Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi), Atupele Mwakibete, akisisitiza jambo kwa Kaimu Meneja wa Bandari za Ziwa Viktoria, Vicent Stephen (katikati) kuhusu mizani ilipo katika bandari ya Mwanza North, jijini Mwanza.
Naibu Waziri wa UJenzi na Uchukuzi (Uchukuzi), Atupele Mwakibete, azungumza na moja ya abiria katika jengo la abiria katika bandari ya bandari ya Mwanza North, wakati alipotembelea bandari ya Mwanza North, jijini Mwanza.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi), Atupele Mwakibete, akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Bandari za Ziwa Viktoria,wakati alipotembelea bandari ya Mwanza North ,jijini Mwanza.Wa kwanza kulia ni Kaimu Meneja wa Bandari za Ziwa Viktoria, Vicent Stephen.
Kaimu Meneja wa Bandari za Ziwa Viktoria Vicent Stephen, akifafanua kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi), Atupele Mwakibete, kuhusu mipaka ya bandari ya Mwanza North, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea bandari hiyo jijini Mwanza.
Kaimu Meneja wa Bandari za Ziwa Viktoria Vicent Stephen, akifafanua kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi), Atupele Mwakibete, kuhusu chelezo kilichopo katikan bandari ya Mwanza South, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea bandari hiyo jijini Mwanza.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi), Atupele Mwakibete, akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Bandari za Ziwa Viktoria,wakati alipotembelea bandari ya Mwanza South ,jijini Mwanza. Wa kwanza kulia ni Kaimu Meneja wa Bandari za Ziwa Viktoria, Vicent Stephen.
PICHA NA WUU
………………………………………………..
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Atupele Mwakibete, ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kukamilisha haraka taratibu za manunuzi ili kuboresha Bandari ya Mwanza North na hatimaye kuruhusu meli kubwa kuweza kushusha na kupakia abiria na mizigo.
Ametoa kauli hiyo jijini Mwanza mara baada ya kutembelea Bandari za North na South na kusisitiza kuwa Meli ya MV Mwanza itakapokamilika itaingia ziwani kuanza kutoka huduma hivyo TPA itatakiwa kuboresha bandari za Mwanza, Kemondo na Bukoba kwa kuongeza kina ili kuruhusu meli hiyo kutoa huduma.
“Ninafahamu kwa miuondombinu iliyopo haiwezi kuruhusu meli kubwa kutoa huduma katika bandari hizi, kamilisheni taratibu zenu ili MV Mwanza ikikamilika iweze kutoa huduma bila kikwazo chochote”, amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu Waziri Mwakibete ameeleza umuhimu wa Idara ya Masoko ya TPA kusukwa upya kwa ajili ya kuzitangaza Bandari za Ziwa Viktoria ili kuweza kupata mzigo na hatimaye kukuza pato la Mamlaka kupitia mizigo inayosafirishwa kwa kutumia bandari hizo kwa nchi zinazozunguka Ziwa Viktoria.
Aidha, Naibu Waziri Mwakibete ameitaka TPA kusimamia miradi inayoendelea kwa kuzingatia thamani ya fedha ili iweze kuwa na matokeo chanya kwa Mamlaka na kwa pato la Taifa.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Bandari za Ziwa Viktoria, Vicent Stephen, amesema Mamlaka iko kwenye hatua mbalimbali za awali za kuboresha Bandari za Mwanza, Kemondo na Bukoba ili kuweza kuhudumia meli kubwa kama ya MV Mwanza.
Kaimu Meneja Stephen ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika bandari za ziwa kwani uwezekezaji huo umeongeza shehena iliyokuwa inahudumiwa kwenye bandari kutoka tani laki 2 na kufikia tani laki 3.
Naibu Waziri Mwakibete yuko Mkoani Mwanza kwa ziara ya siku mbili akikagua miundombinu ya Sekta ya Uchukuzi.