Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo na Makazi Dk.Angelina Mabula na Mkurugenzi wa Shirika la Koica kutoka Korea ambalo limefadhili mchakato wa kurasimilisha ardhi kimila kwa Halmashauri ya Ikungi Kyucheol Eo (katikati) wakimkabidhi kitabu cha mpango wa matumizi bora ya Ardhi ya Kijiji cha Mnang’ana Mwenyekiti wa kijiji hicho Pascal Mdini katika hafla ya utoaji hati miliki za kimila kwa baadhi ya wananchi iliyofanyika wilayani Ikungi mkoani Singida juzi.
Mkuu wa Mkoa Singida Dk. Binilith Mahenge akizungumza katika hafla hiyo katika Kijiji cha Nkwae. |
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Justice Kijazi akitoa taarifa ya mpango wa matumizi bora ya ardhi katika wilaya hiyo. |
Mjumbe wa kamati hiyo , Asia Halamga akizungumza kwenye hafla hiyo. Kushoto ni Mjumbe wa Kamati hiyo Dk. Florence Samizi.
Mjumbe wa kamati hiyo , Asia Halamga akimkabidhi hati Mkazi wa Kijiji cha Nkwae Benjamini Shija.
Wananchi wa Wilaya ya Ikungi wakiwa kwenye hafla ya kukabidhiwa hati hizo.
Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakikabidhiwa hati.
Na Dotto Mwaibale, Singida
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo na Makazi Dk.Angelina Mabula ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa kufanikisha Mpango wa Matumizi ya Ardhi pamoja na upimaji ardhi wilayani humo.
Dk.Mabula alitoa pongezi hizo katika hafla ya utoaji hati miliki za kimila kwa baadhi ya wananchi iliyofanyika wilayani Ikungi mkoani Singida juzi na kuhudhuriwa na mamia ya watu.
“Niipongeze halmashauri ya wilaya ya Ikungi kwa kufanikisha mpango huu wa kutoa hati miliki za kimila kwa wananchi ambapo leo tunashuhudia hati 5050 zikitolewa ili ni jambo zuri la kuigwa na halmashauri nyingine” alisema Mabula.
Aidha Dk. Mabula alishuhudia wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii wakitoa hati 54 kwa wananchi wa vijiji vya Ntondo na Nkwea vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Singida huku wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Ally Makoa.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa hati hizo Makoa alisema, kazi ya upangajii iliyofanywa na wizara ya ardhi kupitia mradi wa KKK unatimiza kiu na matarajio ya Wizara pamoja na ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Aidha, Kamati hiyo imempongeza pia Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutolewa Sh.ilingi Bilioni 50 kwa ajili ya mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi unaotekelezwa katika halmashauri nchini.
Halmashauri ya wilaya ya Singida ina jumla ya vijiji 84 kati ya vijiji hivyo vijiji 20 vinapitiwa na Mkuza wa Bomba la Mafuta na Mipango ya Matumizi bora ya ardhi imeandaliwa katika vijiji 16 kati ya 20 na kufanya jumla ya vijiji 50 katika wilaya ya Singisa kuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imeitaka Wizara ya Ardhi kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishajj ardhi kwenye maeneo mbalimbali ili kufikia mwaka 2025 iwe imetimiza malengo na matakwa ya Wizara na kuboresha sekta ya ardhi ili kuiwezesha serikali kuinua uchumi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ikungi Justice Kijazi akisoma taarifa ya mradi wa urasimishaji na umilikishaji wa ardhi kimila alisema takribani hati 5050 za zimemilikishwa kwa wananchi huku wanawake wakimili hati 2030 sawa na asilimia 40.2 lakini imani potofu ya kumnyima mwanamke kumiliki ardhi ikiwa ni moja ya changamoto katika halmashauri hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge alisema kitendo cha kupima na kurasimisha ardhi kinafungua fursa za uwekezaji ndani ya mkoa huo kwa kuwa thamani ya ardhi inaongezeka baada ya kurasimishwa huku Mkurugenzi wa Shirika la Koica kutoka Korea ambalo limefadhili mchakato wa kurasimilisha ardhi kimila kwa Halmashauri ya Ikungi Kyucheol Eo alisema shirika hilo linashirikiana na serikali katika kuleta usawa kati ya mwanamke na mwanaume ikiwemo katika umiliki na matumizi bora ya ardhi.