Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Remedius Emmanuel akishiriki kwenye zoezi la kufyeka nyasi katika Hospitali la Rufaa Mkoa wa Dodoma, usafi ambao uliandaliwa na UVCCM Tawi la Kizota Relini Mkoani Dodoma ikiwa ni kama kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan haswa kwenye sekta ya afya.
Baadhi ya Wanachama kutoka UVCCM Tawi la Kizota Relini wakifanya usafi kwenye maeneo ya Hospitali la Rufaa mkoa wa Dodoma ikiwa ni kama kuunga mmkono juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake hasa kwenye sekta ya afya.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Remedius Emmanuel akimkabidhi sabuni pamoja na taulo za kike mmoja kati ya wagonjwa waliolazwa kwenye kwenye wodi ya wazazi katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Remedius Emmanuel (kulia) akipokea risala kutoka kwa Mwenyekiti wa UVCCM Tawi la Kizota Relini Irine Sangautwa (kushoto) baada ya kumaliza zoezi la kufanya usafi na kuwapatia wagonjwa baadhi ya mahitaji.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma Baraka Mponda akizungumza na wana UVCCM Tawi la Kizota Relini baada ya kutembelewa hospitalini hapo ambapo aliupongeza uongozi wa UVCCM Tawi la Kizota Relini na serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele sekta ya afya.
…………………………………………………….
Na Bolgas Odilo-Dodoma
UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Tawi la Kizota Relini limeadhimisha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kufanya usafi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kutoa msaada wa taulo za kike na sabuni kwa wagonjwa waliolazwa kwenye jengo la idara ya magonjwa ya wanawake.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa shughuli hizo Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Remedius Emmanuel aliwapongeza vijana hao kwa kuamua kumuunga mkono Rais Samia kwa kazi anazoendelea kuzifanya hasa kwenye kipindi chake cha mwaka mmoja akiwa madarakani.
“Ni mwaka mmoja wa uongozi wa serikali ya awamu ya sita chini ya kiongozi wetu Rais Samia na jambo hili mnalolifanya sidhani kama watu wengi wamefanya, na ni ishara tosha ya kushukuru kwa yale yote ambayo Rais ameyafanya katika kipindi chake chote cha uongozi,” alisema.
Emmanuel ambaye alikuwa anamuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Antony Mtaka alisema, misingi ya kujenga chama na serikali inaanzia katika ngazi ya tawi na shina.
Kwa Upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Baraka Mponda aliishukuru serikali inayoongozwa na CCM kwa jitihada zake ikiwemo kuhakikisha inaboresha huduma za afya katika hospitali zote nchini.
Alisema wataendelea kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wagonjwa wanaokuja katika hospitali hiyo ikiwa ni kama jitihada za kumuunga mkono Rais Samia katika utendaji kazi wake kwa Watanzania.
“Sisi ni watumishi wa umma ambao tumeajiriwa na serikali ya CCM tumefurahi leo tumekuja kutembelewa na waajili wetu ambao ni wana CCM tumefurahi na tunatambua mchango wao katika kulijenga taifa,” alisema.
Awali akisoma Risala Mbele ya Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa UVCCM Tawi la Kizoto Relini Irine Sangautwa alisema tangu Rais Samia alipoingia madarakani amekuwa ni mfano wa kuigwa katika kuendeleza na kukuza uchumi wa nchi.
Aidha, Sangautwa alisema kuwa Rais Samia amekuwa ni kiongozi anayejali sekta ya elimu, utalii, sanaa na michezo hivyo kama vijana kuna haja ya kuendelea kuunga mkono jitihada hizo.
“Kwa kuona hilo vijana wa kata ya kizota relini kwa nia safi kabisa tunapenda kwenda pamoja na mama kwa kauli mbiu isemayo “kizota mpya na vijana wenye lengo la kupinga vita madawa ya kulevya, kutoa elimu ya afya, kuinua elimu, michezo, sanaa na utamaduni,” alibainisha.
Naye Katibu wa UVCCM Tawi hilo Ibrahim Hashim alisema Kizota Relini imekuwa ikifanya vizuri katika michezo ikiwemo mpira wa miguu, na pete hivyo wameadhimia kuzindua timu ya chipukizi football club ikiwa ni mojawapo ya mafanikio.
Hashim alitaja changamoto wanazokumbana nazo kuwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya michezo kama Jezi,Mpira na fedha kwaajili ya usajili wa timu.
“Changamoto nyingine ni ukosefu wa mafunzo ya mara kwa mara ya vijana ya UVCCM na ukosefu wa umiliki wa uwanja rasmi wa mpira wa miguu,” alisema.