**********************
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imesema itashirikiana na Kamati ya Kitaifa ya Udhibiti na Kuzuia Mauji ya Kimbari (TNCPG), ili kuhakikisha migogoro na matukio yoyote ambayo yanaweza kusababisha amani ya nchi kupotea yanaepukika.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Sheria na Katiba, George Simbachawene wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Waziri Simbachawene amesema kamati hiyo hadi sasa imekuwa ikitatua migogoro ya ndani ya nchi nan je pale inapohitajika jambo ambalo linachangia nchi kuwa salama.
Amesema kamati hiyo ambayo inaundwa na wadau kutoka katika vyombo mbalimbali vya Serikali na sekta binafsi, imekuwa na mchango mkubwa katika kudumisha amani.
“TNCPG imekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia amani yetu kuwa endelevu, sisi kama Serikali tutawaunga mkono kwa kila njia, hivyo basi naomba wananchi waendelee kuiunga mkono,” amesema.
Simbachawene amesema kamati hiyo imefanikiwa kutatua mgogoro wa kulima na wafugaji wilayani Kiteto mkoani Manyara na kwingine.
Amesema katika kuhakikisha kamati hiyo inafanya kazi kwenye mazingira rafiki Shirika la Mpango wa Maendeleo Duniani (UNDP), linarajia kuiwezesha kamati kuwa ofisi rasmi ambayo itawezesha uratibu wa shughuli za kila siku.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula amesema kamati hiyo ni chombo muhimu katika kuchochea maendeleo na uchumi ndani na nje ya nchi.
Balozi Mulamula amesema kamati hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2011 imeshiriki kutatua mgogoro uliotokea Mtwara katika sakata la gesi.
“Mimi nimekuwa kama mlezi tangu kipindi kile nikiwa Katibu wa Maziwa Makuu, natambua faida yake, hivyo sisi tutaiunga mkono kuhakikisha inaendelea kujenga amani na mshikamano nchini nan je ya nchi,” amesema.
Amesema wataisadia kamati hiyo kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuijua na kuitumia kwenye kutatua migogoro ya ndani na nje.
Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Christine Musisi amesema wao wamejipanga kushirikiana na kamati hiyo kutokana na ukweli kuwa inachosimamia kina maslahi kwa dunia.
Musisi amesema amani ndio msingi mkubwa kwa maendeleo ya nchi na jamii, hivyo watasaidia kila kinachowezekana kuhakikisha dunia inakuwa salama.
“Msingi wa maendeleo dunia umejikita katika amani, haki na mshikamano, hivyo UNDP haina budi kuungana na kila mdau ambaye anasimamia eneo hilo,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa TNCPG, Felister Mushi amesema wamejipanga kushirikiana na wadau wote ambao wanapigania amani nchini na duniani, kwa maslahi mapana ya wananchi na nchi.
Amesema kamati yao imekuwa ikipata ushirikiano mzuri kwa Serikali, hali ambayo inawarahisishia kutekeleza majukumu yao.