Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Bw. Sebastian Masanja, akifungua kikao cha siku mbili kati ya OSHA na wadau wa sekta mbalimbali wa Mkoa wa Tanga kilicholenga kujadili changamoto mbalimbali za utekelezaji wa Sheria Na 5 ya Usalama na Afya ya Mwaka 2003 pamoja na ufumbuzi wa changamoto hizo.
Mkurugenzi wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi wa OSHA, Bw. Alexander Ngata, akizungumza na wadau wa sekta mbalimbali wa Mkoa wa Tanga wakati wa kikao na wadau hao kilicholenga kukuza uelewa juu ya utekelezaji wa Sheria Na 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya Mwaka 2003.
Kaimu Mkuu Kitengo cha Sheria wa OSHA, Bi Netiwe Mhando, akitoa elimu kwa wadau kutoka sekta mbalimbali wa Mkoa wa Tanga juu ya umuhimu wa utekelezaji wa Sheria Na 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya Mwaka 2003 wakati wa kikao kati ya OSHA na wadau hao.
Mdau kutoka sekta ya hoteli akiwasilisha changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wafanya biashara hao katika utekelezaji wa Sheria Na.5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya Mwaka 2003, ambapo changamoto hizo zilitolewa majibu na jopo la viongozi kutoka OSHA.
Meneja wa Afya wa OSHA, Bw. Jerome Materu, akitoa ufafanuzi juu ya umuhimu wa upimaji afya kwa wafanyakazi katika hatua zote tatu muhimu yaani kabla ya ajira, wakati wa ajira na baada ya ajira kwa wadau wa sekta mbalimbali wa mkoa wa tanga.
***************************
Na Mwandishi Wetu
Wadau wa sekta ya utalii na hoteli mkoani Tanga wametakiwa kuzingatia viwango vya usalama na afya mahali pa kazi ikiwa ni mkakati mojawapo wa kujiandaa kunufaika na fursa mbali mbali za kiuchumi ukiwemo mradi mkubwa wa bomba la mafuta la Hoima-Tanga.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima katika ujumbe wake uliofikishwa kwa wadau hao kwa niaba yake na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Bw. Sebastian Masanja wakati akifungua kikao baina ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na wadau hao.
“Nitumie fursa hii kuwaeleza kwamba nyinyi kama wadau wa sekta ya utalii na hoteli mna mchango mkubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu kwani sekta hii inashika nafasi ya pili baada ya sekta ya uzalishaji hivyo pamoja na umuhimu huo nilioueleza nitumie nafasi hii kuwasihi kuzingatia taratibu muhimu za afya na usalama mahali pa kazi,” ameeleza mwakilishi huyo wa Mkuu wa Mkoa.
Aliongeza: “Nadhani mmeshuhudia jitihada zinazofanywa na serikali ili kuinua sekta ya utalii iliyokuwa imeyumba kidogo kutokana na athari za janga la uviko-19. Jitahadi hizo zinaongozwa na Rais wetu mpendwa, Samia Suluhu Hassan ambaye aliweza hata kushiriki katika filamu ya The Royal Tour yenye lengo la kutangaza vivutio vyetu vya utalii. Lakini pia amekuwa akifanya jitahadi nyingine nyingi za kuwavutia wawekezaji na hivyo kuzalisha fursa nyingi za kiuchumi ambazo endapo hatutaweza kufanya biashara zetu kwa kuzingatia sheria za nchi na viwango vya kimataifa ikiwemo masuala ya afya na usalama mahali pa kazi fursa hizi zitatupitia mbali.”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usalama na Afya wa OSHA, Alexander Ngata, ambaye alimwakilisha Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema kikao hicho ni cha mashauriano na kuwataka washiriki kufuatilia kwa makini mada zilizoandaliwa pamoja na kueleza changamoto zinazowakumba katika utekelezaji wa masuala ya usalama na afya katika sehemu zao za kazi.
“Tumekuwa tukizungumza na baadhi ya wadau wa hapa Tanga lakini bado tunaona kama kuna vizingiti katika utekelezaji wa sheria ya Usalama na Afya mahali pa kazi hivyo tumeona ni vyema tukazungumza na wafanya biashara wote wa Tanga ili tuweze kueleweshana na kutatua changamoto zilizopo na hivyo kuwezesha biashara zenu kukua na kupata sifa za kushiriki katika fursa kubwa za kiuchumi ambazo miongoni mwa masharti yake muhimu ni kukidhi viwango mbali mbali yakiwemo masuala ya usalama na afya mahali pa kazi,” amesema Mkurugenzi Ngata.
Baadhi ya wadau walioshiriki kikao hicho wameeleza kuridhishwa na kikao hicho ambapo wameonesha matumaini makubwa kwamba maazimio yaliyowekwa yatatekelezwa.
“Kupitia kikao hiki tumepata fursa ya kujifunza na kujijenga zaidi hususan katika mambo tuliyokuwa hatuyafahamu jambo lilikuwa linapelekea kukwepa kuyatekeleza lakini tunaamini kwamba baada ya hapa tutakwenda kushirikiana vyema na OSHA,” amesema James Maurice, mmoja wa washiriki wa kikao.
Mshiriki mwingine ambaye alijitambulisha kwa jina la Fatma Jokho amesema: “Tunashukuru kikao kimeenda vizuri, tumeweza kutoa maoni na kueleza changamoto zetu mbali mbali na tumetoa mapendekezo yetu ambayo tunaimani kwamba OSHA watayafanyia kazi.”
Kikao hicho kilichofanyika kwa siku mbili kimewahusisha wadau wa sekta za utalii na hoteli ,usafirishaji, ujenzi, viwanda vidogo vidogo na madini ambapo mada mada mbali mbali zimewasilishwa na kujadiliwa ikiwemo dhana nzima ya Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi, Huduma za Ukaguzi mahali pa kazi pamoja na Upimaji Afya kwa wafanyakazi.
Miongoni mwa majukumu makuu ya OSHA ni kukuza uelewa wa masuala ya Usalama na Afya miongoni mwa wadau na wananchi kwa ujumla ambapo kikao hiki imekuwa ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu hilo. Majukumu mengine ni pamoja na; Kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi, Kufanya tafiti kuhusiana na masuala husika pamoja na kuishauri serikali kuhusiana na masuala ya Usalama na Afya ikiwemo uridhiaji wa mikataba ya Kimataifa.
Mwisho………………………..