Mummy Katolila akizungumza na waandishi wa habari kwani niaba ya wenzake kuhusu madai yao ya Sh.bilioni 5 kwa Shirika la Ndege la Fastjet Tanzania baada ya kuachishwa kazi.
****************
Na Mwandishi Wetu
WAFANYAKAZI 105 wa Shirika la Ndege ya Fastjet Tanzania wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuzuia ndege aina ya Embraer 190 (5H-FJH) ya shirika hilo ili waweze kulipwa stahiki zao.
Wafanyakazi hao wamefikia uamuzi huo baada ya kusotea haki zao takribani Sh.bilioni 5 ambazo ni mishahara kuanzia Septemba 2018 hadi Januari 2019 pamoja na michango ya hifadhi ya jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari aliyekuwa Mfanyakazi wa Ndani ya Ndege hiyo, Mummy Katolila alisema baada ya kufukuzwa kazini mwaka 2019 wafanyakazi 105 wakiwakilishwa na mwenzao Alex Mjoge walifungua Kesi iliyopewa jina la CMA/DSM/Ilala 914/19 chini ya Tume ya Usulihosho na Uamuzi (CMA).
Amesema wamesotea haki zao kwa takribani miaka mitatu pamoja na kushinda katika kesi zote ambazo walifungua hivyo wanaomba Rais Samia kuingilia kati, ili mamlaka husika zisimamie waweze kulipwa haki zao.
“Sisi tumeshinda kesi ambayo tulifungua CMA tunadai sh.bilioni 5 kwa Fastjet, ila hawataki kutulipa, mbaya zaidi kuna taarifa kuwa ndege hiyo imefutiwa usajili hivyo inaweza kuondoka na wao kukosa haki zao,” amesema.
Katolila amesema wanamuomba Rais Samia kuelekeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TCAA), kuzuia ndege hiyo ili isiondoke kwenye anga la Tanzania hadi walipwe fedha zao ambazo wamezisotea kwa miaka mingi.
Amesema kesi hiyo iliendeshwa CMA ambapo mwishoni mwa mwaka 2019 hukumu ya zuio hilo ilitoka, ambapo baada ya miezi sita zuio hilo lilifika kikomo, hivyo hawakuweza kuendelea na kesi katika mahakama bali walisiliana na mfilisi ambaye aliteuliwa na mahakama kuu.
Amesema ndege hiyo hadi sasa imeegeshwa kwenye anga la Precions Air, hivyo kuzitaka mamlaka kuchukua hatua haraka..
“Tunamuomba Rais Samia atusaidie kuzuia ndege hiyo kuondoka hapa nchini kwani ndio dhamana iliyobakia, ndege nyingine imeshaondoka, sisi ni watoto wa Kitanzania hatuna pengine pakukimbilia,” alisema.
Aidha, amesema kutokana na sakata hilo, waliona ni vyema kwenda kuifahamisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA- Mkoa wa Ilala) kuhusiana na madai ya kodi (kwa mishahara ya wafanyakazi iliyokwisha lipwa ambapo walichukua hatua na kuitaka TCAA kuzuia ndege husika 5H-FJH kuondoka, hivyo kuwepo kwa taarifa kuwa imefutiwa usajili ni habari ya kuwasikitisha.
“Pamoja na kutolipwa mishahara, pia michango ya mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSSSF na NSSF tangu September 2018 mpaka January 2019 haikupelekwa, jambo ambalo limezidisha ugumu wa maisha,” amesema.
Naye Mfanyakazi Ernest Robert amesema kadhia hiyo ya kuondolewa kazi imesababisha aishi katika maisha magumu kwa miaka mitatu sasa, hivyo anamuomba Rais Samia kuwasaidia kutatua changamoto hiyo.
“Kitendo cha kudaiwa usajili wa ndege hiyo umefutwa kinaacha maswali mengi kwetu naomba Rais aagize vyombo vyake kuchunguza ni nini kilichopo nyuma ya pazia,” amesema.
Akizungumzia sakata hilo Kiongozi wa Kampuni ya Ufilisi Arnold Shirima, amesema ni kweli amepokea maombi ya wafanyakazi hao kuwa wanufaika katika mchakato wa kufilisi shirika hilo, ila hadi sasa bado ufirisi haujafanyika.
Shirima amesema Fastjet inadaiwa na taasisi mbalimbali zaidi Sh.bilioni 46 ambapo TRA inadai zaidi ya Sh. bilioni 16 na kwamba wapo kwenye mchakato wa kuhakisha wadai wote wanalipwa.
“Ni kweli madai hayo ya waliokuwa wafanyakazi wa Fastjet yamefika mezani kwetu tunayafanyia kazi ni imani yangu iwapo mdaiwa akilipa watalipwa, hicho ndicho naweza kusema kwa sasa, niwasihi wawe na subira,” amesema.