Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Afrika cha Nelson Mandela kimekuja na teknolojia mpya ya kuchuja maji taka kutoka chuoni na kuweza kutumika kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji wa mazao mashambani.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Makamu kiongozi wa kituo cha umahiri cha miundombinu ya maji na nishati endelevu (Wise-Futures) ,Yusufu Abeid wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja na watafiti waliotembelea kituo hicho ikiwa ni sehemu ya mafunzo kwa vitendo baada ya kushiriki mafunzo juu ya kuripoti habari za sayansi na teknolojia iliyoandaliwa na Tume ya Taifa sayansi na teknolojia nchini Tanzania (COSTECH).
Yusufu amesema kuwa,teknolojia hiyo ambayo inaratibiwa na kituo hicho kilichopo chini ya chuo cha sayansi na teknolojia kimekuwa kikitumia teknolojia hiyo ambayo inasaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa maji taka na kuweza kutumika kwenye shughuli zingine ikiwemo ya kilimo cha umwagiliaji kwenye mbogamboga nk.
Amesema kuwa,wamefikia hatua ya kufanya hivyo kwani kituo hicho kimekuwa kikihusika na maswala ya utunzaji wa mazingira ambapo matumizi ya teknolojia hiyo inasaidia sana kuwa na vyoo endelevu kwani majitaka hayo yanatumika kwa ajili ya kumwagilia mboga mboga na hata kutengeneza mabwawa ya samaki.
Amewataka wananchi kuitumia teknolojia hiyo ambayo ni nzuri sana kwa maswala ya kilimo na hata utunzaji wa mazingira na kuweza kujipatia kipato .
“pamoja na utekelezaji wa teknolojia hii tumekuwa na changamoto kwenye swala la manunuzi ambapo imekuwa ikichukua muda kupatikana kwa fedha kwa ajili ya kufanya tafiti kitendo ambacho wameomba kuharakishwa kwa mchakato huyo ili tafiti ziweze kufanyika kwa wakati.”amesema.
Kwa upande wake Msimamizi wa utafiti katika chuo kikuu cha sayansi na teknolojia cha Afrika cha Nelson Mandela ,Profesa Linus Munishi amesema kuwa,chuo hicho kimekuwa kikitoa kozi za uzamili na uzamivu pamoja na kujifunza juu ya maswala ya biashara na ujasiriamali.
Amesema kuwa, wamekuwa wakifanya tafiti katika mswala ya nishati na mazingira,maswala ya viumbe hai,maji,mawasiliano na maswala ya kompyuta .