Kaimu Meneja miradi kutoka Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na shughuli mbalimbali za kijamii (SOS CHILDREN’S VILLAGES) Kizito Kundamwali akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya afya ya kinywa na meno leo hii Jijini Mwanza .
Mratibu wa afya ya kinywa na meno kutoka Wilaya ya Kwimba Dr Ditrick Kabadi akiendelea kufanya uchunguzi wa meno kwa Mtoto anaelelewa na kituo cha SOS CHILDREN’S VILLAGES leo katika maadhimisho ya siku ya afya ya kinywa na meno
Watoto wa SOS CHILDREN’S VILLAGES wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi katika maadhimisho ya siku ya kinywa na meno
***********************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa huduma za afya ya kinywa na meno wameadhimisha siku ya afya ya kinywa na meno kwa kutoa elimu katika shirika linalofanya shughuli mbalimbali za kijamii( SOS CHILDREN’S VILLAGES).
Mkoa huo umeazimisha siku ya afya ya kinywa na meno leo hii Ijumamosi Machi 19, 2022 katika Makazi ya SOS yaliyopo Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza,ili kupisha maadhimisho ya Kitaifa yatakayo fanyika katika Mkoa wa Ruvuma Machi 20, 2022.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Mratibu wa afya ya kinywa na meno kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Dk. Mary Kiango amesema kuwa maadhimisho hayo yamelenga kuifahamisha Jamii umuhimu wa kutunza afya ya kinywa ili waweze kuzuia magonjwa yasiyoambukiza.
Amesema kuwa wameanza ziara ya kutoa elimu ya kinywa na meno kuanzia Machi 14, 2022 ambapo watu 1525 wamepatiwa elimu hiyo kutoka Shule za msingi, Kiliniki ya Baba,Mama na Mtoto,wagonjwa wa nje,kwenye makazi ya watoto wenye mahitaji maalumu, wazee wasiojiweza pamoja na Kiliniki ya huduma na matibabu kwa wanaoishi na virusi vya ukimwi.
“Katika ziara hiyo tumetoa elimu kuhusu magonjwa ya kinywa na meno, ambayo ni kutoboka kwa meno,fizi kutoa damu, uvimbe unaotokea sehemu ya jino ili wanapoona dalili hizo wafike katika vituo vya afya kwaajili ya uchunguzi”, amesema Kiango.
Kwaupande wake Dk. Ditrick Kabadi ambae ni mratibu wa afya ya kinywa na meno kutoka Wilaya ya kwimba amesema kuwa, ujio wao katika Shirika la SOS ni kufanya uchunguzi wa awali wa magonjwa ya afya ya kinywa na meno, ambapo wamebaini Watoto 80 kuwa na matatizo ya kuoza meno na fizi kutoa damu.
“Tumetoa elimu juu ya kupiga mswaki na matumizi sahihi ya dawa kwa watoto kwani Kuna dawa zao ambazo wakizitumia zinawasaidia katika kuimarisha meno yao”,amesema Kadadi.
Nae Kaimu Meneja miradi kutoka Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na shughuli mbalimbali za kijamii (SOS CHILDREN’S VILLAGES), Kizito Kundamwali ameushukuru uongozi wa Mkoa kwa hatua waliyoichukua ya kutoa elimu ya afya ya kinywa sanjari na kufanya uchunguzi wa meno kwa watoto wanaolelewa katika shirika hilo.
Awali akizungumza katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa huduma za maabara Julius Shigella, amesema kuwa ili Taifa liwe na uchumi ulio imara ni lazima liwe na watu wenye afya njema hivyo ameishauri jamii kuwa na utatatibu wa kufanya uchunguzi wa kinywa mara kwa mara na kupata ushauri wa wataalamu hali itakayosaidia kuondokana na changamoto ya kung’olewa meno