Naiba Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bw. Ally Gugu akitoa ufafanuzi kuhusu mkutano wa wadau wa kupata maoni ya rasimu ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 2022 uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.Mshauri Mwelekezi wa rasmu wa Sera Prof. Samweli Wangwe akitoa mada kwa wadau kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzani (TPSF) kuhusu namna wanavyoweza kushiriki kutoa maoni ya rasimu ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 2022Mkurugenzi wa Sera na Utafiti Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Bw. Andrew Maige akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa sekta binafsi katoa maoni ya rasimu ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 2022 Baadhi ya washiriki wa wadau kutoka sekta binafsi wakiwa katika mkutano wa kupata maoni ya rasimu ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 2022 uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
*******************
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema itaendelea kusimamia mabadiliko ya sera, sheria na kanuni zinazosimamia uwekezaji kwa lengo la kuwavutia wawekezaji pamoja kuondokana na urasimu katika utoaji wa vibali vya kufanya kazi na kuidhinisha miradi ya uwekezaji jammbo ambalo litasaidia kutengeneza ajira zisizopungua milioni nane katika kipindi cha mwaka 2020 – 2025.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa wadau kupata maoni ya rasimu ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 2022, Naiba Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bw. Ally Gugu, amesema kuwa serikali imedhamilia kuendeleza juhudi za kuongeza imani kwa wawekezaji ili kuchangia ukuaji wa uchumi.
Bw. Gugu amesema kuwa uundwaji wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Uwekezaji wa mwaka 2022 kwa miaka 10 ijayo (2022- 2023) imedhamiriwa kuchangia kufikia malengo matukufu ya serikali hasa katika utekelezaji wa sera ili kuhamasisha na kuvutia uwekezaji utakaohakikisha ukuaji shirikishi na maendeleo endelevu ya wananchi.
Amesema kuwa mkutano huo umehusisha wadau wa sekta binafsi ambao ni wa kwanza kati ya mikutano mitano iliyoandaliwa kwa lengo la kupata maoni mahususi ya wadau wa sekta ya umma na binafsi kuhusu rasimu ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 2022.
Ameeleza kuwa kutokana na utekelezaji wa mipango ya mikakati mbalimbali ya kuboresha mazingira ya uwekezaji, serikali ilifanikiwa kuanzisha kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC) mwaka 1997 ambapo hadi Desemba 2021 kimefanikiwa kusajili miradi 10,838.
Bw. Gugu amefafanua kuwa miradi hiyo inakadiriwa kuwekeza kiasi cha mtaji wa dola za marekani bilioni 103.05 “Tumeimarisha uratibu na usimamizi wa masuala ya uwekezaji kwa kuanzisha idara maalum ya kuratibu maendeleo ya uwekezaji katika wizara inayosimamia masuala ya uwekezaji ili kuvutia uwekezaji wa ndani na kutoka nje” amesema Bw. Gugu.
Amesema kuwa kuimarishwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kupitia Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na mabaraza ya biashara ya Mikoa na Wizara uliwezesha mikutano ya mashauriano baina ya serikali na wafanyabiashara na wawekezaji katika kuimarishwa kwa jitihada za kubaini na kunadi fursa za uwekezaji kwa ngazi za Mikoa kwa kuandaa miongozo ya uwekezaji ya Mikoa na Wilaya.
Amesema kuwa hivi sasa kila nchi inafanya jitihada za kuvutia wawekezaji kwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji ili kulinda na kukuza chumi zao kwa kuvutia teknoloji, mitaji, fedha za kigeni na kuongeza ajira katika mataifa yao katika kipindi hiki ambacho tumeingia kwenye soko la pamoja la Afrika Mashariki (EAC), Soko la Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za kusini mwa Afrika (SADC) pomoja na soko la eneo la Huru la Biashara Afrika (Africa Continental Free Trade Area – AfCFTA).
“Tunaitaji kuwa na sera madhubuti za kuvutia na kuwezesha uwekezaji katika sekta mbalimbali ili kutumia vilivyo fursa zitokanazo na jumuiya hizi”amesema Bw. Gugu.
Amebainisha kuwa Wizara kwa kuzingatia maoni ya wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi, imeandaa rasimu mpya ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 2022 pamoja na kuanisha malengo mapya ya kitaifa katika kukuza uwekezaji ya mikakati ya kufika malengo hayo.
“Sote tunatambua kuwa sera iliyopo sasa iliandaliwa kabla ya dira ya Taifa ya mwaka 2025 ambayo tunakaribia kufikia hivi karibuni” amesema Bw. Gugu.
Mshauri Mwelekezi wa rasimu wa Sera Prof. Samweli Wangwe, amesema kuwa sera ya mwaka 2022 inawashirikisha wawekezaji ili waweze kutoa mawazo yao jambo ambalo litasaidia kutengeneza mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje nchi.
Prof. Wangwe amesema kuwa Sera ya mwisho ya Uwekezaji ilikuwa mwaka 1996 ambayo imeonekana kuwa na changamoto, hivyo sera ya 2022 kabla ya kuandikwa wadau wa sekta binafsi wamepata fursa ya kutoa maoni ili kuhakikisha inakuwa rafiki kwa wawekezaji.
“Lengo ni kupata mawazo kutoka kwa wewekezaji ili kuhakikisha sera inakuwa rafiki kwa kuzingatia ukuzaji wa kiuchumi na kuchangamsha sekta nyengine” amesema Prof. Wangwe.
Mkurugenzi wa Sera na Utafiti Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzani (TPSF) Bw. Andrew Maige, amesema kuwa sera imara inawasaidia sekta binafsi katika kutekeleza majukumu katika kufanya uwekezaji.
Amesema kuwa miongoni mwa changamoto zilizopo katika sera ya mwaka 1996 ni pamoja namna ya kuratibu mwekezaji anapotaka kuwekeza hapa nchini, kutangaza fursa zilizopo pamoja na kuwezesha uwekezaji katika kuhakikisha mwekezaji anapewa ushirikiano wa kufikia malengo.
Mkutano wa leo umehusisha wadau wa sekta binafsi ambao ni wa kwanza kati ya mikutano mitano iliyoandaliwa kwa lengo la kupata maoni mahususi ya wadau wa sekta ya umma na binafsi kuhusu rasmu ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 2022.
Mikutano mengine imepangwa kufanyika Mkoani Dodoma kuanzia tarehe 21 – 22 Machi 2022, Arusha na Mbeya kuanzia tarehe 24 Machi 2022 pamoja na Mkoa wa Mwanza Machi 28 2022.