Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani, Dkt..Harrison Chuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Semina fupi kwa waandishi wa habari kuhusu ugonjwa wa saratani na utekelezaji wa mradi wa TCCP iliyofanyika leo tarehe 17/03/2022 Jijini Dar es Salaam Mtaalamu wa Masuala ya Saratani kutoka katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt.Carolyine Swai akiwasilisha mada katika Semina fupi kwa waandishi wa habari kuhusu ugonjwa wa saratani na utekelezaji wa mradi wa TCCP iliofanyika leo Jijini Dar es salaam Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani, Dkt..Harrison Chuwa akipata picha ya pamoja na waandishi wa habari katika Semina fupi kwa waandishi wa habari kuhusu ugonjwa wa saratani na utekelezaji wa mradi wa TCCP iliyofanyika leo tarehe 17/03/2022 Jijini Dar es Salaam.
*********
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika mradi mtambuka wa Saratani (TCCP) ni pamoja na kufunga mashine ya ultrasound ya kisasa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road yenye thamani ya Sh. milioni 150 ambayo itahudumia wagonjwa takribani 50 hadi 80 kwa siku.
Ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani, Bw.Harrison Chuwa katika Semina fupi kwa waandishi wa habari kuhusu ugonjwa wa saratani na utekelezaji wa mradi wa TCCP.
Amesema kupitia Mradi Mtambuka wa Saratani (TCCP) wanatarajia kujenga hospitali ya saratani yenye mashine mbili za kisasa za mionzi ya nje (Linacs) na mashine moja mionzi ya ndani (Brachytherapy) katika Hospitali ya Aga khan Dar es Salaam ambapo ujenzi huo utaanza mwezi Aprili 2022.
“Kupitia mradi wa TCCP tunatarajia kufunga mashine za kuweza kutoa matibabu ya mionzi ya ndani katika koromeo la mlo (Intraluminal brachytherapy) katika Taasisi ya Saratani Ocean Road na Huduma hii itakuwa ni ya kwanza kupatikana Afrika Mshariki na Kati,”. Amesema Dkt.Chuwa.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Masuala ya Saratani kutoka katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt.Carolyine Swai amesema utumiaji wa tumbaku na pombe kupita kiasi huchangia kwa kiasi kikubwa katika maambukizi ya magonjwa ya saratani.
Amesema ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi umekuwa ukitokea kwa mara nyingi kwa wanawake kuliko kwa wanaume na pia huambukizwa kwa wingi kupitia ngono zembe.