Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na wazee wa Mkoa wa Kagera wakati akiwa ziarani katika Mkoa huo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akisalimiana na wazee wa Mkoa wa Kagera mara baada ya mazungumzo aliyoyafanya na wazee hao akiwa ziarani katika mkoa huo.
****************************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema serikali ya awamu ya sita inaendelea kushughulikia changamoto za wazee hasa katika sekta ya afya pamoja na ulipaji wa mafao kwa wazee hapa nchini.
Makamu wa Rais amesema hayo alipozungumza na wazee pamoja na viongozi wa dini wa Mkoa wa Kagera ambapo amewahakikishia kuimarishwa kwa madawati ya wazee pamoja na serikali kuanza mchakato wa bima za afya zitakazoondoa changamoto za upatikanaji wa huduma za afya kwa wazee zilizopo hivi sasa.
Makamu wa Rais amewaasa wazee hao pamoja na viongozi wa dini kuendelea kudumisha amani iliopo hapa nchini ikiwa pamoja na kutatua kwa amani migogoro iliopo katika jamii. Amesema wazee wanapswa kuendeleza mila na desturi za nchi hii ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili miongoni mwa vijana. Aidha amewaomba viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa pamoja na viongozi wake ili waweze kupata hekima ya Mungu katika kuwatumikia wananchi.
Kwa upande wao wazee wa mkoa wa Kagera wamemueleza Makamu wa Rais changamoto zinazoukabili mkoa huo ikiwemo kukosekana kwa maadili kwa baadhi ya watendaji wanaosimamia sekta uvuvi hivyo kufanya sekta hiyo kurudi nyuma. Aidha wamesema umefika wakati wa mkoa wa Kagera kupata chuo cha ufundi kitakachosaidia kuinua uchumi wa mkoa huo unaoonekana kukwama kwa muda mrefu.
Halikadhalika wazee hao wamemuiomba serikali kuwaandaa wananchi wa mkoa wa Kagera katika kutumia fursa za kiuchumi ikiwemo ya mradi mkubwa wa Kabanga Nikel utakaotekelezwa katika mkoa huo. Wamsema serikali inapaswa kuusaidia mkoa huo katika kuinua kilimo kutokana na shughuli hiyo muhimu ya kiuchumi kufanyika chini ya kiwango kwa muda mrefu.