Meneja Mauzo na Masoko wa SGA Security SGA Bi. Faustina Shoo, (kushoto) na Meneja Usafirishaji Bi. Stella Chiwango – (katikati) wakikabidhi vifaa kwa Afisa Ustawi wa Jamii wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Bw. Justin Chambo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Meneja Usafirishaji wa SGA Security, Stella Chiwango (kulia) akifurahia jambo na Matron wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Bi. Jesca Kawegere (kushoto) baada ya wafanyakazi wa kike wa kampuni hiyo kukabidhi vifaa after SGA female employees handed over medical items to the institute.
Wafanyakazi wa kike wa Kampuni ya SGA Security wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Jijini Dar es Salaam wakati wakikabidhi vifaa kwa taasisi hiyo.
************************
Na Mwandishi wetu, Michuzi TV
WAFANYAKAZI wa kike wa kampuni ya ulinzi ya SGA Security, wamekabidhi vifaa tiba kwa uongozi wa hospitali ya saratani ya Ocean Road, ikiwa ni mchango wa kampuni hiyo katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani inayoadhimishwa Machi 8, kila mwaka.
Wafanyakazi hao wa kike zaidi ya 60, wakiongozwa na Meneja Mauzo na Masoko, Bi Faustina Shoo, walikabidhi viti vya magurudumu kadhaa, mifuko ya colostomy na mafuta maalum (cream) yanayotumiwa na watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) kwa ajili ya watoto wenye ualbino waliolazwa katika taasisi ya Saratani ya Ocean Road iliyoko jijini Dar es Salaam.
“Tuliitumia siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka huu kujumuika kwa pamoja na wagonjwa walioko Ocean Road kwani sote tunajua kwamba wagonjwa wanahitaji upendo, matumaini na huduma zifaazo za matibabu”, alisema Bi Shoo na kuongeza kuwa uamuzi wao pia ulilenga kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema “Tuepuke Upendeleo”.
Kwa upande wake Meneja wa kitengo cha SGA Courier, Bi Stella Chiwango, alisema michango hiyo imelenga kuwasaidia wahitaji haswa ikitiliwa maanani ya kuwa dawa za kuhudumia wenye saratani ni ghali sana ambazo wagonjwa wengi hawawezi kuzimudu gharama hizo, ambazo pia alisema wengine hulazimika kuzifuata dawa hizo Jijini Dar es Salaam, wakitokea maeneo mengine hapa nchini.
Akizungumza na baadhi ya walioshiriki hafla hiyo, Bi Chiwango alisema, “Kama akina mama, dada zetu na mabinti zetu, tumekuja kutoa michango yetu hii ikiwa ni michango yetu ya vifaa vya tiba ikiwa ni mchango wetu kwa kazi nzuri zinazofanywa na uongozi wa hospitali hii”.
Msaada huo wa vifaa tiba ulipokelewa katika hospitali ya Ocean Road na Mlezi wa taasisi hiyo Bi Jesca Kawegere ambaye aliishukuru kampuni hiyo maarufu ya ulinzi kwa kuwafikiria wagonjwa wanaopata huduma hospitalini hapo, amapo alisema kuwa viti vya magurudumu vitarahisisha huduma zinazotolewa kwa wagonjwa wa saratani waliolazwa katika hospitali hiyo.
“Ugonjwa wa Saratani una athari kubwa ndani ya jamii, tunashukuru sana uongozi wa kampuni ya ulinzi ya SGA Security kwa mchango huu mkubwa ambao utatusaidia kukabiliana na changamoto tunazokabiliana nazo katika kuhudumia wagonjwa kwenye taasisi hii”, alisema Bi Kawegere.
SGA Security, kampuni ya kwanza ya ulinzi binafsi kufanya kazi nchini Tanzania, imeendelea kutoa fursa sawa za ajira, ambapo wanawake na watu wenye kuishi na ulemavu huwa wanahimizwa kutuma maombi yao ya ajira.
Mkurugenzi Mkuu wa SGA, Bw Eric Sambu, alisema kuwa SGA inajivunia fursa sawa katika kuajiri wafanyakazi wake bila kujali jinsia, kabila, rangi, dini, utaifa, umri, hali ya ndoa, ulemavu au swala linguine lolote.
“Tuna asilimia 40 ya wanawake walioajiriwa katika ngazi ya Menejimenti ya SGA ambao naweza kusema wamefanya vyema kazi zao na wamechangia ukuaji wa biashara yetu hapa Tanzania”, Bw Sambu aliongeza.
SGA ina programu ya kuwashauri wanawake kwa ajili ya majukumu ya usimamizi na kwamba hivi karibuni uongozi wa kampuni hiyo uliandaa mafunzo ya ngazi ya juu ya uongozi.
“Kusema ukweli, wanawake wa SGA wameonyesha umahiri katika Nyanja za uongozi ikiwemo katika majukumu muhimu, ambapo wametoa michango chanya katika ukuaji wa kampuni,; tunajivunia sana uchapakazi wao, na tunawahimiza wanawake waliohitimu kuendelea kukumbatia fursa zinazojitokeza”, alishauri Bw. Sambu.
Akitoa shukrani kwa niaba ya taasisi hiyo Ofisa Ustawi wa Jamii wa taasisi ya Ocean Road, Justin Chambo, ameishukuru kampuni ya SGA hususan wafanyakazi wa kike wa kampuni hiyo kwa michango yao hiyo ambayo amesema itatoa mchango mkubwa sana katika kuwahudumia wagonjwa ambapo pia alitoa elimu kuhusu umuhimu wa watu kufanya uchunguzi kuhusu ugonjwa wa saratani ambao ni bure.
Pia aliwaeleza wafanyakazi hao ya kuwa taasisi ya Ocean Road ndicho kituo pekee cha afya maalumu na kongwe zaidi kwa matibabu ya saratani nchini Tanzania.
Alisema kuwa Ocean Road inatoa huduma nyingi za tiba ambazo alisema ni pamoja na huduma za maabara, picha za uchunguzi, huduma ya tiba ya chemotherapy, radiotherapy, huduma za uponyaji pamoja na uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi.
Aidha aliendelea kusema kuwa kampuni ya SGA imeendelea na programu zake za uwajibikaji kwa jamii kwa michango kwa ajili ya jamii inakofanyia kazi, ikiwemo kufadhili matukio mengi ya mbio za marathoni, uchangiaji damu, usafi wa mazingira, huduma za kukabiliana na dharura, ambapo alisema huduma nyingine ni zile za magari ya wagonjwa, kukabiliana na majanga ya moto, pamoja na kusaidiana na jeshi la polisi katika kuhakikisha kuna kuwa na usalama.
Hivi majuzi kampuni ya SGA ilishinda tuzo ya juu katika Utendaji wa Maudhui ya Ndani kwa shughuli za Madini kwa mwaka wa 2021, ambapo miongoni mwa sifa nyingine, ni pamoja na pongezi kutoka kwa uongozi wa jeshi la polisi kwa kuzingatia viwango vya juu wakati wa kutoa ajira zake. SGA ndiyo kampuni pekee hapa nchini iliyoidhinishwa kuwa na ubora unaotambuliwa na taasisi ya kimataifa ya kiusalama ISO 18788.