikana katika zao la parachichi .(Happy Lazaro).
………………………………………………………
Happy Lazaro, Arusha
Zaidi ya vikundi vya wakulima 271 kutoka kanda ya kaskazini vimenufaika na soko la uhakika la zao la parachichi sambamba na kupatiwa mitambo maalumu kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta ya parachichi.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkurugenzi mwanzilishi wa kampuni ya Avomero group Ltd iliyopo Njiro,Jesse Oljange wakati alipotembelewa na waandishi wa habari katika kujionea shughuli hizo ikiwa ni sehemu ya mafunzo yaliyotolewa kwa waandishi wa habari yaliyolenga kuandika habari za Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) .
Amesema kuwa, kampuni hiyo imekuwa ikiwasaidia wakulima wa zao la parachichi kuwa na soko la uhakika baada ya kuwapatia elimu namna ya kuzalisha mafuta hayo kupitia mitambo waliyowafungia na mafuta hayo kuweza kutumika kwenye nywele .
“Wakishavuna parachichi wanazalisha wenyewe kutokana na elimu tuliyowapatia na baadaye tunanunua hayo mafuta kwao ambayo hutumika kwenye nywele ,hivyo wakulima wengi wameweza kuwa na soko la uhakika kupitia teknolojia hizo tulizowafungia”amesema.
Ameongeza kuwa, ni wakati sasa wa wakulima kuchangamkia fursa hiyo ya kuwa na soko la uhakika la parachichi kwani mbali na kutumika Kama matunda yana uwezo mkubwa wa kuzalisha mafuta mazuri ambayo hayana kemikali yoyote na yanaweza kutiba magonjwa ya mba n.k.
“Tunawashukuru Sana COSTECH kwa namna ambavyo waliweza kutufadhili kwa mara ya kwanza na kuweza kuendeleza teknolojia hii ambayo imeweza kuwafikia wakulima wengi ambao wamenufaika na kuwa na soko la uhakika la mazao hayo.”amesema.
Ameongeza kuwa, wamekuwa wakitoa elimu juu ya teknolojia hiyo kwa vikundi mbalimbali vya wakulima pamoja na kuingia mkataba na vikundi hivyo kwa ajili kufanya biashara hiyo .
“Pamoja na mafanikio mbalimbali wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya uhitaji wa matanki makubwa kwa ajili ya kuhifadhi mafuta hayo ili yauzwe mwaka mzima , huku changamoto nyingine ni soko kuhitaji mafuta mengi kuliko uzalishaji uliopo,hivyo tunaendelea kufanya juhudi zaidi katika kuhakikisha uzalishaji unaongezeka kila siku.”amesema Jesse.